KWA muda mrefu watu wanaopenda vipepeo barani Ulaya wamevutiwa sana na vipepeo maridadi wenye madoadoa wanaoitwa painted lady (Vanessa cardui) na wamejiuliza vipepeo hao huenda wapi mwishoni mwa majira ya kiangazi. Je, wao hufa mara tu majira ya baridi kali yanapoanza? Utafiti wa hivi karibuni unafunua jambo lenye kustaajabisha. Vipepeo hao husafiri kila mwaka kutoka Ulaya kaskazini hadi Afrika.

Watafiti hao waliunganisha ripoti walizopata kutoka kwa vifaa vya hali ya juu vya rada na ripoti kutoka kwa watu wengi katika maeneo tofauti-tofauti ya Ulaya. Matokeo yalionyesha kwamba majira ya kiangazi yanapokwisha, mamilioni ya vipepeo hao huhama kuelekea upande wa kusini, wakipaa mita zaidi ya 500 juu ya usawa wa bahari—na hivyo si rahisi kwa wanadamu kuwaona. Vipepeo hao husubiri upepo ambao utawasukuma kwa mwendo wa kilomita 45 kwa saa katika safari yao ndefu kuelekea Afrika. Wao hufunga safari hiyo ya umbali wa kilomita 15,000 kila mwaka, kuanzia kaskazini kwenye miisho ya Aktiki kuelekea kusini hadi Afrika Magharibi. Umbali wa safari hiyo ni mara mbili hivi ya ile inayofungwa na kipepeo anayeitwa monarch wa Amerika Kaskazini. Kizazi cha sita cha kipepeo anayeitwa painted lady ndicho kitakachorudi Ulaya baada ya safari hiyo ndefu.

Profesa Jane Hill wa Chuo Kikuu cha York, nchini Uingereza anaeleza hivi: “Painted Lady huendelea tu kusafiri, wakizaana na kuhama.” Kufanya hivyo huwawezesha vipepeo hao kusafiri kila mwaka kutoka Ulaya kaskazini hadi Afrika na kurudi tena.

“Kiumbe huyo mdogo aliye na uzito unaopungua gramu moja na ubongo wenye ukubwa kama kichwa cha pini anafaulu kuhama kutoka bara moja hadi lingine bila kupata mafunzo yoyote kutoka kwa vipepeo wengine wenye umri mkubwa na uzoefu kuliko yeye,” anasema Richard Fox, msimamizi wa uchunguzi katika kituo kinachoshughulikia kuhifadhi vipepeo. Fox anaendelea kusema kwamba “wakati fulani ilifikiriwa kuwa kipepeo huyo anasukumwa popote tu ambapo upepo utampeleka na mwishowe anakufa kutokana na majira ya baridi kali ya Uingereza.” Lakini uchunguzi huo “umeonyesha kwamba Painted Lady ni wasafiri stadi sana.”