KITI cha pweza anayeitwa brittle star anayeishi katika matumbawe, ana gamba la ajabu katika sehemu ya juu ya mwili wake. Gamba lake limejaa lenzi nyingi ndogondogo zinazomfanya awe na jicho kubwa lililogawanywa katika sehemu nyingi.

Vinundu vyenye kung’aa vilivyo kwenye gamba vinatumika kama lenzi ndogo sana za hali ya juu

Fikiria hili: Gazeti Natural History linasema kwamba wanasayansi walipochunguza mabamba yaliyo kwenye gamba la kiumbe huyo, waliona “umbo la ajabu la vinundu vingi vyenye kung’aa vilivyokuwa karibu-karibu na kila kimoja kilikuwa chembamba kuliko unywele wa mwanadamu.” Vinundu hivyo vilivyotengenezwa kwa kalisi kaboni vilikuwa lenzi ndogo sana za hali ya juu ambazo hupitisha mwangaza kwenye neva za kupokea mwangaza zilizokuwa chini ya mabamba hayo. Isitoshe, lenzi hizo zina umbo barabara linalohitajiwa kutokeza picha inayotakiwa.

Mwanakemia Joanna Aizenberg, anasema kwamba gamba la kiumbe huyo lililo na matumizi mawili “linaonyesha kanuni hii muhimu: katika biolojia, mara nyingi vitu huwa na matumizi mengi.”

Wakijifunza kutokana na brittle star, watafiti wamebuni njia rahisi na isiyogharimu pesa nyingi ya kutengeneza lenzi nyingi ndogondogo kutokana na kalisi kaboni. Matumizi mbalimbali ya lenzi hizo yanatia ndani mawasiliano ya simu, ambapo lenzi hizo hutumiwa kutuma ishara za mwangaza kupitia nyuzi nyembamba za kioo.

Una maoni gani? Je, gamba la kiti cha pweza anayeitwa brittle star lilitokana na mageuzi? Au lilibuniwa?