Marekani

Baadhi ya polisi wanatumia teknolojia ili kupunguza hatari wanapofuatilia magari. Njia moja inayojaribiwa ni magari ya polisi kuwekwa mfumo wa kurusha Vifaa vya Kupokea Habari Kutoka Kwenye Satelaiti (GPS). Mfumo huo hurusha vifaa hivyo ambavyo hunata kwenye gari wanalofuatilia. Hivyo, washukiwa wanaweza kufuatwa kwa mwendo salama.

India

Imekadiriwa kwamba kila saa, mwanamke huuawa kwa sababu ya ugomvi kuhusu mahari. Ingawa desturi ya kutoa na kupokea malipo hayo imepigwa marufuku, mwaka wa 2012 zaidi ya wanawake 8,200 waliuawa kwa sababu bwana-arusi au watu wa familia yake hawakutosheka na mahari iliyotolewa na bibi-arusi.

Uswisi

Vifaa vidogo vya setilaiti vilivyofungwa kwenye mbayuwayu watatu walipokuwa kwenye eneo wanalotagia mayai, vilionyesha kwamba ndege hao walisafiri angani bila kutua kwa zaidi ya siku 200 walipokuwa wakihamia Afrika. Awali uwezo kama huo wa kusafiri kwa muda mrefu ulihusianishwa tu na wanyama wa baharini.

Pembe ya Afrika

Maharamia waliteka nyara meli 179 katika pwani ya Pembe ya Afrika kati ya Aprili 2005 na Desemba 2012. Benki ya Dunia inakadiria kwamba wahalifu hao walilipwa jumla ya dola milioni 413 za Marekani kama fidia.