Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

Amkeni!  |  Februari 2013

 JE, NI KAZI YA UBUNI?

Mkia wa Mjusi Anayeitwa Agama

Mkia wa Mjusi Anayeitwa Agama

MJUSI anayeitwa agama huruka kutoka mahali tambarare hadi ukutani bila matatizo yoyote. Lakini iwapo mahali tambarare ni laini, mjusi huyo huteleza lakini bado anafaulu kuruka na kujishikilia ukutani. Anafanyaje hivyo? Siri ya mjusi huyo ni mkia wake.

Fikiria hili: Mijusi hao wanaporuka kutoka kwenye eneo tambarare lenye mikwaruzo—ambalo huwasaidia kujishikilia vizuri—kwanza wao husawazisha miili yao na kuhakikisha mkia wao umelala chini. Hilo huwawezesha kuruka kwa pembe inayofaa. Hata hivyo, mijusi hao wanapokuwa kwenye sehemu laini, wao huteleza na kuruka kwa pembe isiyofaa. Lakini wakiwa hewani, wao husawazisha mwili wao inavyofaa kwa kurusha mkia wao juu. Hawafanyi hivyo ovyoovyo tu. “Lazima mijusi hao wabadili pembe ya mkia wao kwa njia inayofaa kabisa ili waendelee kuwa wima,” inasema ripoti moja iliyotolewa na Chuo Kikuu cha California, Berkeley. Kadiri sehemu anayokanyaga ilivyo na utelezi ndivyo mjusi huyo anavyolazimika kuinua mkia wake ili atue kwa njia inayofaa.

Mkia wa mjusi huyo unaweza kuwasaidia mainjinia kubuni magari ya roboti yasiyoanguka kwa urahisi ambayo yanaweza kutumiwa kuwatafuta waokokaji baada ya tetemeko la nchi au msiba mwingine. “Roboti hazina uwezo wa kujisawazisha kama wanyama,” anasema mtafiti Thomas Libby, “kwa hiyo, chochote kinachoweza kuzifanya ziwe imara zaidi ni maendeleo.”

Una maoni gani? Je, mkia wa mjusi anayeitwa agama ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?