WATU wengi husema kwamba mnyama huyu ana sura nzuri; hata hivyo wengine husema kwamba ana sura ya ajabu. Ana miguu myembamba, manyoya laini, na macho makubwa yanayong’aa. Pia, ana urefu wa sentimita 12.5 na uzito wa gramu 114. Ni mnyama gani huyo? Anaitwa tarsier!

Acheni tumchunguze tarsier wa Ufilipino. Kwa sababu ana mwili mdogo sana—macho yake, masikio, mikono, miguu na mkia huonekana mikubwa sana. Hata hivyo, tukimchunguza kwa makini tutagundua jinsi alivyoumbwa kwa njia ya pekee sana.

UWEZO WA KUSIKIA: Masikio yake membamba kama karatasi yanaweza kujikunja na kujikunjua, na hata kunasa sauti ndogo kabisa. Uwezo huo wa kusikia humsaidia aepuke wanyama hatari na kujua mawindo yake yalipo. Usiku, masikio ya mnyama huyu yanamwezesha kusikia milio ya nyenje, mchwa, mbawakawa, ndege, na vyura. Anaposikia mlio wa windo lake yeye huelekeza kichwa mahali hapo akiwa amekodoa macho yake makubwa.

UWEZO WA KUSHIKA: Mikono ya tarsier ina uwezo wa pekee wa kushika matawi membamba. Ncha za vidole vyake zina miinuko kama ile ya gurudumu la gari inayomsaidia kukamata vizuri. Hata anapokuwa amelala, mnyama huyu anahitaji kujishikilia kwa nguvu. Miinuko iliyo kwenye sehemu ya chini ya mkia wake mrefu humsaidia asianguke anapokuwa amelala.

 UWEZO WA KUONA: Hakuna mnyama mwingine mwenye mwili mdogo na macho makubwa kama mnyama huyu. Isitoshe, jicho lake moja tu ni kubwa kuliko ubongo wake! Macho yake hayazunguki; sikuzote hutazama mbele tu. Je, hilo ni tatizo? Hapana. Kwa sababu mnyama huyo anaweza kugeuza shingo yake pande zote kufikia nyuzi 180.

WEPESI: Miguu mirefu ya tarsier inaweza kumsaidia kuruka kufikia umbali wa mita 6. Umbali huo ni zaidi ya mara 40 ya mwili wake! Mnyama huyu mdogo huwinda usiku akitumia vidole vyake kukamata mawindo yake bila kukosea.

Wanyama hawa hawawezi kuishi muda mrefu wakiwa wamefungiwa, kwa sababu wanapenda sana kula wadudu walio hai na pia hawapendi kuguswa. Licha ya hilo, mnyama huyu wa ajabu huwavutia sana watu wa Ufilipino. Karibu kila sehemu ya mwili wa mnyama huyu wa msituni inastaajabisha kwelikweli!