INASEMEKANA kwamba watu wa kabila la Baka—ambao pia hujulikana kama Mbilikimo—ndio wakazi wa mapema zaidi wa nchi ya Kamerun. Kisha, katika miaka ya 1500, Wareno walifika nchini Kamerun. Baada ya miaka mingi, watu wa kabila la Fulani—ambao ni Waislamu—walishinda na kumiliki maeneo ya kaskazini mwa Kamerun. Leo, asilimia 40 ya wakazi wa Kamerun ni Wakristo, asilimia 20 ni Waislamu, na asilimia 40 wanaosalia ni wa dini za kienyeji za Afrika.

Mashahidi wa Yehova wamechapisha machapisho yanayotegemea Biblia katika lugha ya Bassa inayozungumzwa nchini Kamerun

Watu wanaoishi maeneo ya vijijini ni wakarimu sana. Wao huwasalimu wageni na kuwakaribisha ndani ya nyumba zao na kuwapa chakula na maji. Ikiwa mgeni anakataa ukarimu wa mwenyeji wake anaonekana kuwa amekosa heshima, kwa upande mwingine kukubali kunaonwa kuwa heshima.

Mazungumzo huanza kwa kuwasalimu watu wa familia na kuuliza kuhusu hali yao. Wakati mwingine ni kawaida watu kuuliza kuhusu hali ya mifugo! “Mgeni anapoondoka, haitoshi tu kusema, ‘Kwaheri,’” anasema  Joseph, mwenyeji wa Kamerun. “Mara nyingi, mwenyeji humsindikiza mgeni wake umbali fulani huku wakiendelea kuzungumza. Kisha, atamuaga mgeni wake na kurudi nyumbani kwake. Mgeni asipotendewa kwa njia hiyo anaweza kuhisi kwamba amedharauliwa.”

Ni kawaida kuona mitumbwi kwenye Mto Sanaga. Matanga hutengenezwa kwa vifaa vyovyote vinavyopatikana

Wakati wa mlo, nyakati nyingine watu hula kutoka kwenye sahani moja—na nyakati nyingine wanafanya hivyo kwa mikono yao. Nchini Kamerun, mazoea hayo ya kula pamoja ni ishara yenye nguvu ya kuonyesha umoja. Nyakati nyingine kula pamoja kumetumiwa kama njia ya kuwapatanisha marafiki ambao huenda urafiki wao umezorota kwa sababu fulani. Watu wanapokula pamoja ni kana kwamba wanasema, “Sasa tumepatana.”

Mashahidi wa Yehova, wachapishaji wa gazeti hili, wana zaidi ya makutaniko 300 nchini Kamerun na wanajifunza Biblia na watu karibu 65,000 katika nchi hiyo