Marekani

Mwaka wa 2012, asilimia 14.5 ya familia nchini Marekani, yaani, watu milioni 49, “hawakuwa na hakika kama wangepata, au walishindwa kupata, chakula cha kutosha wote katika familia zao” wakati fulani katika mwaka huo, kulingana na takwimu za Wizara ya Kilimo.

Hispania

Uchunguzi uliofanyiwa wanafunzi wa chuo kikuu ulionyesha kwamba asilimia 56 ya wanawake na asilimia 41 ya wanaume walikiri wanakunywa pombe kupita kiasi, yaani, kulingana na uchunguzi huo, wanakunywa angalau chupa nane (kwa wanaume) au sita (kwa wanawake) katika kipindi kimoja.

Bahari ya Pasifiki

Wanasayansi waliochukua mchanga uliokuwa mita 11,000 ndani ya bahari katika Bonde la Mariana walipata bakteria na vijidudu vingine vikiwa hai—licha ya eneo hilo kuwa na giza kabisa, shinikizo kubwa, na baridi kali sana. Awali, ilidhaniwa kwamba haingewezekana kupata uhai katika eneo kama hilo.

Muungano wa Falme za Kiarabu

Katika jitihada za kukabiliana na kunenepa kupita kiasi, hivi karibuni wenye mamlaka huko Dubai walitoa zawadi ya gramu moja ya dhahabu, ambayo wakati huo ilikuwa na thamani ya karibu dola 45 za Marekani, kwa kila kilo moja ambayo mtu alipunguza. Ili kupokea dhahabu hiyo, watu walipaswa kujiandikisha kisha wapunguze angalau kilo mbili katika mwezi wa Ramadhani.