Israel, Jordan, na Palestina

Maji ya Bahari ya Chumvi yanazidi kupungua kwa kiwango cha karibu mita moja kwa mwaka. Baadhi ya watu wanahofia kwamba huenda maji hayo yakakauka kabisa kufikia mwaka wa 2050. Wataalamu wanatafuta suluhisho la tatizo hilo. Mbinu moja wanayofikiria ni kuyachuja maji yenye chumvi ya Bahari Nyekundu kwa ajili ya matumizi ya wanadamu na kisha kuyaelekeza kwenye Bahari ya Chumvi maji yenye chumvi yanayobaki. Watu wengine wanasema kwamba kufanya hivyo kutaharibu mazingira ya Bahari ya Chumvi.

Ujerumani

Uchunguzi mmoja uliofanywa na kampuni fulani ya bima unasema kwamba siku ya Krismasi huwa na ongezeko la karibu asilimia thelathini ya watu wanaolazwa hospitalini kwa sababu ya mshtuko wa moyo kuliko siku nyingine yoyote ya mwaka. Kampuni hiyo inasema kwamba chanzo kikuu cha hali hiyo ni mkazo unatokana na kutafuta zawadi za Krismasi na pia matarajio makubwa ya familia na marafiki.

Uingereza

Wanasayansi nchini Uingereza wametangaza kwamba yule konokono aliyepatikana nchini Iceland alikuwa na umri wa miaka 507 alipokufa mwaka wa 2006 na si miaka 405 kama ilivyodhaniwa. Huyo ndiye mnyama aliyeishi muda mrefu zaidi * katika historia. Konokono huyo alikufa wanasayansi walipomgandisha ili wampeleke kwenye maabara.

Amerika ya Latini na Karibea

Katika mkutano uliofanyika Havana, nchini Kuba, mapema mwaka huu, mataifa 33 yaliyopo Amerika ya Latini na Karibea yametangaza nchi zao kuwa ‘ukanda wa amani’ kwa kufikia makubaliano ya kutatua migogoro yao bila kutumia nguvu za kijeshi. Miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon.

^ fu. 7 Tunaposema “mnyama aliyeishi muda mrefu zaidi” katika kisa hiki, jambo hilo halitii ndani vitu vilivyo hai kama vile matumbawe ambayo yanasemekana yamekuwepo kwa maelfu ya miaka.