Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

Amkeni!  |  Aprili 2014

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Marekani

Jiji la Los Angeles, California, limepatanisha taa zote karibu 4,500 za barabarani zilizosambaa kotekote katika eneo la kilomita 1,215 za mraba. Kulingana na gazeti la The New York Times, Los Angeles ndilo “jiji la kwanza duniani lenye wakaaji wengi sana kufanya hivyo.”

Ulimwenguni

Uchunguzi wa kiafya ulimwenguni umeonyesha ongezeko la asilimia 82 la watu wanene kupita kiasi kati ya mwaka wa 1990 na 2010. Vifo vinavyotokana na kunenepa kupita kiasi ni mara tatu zaidi ya vifo vinavyosababishwa na kukosa chakula chenye lishe, ingawa bado nchi nyingi zinapambana na ukosefu wa chakula. Majid Ezzati, mmoja wa watafiti hao alisema: “Katika ulimwengu ambao miaka 20 iliyopita haukuwa na chakula cha kutosha, sasa hivi tunapata magonjwa yanayotokana na kula kupita kiasi na vyakula vinavyoleta madhara, hata katika nchi zinazositawi.”

Kisiwa cha Midway

Ndege anayeitwa Laysan albatross, anayeaminiwa kuwa “ndege mwenye umri mkubwa zaidi ulimwenguni,” ameangua tena vifaranga. Ndege huyo ana umri gani? Mara ya kwanza alipotiwa alama mwaka wa 1956 alikuwa na miaka mitano hivi, kwa hiyo, sasa ana umri unaozidi miaka 60. Katika maisha yake inawezekana kwamba ndege huyo amesafiri kati ya kilomita milioni 3 hadi 4, umbali unaolingana na kwenda mwezini na kurudi duniani mara nne hadi sita.

Afrika Kusini

Utafiti mmoja unaonyesha kwamba asilimia 30 hivi ya wanawake nchini Afrika Kusini hutumia sabuni na mafuta yanayofanya ngozi kuwa nyeupe. Vipodozi hivyo vinavyobadili rangi vina madhara na vimepigwa marufuku katika nchi nyingi. Madhara hayo yanatia ndani aina fulani za kansa, ugonjwa wa figo, kushuka moyo, wasiwasi, vipele, na makovu.