Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

Amkeni!  |  Januari 2014

 JE, NI KAZI YA UBUNI?

Gundi ya Kipekee ya Buibui

Gundi ya Kipekee ya Buibui

BUIBUI wa kawaida huko Marekani (Parasteatoda tepidariorum) hutengeneza utando wenye gundi yenye nguvu za kuuwezesha kunata ukutani au dhaifu kiasi cha kubanduliwa sakafuni kwa urahisi na hivyo kuwa kama mtego wenye springi unaonasa mdudu anayetambaa. Buibui anawezaje kutengeneza utando wenye nguvu na dhaifu akitumia gundi ileile?

Utando uliofumwa ukutani

Fikiria hili: Buibui hutengeneza utando wake ukutani, kwenye dari, au mahali pengine kwa kufuma nyuzi nyembamba za hariri yenye gundi thabiti isiyoweza kubanduliwa kwa urahisi na mdudu anayeruka. Watafiti katika chuo kikuu cha Akron, huko Ohio, Marekani, wamegundua kwamba kwa upande mwingine buibui hutumia muundo tofauti anapofuma utando sakafuni. Utando wa sakafuni una nyuzi chache kuliko nyuzi zinazofumwa ukutani na hilo huwezesha utando kubanduka kwa urahisi unaponasa mdudu anayetambaa.

Utando uliofumwa sakafuni

Kulingana na ripoti iliyotolewa na chuo kikuu cha Akron, watafiti waliogundua maajabu haya ya uumbaji “tayari wameanza kufikiria jinsi wanavyoweza kutengeneza gundi inayofanana na ile ya buibui.” Wanasayansi wanatumaini kutengeneza gundi inayoweza kutumiwa kufunga bendeji na pia kuunganisha mifupa iliyovunjika.

Una maoni gani? Je, uwezo wa buibui wa kutengeneza utando wenye nguvu au ulio dhaifu kwa kutumia gundi ileile ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?