Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

Amkeni!  |  Mei 2014

 MAHOJIANO | GUILLERMO PEREZ

Daktari wa Upasuaji Anaeleza Kwa Nini Anamwamini Mungu

Daktari wa Upasuaji Anaeleza Kwa Nini Anamwamini Mungu

Dakt. Guillermo Perez aliyekuwa mkuu wa upasuaji katika hospitali inayohudumia wagonjwa 700 wa kulazwa nchini Afrika Kusini, alistaafu hivi karibuni. Kwa miaka mingi aliamini fundisho la mageuzi. Lakini baadaye alisadikishwa kwamba mwili wa mwanadamu ulibuniwa na Mungu. Mwandishi wa Amkeni! alimwuliza kuhusu imani yake.

Tafadhali tueleze, kwa nini uliamini nadharia ya mageuzi?

Ingawa nililelewa katika dini ya Katoliki, nilikuwa na shaka kuhusu Mungu. Kwa mfano, sikuamini kwamba Mungu huchoma watu katika moto wa mateso. Hivyo, maprofesa wa chuo kikuu waliponifundisha kwamba viumbe hai vilitokana na mageuzi na kwamba havikuumbwa na Mungu, nilikubali maoni hayo, nikidhani lilikuwa jambo hakika. Kanisa langu pia halikupinga mageuzi bali lilifundisha kwamba yaliongozwa na Mungu.

Ni nini kilichofanya uvutiwe na Biblia?

Mke wangu Susana alianza kujifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova waliomwonyesha katika Biblia kwamba Mungu hawatesi watu katika moto. * Vilevile, walimwonyesha ahadi ya Mungu ya kuifanya sayari yetu kuwa makao yaliyo paradiso. * Hatimaye tulipata mafundisho sahihi yanayoeleweka! Katika mwaka wa 1989 Shahidi anayeitwa Nick alianza kunitembelea. Tulipokuwa tukizungumza kuhusu mwili wa binadamu na chanzo chake, nilivutiwa na hoja inayoeleweka kwa urahisi iliyo katika Biblia kwenye Waebrania 3:4, linalosema “kila nyumba hujengwa na mtu fulani, lakini yeye aliyevijenga vitu vyote ni Mungu.”

Je, utafiti wako kuhusu mwili wa mwanadamu ulikusaidia kukubali uumbaji?

Ndiyo. Kwa mfano, njia ambayo mwili wetu hujirekebisha, ilibuniwa kwa ustadi. Kidonda hupona katika hatua nne zinazofuatana, jambo hilo lilinikumbusha  kwamba nikiwa mpasuaji nilishirikiana tu na uwezo wa mwili wa kujirekebisha.

Hebu tueleze, nini hutukia mwili wetu unapojeruhiwa?

Katika sekunde chache, hatua ya kwanza kati ya nyingine zinazozuia kuvuja damu huanza kufanya kazi. Hatua hizo ni tata sana na hufanya kazi vizuri. Kwa kuongezea, mfumo wetu wa damu una mishipa ambayo ikiunganishwa ina urefu wa kilomita 100,000 hivi, na mafundi bomba watamani kuiga uwezo wake wa kuzuia kuvuja na kujirekebisha.

Ni nini kinachofanyika katika hatua ya pili ya kujirekebisha?

Baada ya saa kadhaa damu huacha kuvuja na kidonda kinaanza kuvimba. Kuvimba huhusisha matukio yenye kustaajabisha. Kwanza, mishipa ya damu iliyokuwa imejibana ili kupunguza kuvuja damu, hupanuka. Inapanuka ili kuongeza mtiririko wa damu kwenye kidonda. Kisha, umajimaji uliojaa protini hufanya kidonda chote kivimbe. Umajimaji huo ni muhimu ili kuzuia maambukizo, kuondoa sumu, na kuondoa chembe zilizoharibika. Kila hatua inahitaji mamilioni ya molekuli na chembe za kipekee zinazotengenezwa katika matukio yanayofuatana. Baadhi ya matukio hayo huchochea hatua inayofuata, kisha yanakoma.

Kupona huendelea jinsi gani?

Baada ya siku chache mwili huanza kutokeza chembe mpya, tukio linaloanzisha hatua ya tatu inayofikia kilele baada ya majuma mawili hivi. Chembe zinazotokeza nyuzinyuzi huhamia kwenye kidonda na kuongezeka. Vilevile mishipa midogo ya damu huchipuka na kukua ikielekea kwenye kidonda, ambapo huondoa uchafu na kuleta lishe inayohitajika katika kazi hiyo ya kuondoa na kurekebisha. Katika hatua zinazofuata, chembe za kipekee hutokezwa ili kuunganisha ngozi inayozunguka kidonda.

Hayo ni matukio mengi sana! Inachukua muda gani ili kidonda kipone kabisa?

Hatua ya mwisho ya kupona inaweza kuchukua miezi kadhaa. Mifupa iliyovunjika hurudia nguvu zake na nyuzinyuzi zilizokuwa kwenye kidonda huondolewa na badala yake kunakuwa na ngozi imara. Kwa ujumla jinsi kidonda kinavyopona ni mfano mzuri wa mfumo unaofanya kazi kwa upatano.

Je, unaweza kukumbuka kisa kilichokushangaza?

Ninastaajabu kuona jinsi mwili unavyojirekebisha

Ndiyo. Ninakumbuka nilimtibu msichana fulani mwenye miaka 16 aliyepatwa na aksidenti mbaya ya gari. Alikuwa katika hali mahututi kwani wengu lake lilikuwa limepasuka na alikuwa akivuja damu ndani ya mwili. Kama ingekuwa zamani, tungemfanyia upasuaji ili kurekebisha au kutoa wengu. Leo, madaktari wanategemea zaidi uwezo wa mwili wa kujirekebisha. Nilimpa madawa ya kuzuia uchungu na maambukizo, na matibabu ya kuongeza kiwango cha maji na damu. Majuma kadhaa baadaye, uchunguzi ulionyesha kwamba alikuwa amepona wengu! Ninastaajabu kuona jinsi mwili unavyojirekebisha. Na hivyo ninasadiki kabisa kwamba tuliumbwa na Mungu.

Ni nini kilichofanya upendezwe na Mashahidi wa Yehova?

Walikuwa wenye urafiki na sikuzote walijibu maswali yangu wakitumia Biblia. Nilipendezwa pia na ujasiri wao walipowaeleza wengine kuhusu imani yao na kuwasaidia wajifunze kumhusu Mungu.

Je, kuwa Shahidi wa Yehova kulikusaidia katika kazi yako?

Ndiyo. Kulinisaidia kukabiliana na uchovu wa kihisia ambao hasa huwapata madaktari na wauguzi ambao mara nyingi hushughulika na wagonjwa au watu waliojeruhiwa. Vilevile mgonjwa alipotaka kuongea, nilimweleza kuhusu ahadi ya Muumba wetu ya kuondoa magonjwa na kuteseka * na kuleta ulimwengu mpya ambapo, hakuna mkaaji atakayesema, “Mimi ni mgonjwa.” *