KATIDIDI au nyenje wa kichakani wa Amerika Kusini (Copiphora gorgonensis) ana masikio yenye urefu usiozidi milimita moja, hata hivyo, yana uwezo kama ule wa masikio ya wanadamu. Mdudu huyo anaweza kutofautisha mawimbi tofauti-tofauti ya sauti kutoka mbali sana. Kwa mfano, anaweza kutofautisha kati ya sauti ya katididi mwingine na ile ya popo anayewinda.

SIKIO LA KATIDIDI

Fikiria hili: Masikio ya katididi yanapatikana kwenye miguu yake miwili ya mbele. Kama tu sikio la mwanadamu, sikio la katididi hunasa sauti, linaibadili, na kuchanganua mawimbi ya sauti hiyo. Lakini wanasayansi wamegundua kiungo cha pekee ndani ya sikio la mdudu huyo. Kiungo hicho ni kifuko kama puto refu lililojaa umajimaji. Kiungo hicho hufanya kazi kama komboli la sikio la mwanadamu lakini ni ndogo sana kwa kulinganishwa. Kiungo hicho ndicho humsaidia katididi kuwa na uwezo mkubwa wa kusikia.

Profesa Daniel Robert, wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Biolojia cha Bristol, Uingereza anasema kwamba ugunduzi huo utawasaidia mainjinia “kutokeza vifaa vidogo zaidi lakini vyenye uwezo mkubwa zaidi wa kuwasaidia watu kusikia.” Watafiti wanaamini kwamba itachangia katika kutokezwa kwa vifaa vinavyotumia mawimbi ya sauti, kutia ndani vifaa vya eksirei vinavyotumiwa katika hospitali.

Una maoni gani? Je, uwezo wa mkubwa wa kusikia wa katididi ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?