Profesa Stephen Taylor anafundisha na kufanya utafiti katika Chuo Kikuu cha Teknolojia kilichoko Sydney, nchini Australia. Anafanya utafiti kuhusu masoko ya hisa na jinsi yanavyoweza kusimamiwa vizuri. Mwandishi wa Amkeni! alimhoji kuhusu jinsi kazi yake ya utafiti ilivyobadili maoni yake kuhusu imani ya kidini.

Tuambie kuhusu malezi yako.

Wazazi wangu walipenda kwenda kanisani na walikuwa wanyoofu na wachapa-kazi. Walinitia moyo nipate elimu nzuri, kwa hiyo nikajifunza masomo ya biashara katika Chuo Kikuu cha New South Wales. Niligundua kwamba nilipenda sana kufanya utafiti na hivyo nikaamua kuwa mtafiti.

Unafanya utafiti kuhusu mambo gani?

Nilitaka hasa kujua jinsi masoko ya hisa yanavyofanya kazi. * Katika masoko ya hisa watu hununua na kuuza hisa za makampuni na kutumia faida wanayopata kuendesha biashara zao. Pia, ninafanya utafiti kuhusu mambo yanayoathiri bei za hisa.

Je, unaweza kutoa mfano?

Kampuni hutarajiwa kutoa ripoti ya mapato kwa ukawaida. Wawekezaji hutegemea ripoti hizo ili kujua hali ya uchumi ya kampuni. Hata hivyo, baadhi ya mbinu zinazotumiwa na kampuni hizo kutoa ripoti si sahihi. Wachambuzi husema kwamba mbinu hizo husababisha kampuni kuficha taarifa muhimu kuhusu mapato na thamani halisi ya kampuni. Wawekezaji wanawezaje kupata ripoti sahihi na iliyo kamili? Wasimamizi wa masoko ya hisa wanahitaji taarifa zipi ili wahakikishe masoko hayo yanasimamiwa vizuri? Mimi na watafiti wenzangu tunaendelea kutafuta majibu ya maswali hayo.

 Tuambie kuhusu historia ya imani yako ya kidini.

Nilipokuwa mtoto niliandamana na wazazi wangu walipokuwa wakienda kwenye Kanisa la Presbiteri, lakini niliacha mambo ya dini nilipobalehe. Nilimwamini Mungu na kuiheshimu Biblia lakini niliona kwamba dini haiwezi kusuluhisha matatizo ya maisha. Niliona vikundi mbalimbali vya kidini kama tu sehemu ambazo marafiki hukutana. Nilipokuwa Ulaya, nilitembelea makanisa kadhaa makubwa na nilishangaa kuona jinsi yalivyokuwa na utajiri mwingi huku watu wengi ulimwenguni wakiwa maskini. Nilihangaishwa sana na hali hiyo na nikakosa imani katika dini.

Ni nini kilichobadili mtazamo wako?

Mke wangu, Jennifer, alianza kujifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova na pia alihudhuria mikutano yao. Hivyo, niliandamana naye kwenye mikutano yao ili nijionee jinsi wanavyosali. Punde si punde nilitambua kwamba sikujua lolote kuhusu Biblia. Nilishtuka sana! Kwa hiyo nikaanza kujifunza Biblia na Mashahidi.

Njia waliyotumia kunifundisha Biblia ilinifurahisha sana. Waliuliza maswali, wakachunguza na kutoa uthibitisho kuhusu jambo fulani, na kisha kupata ukweli wa jambo hilo na hizo ndizo mbinu nilizokuwa nikitumia katika kazi yangu nikiwa mtafiti! Mwaka wa 1999, miaka michache baada ya Jennifer kubatizwa, mimi pia nilibatizwa na kuwa Shahidi wa Yehova.

Je, ujuzi wako kuhusu mambo ya uchumi umekusaidia kuitumaini Biblia?

Ndiyo. Kwa mfano, Sheria ambayo Waisraeli wa kale walipewa na Mungu ilizungumzia pia mambo ya uchumi ambayo bado wataalamu wa uchumi leo wanajitahidi kusuluhisha. Sheria hiyo iliwaagiza Waisraeli watenge kiasi fulani cha mazao yao kwa ajili ya maskini (aina fulani ya kodi au bima), kuwapatia maskini mikopo bila kuwatoza riba (kuwawezesha kupata mikopo), na kurudisha mashamba ya urithi kwa wale walioyamiliki kila baada ya miaka 50 (kulinda haki za umiliki wa mali). (Mambo ya Walawi 19:9, 10; 25:10, 35-37; Kumbukumbu la Torati 24:19-21) Maandalizi haya na mengine yaliwasaidia watu katika njia tatu kuu zifuatazo: (1) yaliwasaidia walipokuwa na matatizo ya kiuchumi, (2) yalipunguza umaskini, na (3) yaliwasaidia kupunguza tofauti baina ya maskini na matajiri—na yote hayo yalitendeka zaidi ya miaka 3,000 kabla wanadamu hawajaanza kusomea mambo ya uchumi!

Pia, Biblia inawatia moyo watu kuwa na mitazamo na tabia zinazowasaidia kuwa na usalama wa kifedha. Kwa mfano, inawafundisha watu kuwa wanyoofu, wakarimu, wenye huruma na wenye kutegemeka. (Kumbukumbu la Torati 15:7-11; 25:15; Zaburi 15) Jambo la kupendeza ni kwamba baada ya msukosuko wa kiuchumi uliotokea hivi karibuni kote ulimwenguni, shule fulani zinazofundisha masomo ya biashara na mashirika ya kibiashara yalianza kuwasihi wataalamu wa uchumi na wa biashara wafuate maadili na viwango vya juu katika mambo ya uchumi. Naona kwamba viwango vya Biblia vya maadili, ni bora sana kuliko viwango vya kibiashara.

Imani yako imekusaidiaje?

Kujifunza Biblia ndiyo “akiba” bora zaidi niliyowahi kujiwekea

Kwa kweli, mke wangu Jennifer huniambia kwamba nimekuwa mwenye usawaziko zaidi! Kabla ya hapo sikutaka kukosea hata kidogo na nilikuwa mshupavu. Huenda hiyo ndiyo sababu nilifaulu katika uhasibu. Bila shaka, kufuata kanuni za Biblia kumenisaidia kuwa mwenye usawaziko zaidi. Kwa sasa mimi na familia yangu tuna furaha zaidi kuliko mwanzoni. Pia tunafurahia kuwafundisha wengine hekima ya Biblia. Kujifunza Biblia ndiyo “akiba” bora zaidi niliyowahi kujiwekea.

^ fu. 7 Pia huitwa masoko ya mtaji.