NYANGUMI mwenye nundu aliyekomaa ni mkubwa na mwenye uzito kuliko basi. Hata hivyo, mnyama huyo mkubwa hupiga mbizi na kugeuka kwa wepesi wa ajabu sana. Nyangumi huyo anawezaje kufanya mambo hayo kwa wepesi hivyo? Sababu moja ni vinundu vilivyo juu ya kikono chake.

Fikiria hili: Nyangumi wengi kutia na mamalia wengine wanaoishi baharini wa jamii ya cetacean (kama vile pomboo) wana vikono vilivyo na ncha laini. Hata hivyo, nyangumi mwenye nundu ni tofauti. Ana vinundu vikubwa sana kwenye ncha ya vikono vyake. Nyangumi huyo anapoogelea, maji hupita juu ya vinundu hivyo na kutokeza mawimbi. Vinundu hivyo huelekeza maji upande mmoja na kutokeza msukumo nyuma yake. Hilo husaidia kumsukuma nyangumi, na hivyo kumwezesha kuinamisha vikono vyake katika pembe ya juu bila kupunguza mwendo. Vikono vinapoinamishwa katika pembe ya juu sana hivyo, vinundu vyake huzuia maji yasipunguze kasi yake—na hiyo ni faida moja kubwa ya nyangumi huyo kuwa na vikono virefu sana, kwani kila kimoja kina urefu wa asilimia 33 ya mwili wake.

Wataalamu wanajaribu kuiga mbinu hiyo ili kutengeneza usukani bora zaidi wa mashua, tabo za majini, vinu vya upepo, na rafadha za helikopta.

Una maoni gani? Je, kikono cha nyangumi mwenye nundu kilijitokeza chenyewe? Au kilibuniwa?