Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

Amkeni!  |  Januari 2014

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Nchi Za Afrika Zilizo kusini ya Jangwa la Sahara

“Ni asilimia 38 tu ya watoto walio na umri usiozidi miaka 5 walio na vyeti vya kuzaliwa,” inasema ripoti moja ya shirika la UNICEF kuhusu nchi za Afrika zilizo kusini ya jangwa la Sahara. Licha ya hilo, katika maeneo fulani ya nchi hizo, vyeti vya kuzaliwa ni muhimu ili watoto wapate huduma za afya na elimu, na pia ili mayatima warithi mali za wazazi wao,” anasema Elke Wisch, naibu mkurugenzi wa UNICEF katika nchi za Afrika mashariki na kusini.

 

Italia

 

Utafiti mmoja unaonyesha kwamba kunyanyaswa kupitia Intaneti ndilo jambo linalowaogopesha sana vijana nchini Italia. Asilimia 72 ya vijana wenye umri wa kati ya miaka 12 na 17 wanasema kwamba wanahofu sana jambo hilo. Hiyo ni idadi kubwa ikilinganishwa na idadi ya wanaosema wanaogopa dawa za kulevya (asilimia 55), wanaogopa kutendewa vibaya kingono na mtu mzima (asilimia 44), au wanaogopa kuambukizwa ugonjwa wa zinaa (asilimia 24).

Japani

 

Gazeti The Japan Times, linaripoti kwamba idadi ya vijana Wajapani wanaokataa kupandishwa cheo kazini inazidi kuongezeka. Asilimia 40 kati yao wanachukizwa na jinsi ambavyo watu hawawajibiki kazini na kuenea kwa ukosefu wa unyoofu. Wafanyakazi wengi wanashindwa kuzungumza waziwazi na wasimamizi wao. Ingawa zamani watu walifanya kazi katika kampuni ileile kwa miaka mingi, siku hizi asilimia 60 ya vijana walioajiriwa hufanya kazi huku wakitafuta kazi nyingine bora zaidi.

 

Brazili

 

Kuanzia mwaka wa 1980 hadi 2010, watu 800,000 hivi waliuawa kwa kupigwa risasi nchini Brazili. Zaidi ya 450,000 kati yao walikuwa na umri wa kati ya miaka 15 na 29. Uchunguzi wa visa vya uhalifu vya hivi karibuni ulionyesha kwamba mara nyingi mauaji hayo yanatokea kwa sababu ya ugomvi wa nyumbani, kuzozana na jirani, wivu, au ubishi kati ya madereva.