Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Chagua lugha Kiswahili

 TUNAYOJIFUNZA KUTOKANA NA HISTORIA | EL REQUERIMIENTO

Tangazo Katika Jina la Mungu

Tangazo Katika Jina la Mungu

“Ikiwa hamtafanya hivi, . . . kwa msaada wa Mungu nitaingia katika kijiji chenu, nami nitapigana nanyi kutoka pande zote na katika kila njia, na nitawalazimisha kulitumikia na kulitii Kanisa pamoja na Mfalme wa Hispania; nami nitawateka wake wenu na watoto wenu na kuwafanya kuwa watumwa, . . . nami nitachukua mali zenu na kuwaumiza kwa njia yoyote ile ninayoweza. . . . Ninyi ndio mtakaolaumiwa kwa vifo vyote pamoja na madhara yatakayotokea, si Mfalme wa Hispania, wala sisi.”

TANGAZO hilo rasmi ni moja kati ya matangazo ya ajabu zaidi. Ni sehemu fulani ya tangazo lililoitwa el Requerimiento katika Kihispania, ambalo katika karne ya 16, lilipaswa kusomwa na washindi Wahispania walipofika katika mabara ya Amerika ili kuyateka.

Tangazo hilo lilimaanisha nini hasa kwa watu wa maeneo hayo, na kwa nini washindi hao walipaswa kulisoma?

Walazimishwa Kuwa Wakatoliki

Muda mfupi baada ya Columbus kufika Amerika mnamo 1492, Hispania na Ureno zilidai kwamba zina haki ya kutawala maeneo hayo mapya. Kwa kuwa nchi zote mbili ziliamini kwamba papa ndiye mwakilishi wa Kristo duniani, ziliamua kwamba yeye ndiye angetatua suala hilo. Chini ya uongozi wa papa, Kanisa liligawia Hispania na Ureno sehemu mbalimbali za maeneo yaliyotekwa, maadamu tu nchi hizo mbili zingewatuma wamishonari ili wageuze wenyeji kuwa Wakristo.

Kadiri washindi walivyoendelea kuteka maeneo mbalimbali, ndivyo mfalme wa Hispania alivyotafuta njia ya kuhalalisha mambo ambayo washindi wake walifanya. Wahispania walisema kwamba kwa kuwa papa alikuwa akimwakilisha Mungu alipowapa nchi hizo, washindi wake walikuwa na uhuru wa kuwaua wenyeji na kuteka mali zao na hata kuwanyang’anya uhuru wao.

 Wahispania waliandika tangazo la kuwajulisha wenyeji kuhusu uamuzi wa papa. Wenyeji walipaswa kukubali Ukristo na kuwa raia wa mfalme wa Hispania. Iwapo wangekataa, Wahispania walijiambia kwamba walikuwa na “haki” ya kupigana na wenyeji hao katika jina la Mungu.

“Ilionekana kuwa sawa kutenda kwa jeuri iwapo mtu anafanya jambo halali. Kwa sababu hiyo, Hispania ilianza kutafuta njia ya kuhalalisha matendo yake.”—Francis Sullivan, profesa Myesuiti wa theolojia.

“Halikuwa la Haki, Halikumheshimu Mungu, Lilikuwa Lenye Kushushia Heshima”

Kusudi la Mfalme wa Hispania kuamua kwamba tangazo hilo lisomwe lilikuwa kutuliza dhamiri yake na kuonyesha kwamba ukoloni ulikuwa halali. Mara nyingi washindi Wahispania walisoma tangazo hilo wakiwa juu ya meli zao kabla ya kuanza vita au wakiwa kwenye nchi kavu mbele ya wenyeji ambao hakuelewa lugha za Ulaya. Nyakati nyingine tangazo hilo lilisomwa mbele ya nyumba tupu za wenyeji waliokuwa wametoroka kwa sababu ya woga.

Jitihada hizo za kuwalazimisha wenyeji wabadili imani yao zilisababisha umwagaji mwingi wa damu. Kwa mfano, watu 2,000 hivi wa kabila la Araucania walichinjwa katika vita huko Chile mnamo 1550. Mshindi Pedro de Valdivia alimwambia mfalme hivi kuhusu wale walioachwa hai: “Watu 200 wamekatwa mikono na pua zao kwa sababu ya kupinga mamlaka kwa ukaidi, ingawa nilikuwa nimetuma wajumbe mara nyingi na kuwapa amri [lile tangazo] kama ulivyoamuru Ee Mfalme.” *

Huenda dhamiri za wavamizi hao zilitulizwa na tangazo hilo liliposomwa. Hata hivyo, halikusaidia kuwachochea wenyeji wakubali dini ya Wahispania. Bartolomé de las Casas, mmishonari na mtawa wa karne ya 16, ambaye alijionea matokeo ya tangazo hilo, aliandika hivi: “Tangazo hilo halikuwa la haki, halikumheshimu Mungu, lilikuwa lenye kushushia heshima, na halikupatana na akili! Isitoshe, lililetea dini ya Kikristo suto kubwa.” Mwandikaji wa matukio anayeitwa Gonzalo Fernández de Oviedo alilalamika kwamba unyama ambao wenyeji wa asili wa Amerika walitendewa ulifanya wawe na maoni mabaya sana kuhusu Ukristo.

Je, Mungu anapaswa kulaumiwa kwa sababu ya unyama huo uliotendwa na wenye mamlaka wa kisiasa na wa kidini waliodai kumwakilisha? Biblia inasema hivi: “Hasha, Mungu wa kweli asitende kwa uovu, na Mweza-Yote kutenda isivyo haki!”—Ayubu 34:10.

^ fu. 12 Kulingana na vitabu fulani, tangazo hilo lilifutwa katika mwaka wa 1573.