NDANI ya msitu wa mvua wa ikweta katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kuna hazina ya asili ambayo watu wachache wamewahi kuiona. Tulisafiri kwa muda wa saa 12 kupitia njia mbovu ili kufika kwenye Mbuga ya Wanyama ya Dzanga-Ndoki, iliyoko kusini-magharibi mwa nchi hiyo, kwenye mpaka kati yake na nchi za Kamerun na Jamhuri ya Kongo. Lengo letu lilikuwa kumwona sokwe anayeitwa Makumba pamoja na familia yake, wanaoishi kwenye nyanda za chini za magharibi.

Bara, mwenyeji aliyekuwa akitutembeza, alituambia kwamba ni muhimu kutembea pamoja katika kikundi na pia kuwa macho kwa kuwa kila siku tembo hupitia katika njia hizo wanapoenda kutafuta chakula. Hata hivyo, si tembo pekee waliotuogopesha. Bara alituonya hivi: “Sokwe anapojaribu kukushambulia, simama tuli na utazame chini. Hatakuumiza; isipokuwa atapiga makelele. Usimtazame usoni. Mimi huona ni afadhali tu kufunga macho.”

Sisi na Bara tulisindikizwa na mtaalamu wa kufuata alama za wanyama wa kabila la BaAka, watu ambao wanaonwa kuwa Mbilikimo kwa sababu ya maumbile yao na ufupi wao. Mwenyeji huyo stadi wa kufuata alama za wanyama anaweza kutambua ikiwa kuna wanyama  wasioweza kuonekana kwa urahisi kwa kutegemea harufu, sauti, au iwapo ataona sehemu fulani ndogo tu ya mwili wao. Kulikuwa na nyuki wengi waliotusumbua tulipotembea. Ilikuwa vigumu kumfuata kwa ukaribu mwenyeji huyo kwani alipita kwenye vichaka kwa urahisi!

Punde si punde mwenyeji huyo akatuongoza kupitia msitu ambao ni watu wachache kutoka nchi za Ulaya au Marekani wamewahi kufika. Kisha kwa ghafla, akasimama na kutupungia mkono ili kutuonyesha eneo kubwa lililokuwa karibu na njia yetu. Tuliona vichaka vilivyoangushwa na nyasi zilizolazwa ambapo sokwe wadogo walikuwa wamechezea, na pia tuliona matawi yaliyochunwa na kuvunjwavunjwa​—mabaki ya chakula cha asubuhi cha sokwe hao. Hamu yetu ilizidi kuongezeka kadiri tulivyosonga mbele.

Sokwe wa nyanda za chini za magharibi anaweza kukua na kufikia urefu wa mita 1.8 na uzito wa zaidi ya kilogramu 200

Baada ya kutembea kwa kilomita tatu hivi, mtafuta alama huyo alipunguza mwendo. Ili asiwashtue sokwe, alitokeza sauti fulani. Karibu na mahali hapo tulisikia sauti za kukoroma zilizoambatana na kuvunjika kwa matawi ya miti. Bara alituonyesha ishara kwamba tumfuate. Aliweka kidole chake kwenye midomo, ili kuashiria kwamba tunapaswa kunyamaza kimya. Alituambia tuchuchumae na akaelekeza kidole kwenye miti. Karibu mita nane mbele yetu tukamwona Makumba!

Msitu wote ulikuwa kimya, na sasa sauti pekee ambazo tungeweza kusikia ni mapigo ya mioyo yetu. Swali lililokuwa likituhangaisha lilikuwa, Je, Makumba atatushambulia? Makumba alitutazama kwa uso wenye makunyanzi na baada ya kutukagua akatukaribisha kwa kupiga mwayo. Tukashusha pumzi na tukajihisi tumetulia!

Ingawa katika lugha ya Aka jina Makumba humaanisha “Mwenye mbio,” pindi tulipokuwa hapo pamoja na sokwe huyo alikuwa akila taratibu chakula cha asubuhi. Kando ya Makumba, sokwe wawili wadogo walikuwa wakicheza mieleka. Sopo, sokwe mwenye umri wa miezi kumi aliye na macho makubwa, alikuwa akicheza karibu na mama yake, Mopambi, ambaye alikuwa akimvuta kwa wororo ili asiende mbali kwa sababu ya udadisi wake. Sokwe wengine katika familia hiyo walikuwa wakila majani na matawi au kuchezacheza wakipiga kelele huku wakitutazama mara kwa mara kabla hawajachoka na kuendelea na michezo yao.

Baada ya saa moja muda wetu wa kumtazama Makumba ulikuwa umekwisha. Akionyesha amechoshwa nasi, Makumba alikoroma na kuinuka kisha akaelekea msituni. Baada ya sekunde chache, familia yote ikatoweka. Ingawa tulitumia muda mfupi tu pamoja na viumbe hao wa ajabu, hatutawasahau.