Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

Amkeni!  |  Julai 2014

 JE, NI KAZI YA UBUNI?

Mfumo wa Uzazi wa Chura Anayeangua Tumboni

Mfumo wa Uzazi wa Chura Anayeangua Tumboni

CHURA anayeangua tumboni aliyepatikana Australia, ambaye inaaminika alitoweka mwaka wa 2002 alikuwa na mfumo wa ajabu wa uzazi. Chura wa kike alimeza mayai yake na kuatamia watoto wake tumboni kwa majuma sita hivi. Baadaye watoto wake walitokea mdomoni wakiwa vyura waliokomaa.

Ili asimeng’enye mayai yake, ilikuwa lazima chura huyo asile na pia aache kutokeza asidi tumboni. Inaonekana kwamba kemikali zilizotokezwa na mayai na vyura wadogo zilizuia kutokezwa kwa asidi hiyo.

Mama huyo aliangua mayai 24 hivi. Kufikia wakati wa kuzaa, vyura wadogo walifanyiza asilimia 40 hivi ya uzani wake. Yaani, ni kama mwanamke mwenye uzito wa kilo 68 kupata mimba ya watoto 24 wenye uzito wa kilo 1.8 kila mmoja! Vyura hao wadogo walipanua tumbo la mama yao sana hivi kwamba waliziba mapafu yake na kumlazimu apumue kupitia ngozi yake.

Vyura wadogo walitokea kwa kipindi cha siku kadhaa kulingana na jinsi walivyokuwa wamekomaa. Mama huyo alipohisi hatari, aliangua kwa kuwatapika vyura wadogo. Pindi moja, watafiti walimwona chura akiwatapika vyura wadogo sita kwa pamoja na kuwarusha hewani umbali wa mita 1 hivi.

Ikiwa, mfumo wa uzazi wa chura huyo ulijitokeza wenyewe, kama wengine wanavyodai, basi angehitaji kufanya mabadiliko makubwa katika umbo na tabia yake mara moja. Mwanasayansi anayeamini mageuzi Michael J. Tyler aliandika hivi: “Haiwezekani kwamba angebadili mfumo wake wa uzazi hatua kwa hatua. Mfumo huo hauwezi kamwe kubadilika hatua kwa hatua.” Kulingana na Tyler, ufafanuzi pekee unaoweza kueleweka ni “tukio moja kubwa.” Watu wengi wanaamini tukio hilo kubwa ni uumbaji. *

Una maoni gani? Je, mfumo wa uzazi wa chura anayeangua tumboni ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?

^ fu. 7 Katika kitabu chake Origin of Species, Charles Darwin aliandika: “Uteuzi wa kiasili hutokea kupitia mabadiliko madogo; hauwezi kutokea kupitia mabadiliko makubwa.”