WANASAYANSI wanajitahidi kuboresha uwezo wa vyombo vinavyofyonza mwangaza wa jua ili kupunguza matumizi ya mafuta yanayochimbwa ardhini. Mwanasayansi mmoja alisema hivi: “Suluhisho la tatizo hilo limekuwepo ingawa halijatumika.”

Magamba yaliyo kwenye bawa la kipepeo yana mashimo yanayofanana na sega la asali

Fikiria hili: Ili wapate joto msimu wa baridi, vipepeo hutandaza mabawa yao juani. Mabawa ya vipepeo wanaoitwa swallowtail yana uwezo mkubwa wa kufyonza na kuhifadhi mwangaza wa jua. Hilo linawezekana kwa sababu rangi ya asili ya vipepeo hao ni nyeusi na pia wana magamba madogo sana yaliyolaliana juu ya mabawa. Magamba hayo yana mistari ya mashimo yanayofanana na sega la asali ambayo yametenganishwa na miinuko yenye umbo la V inayoingiza mwanga ndani ya mashimo hayo. Muundo huo wa kipekee unaofyonza mwangaza wa jua hufanya mabawa yawe meusi na kupasha kipepeo joto vizuri.

Gazeti la Science Daily linasema: “Mabawa ya kipepeo ni kati ya vitu laini sana ulimwenguni, hata hivyo, yamewachochea watafiti kuvumbua teknolojia mpya inayozalisha maradufu gesi ya hidrojeni—ambayo haichafui mazingira—kwa kutumia maji na mwangaza wa jua.” Huenda mbinu hiyo ikatumika pia kutengeneza darubini na miwani na pia mitambo inayofyonza mwangaza wa jua.

Una maoni gani? Je, uwezo wa pekee wa bawa la kipepeo wa kufyonza mwangaza ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?