JE, UNA wasiwasi kuhusu wakati ujao? Ikiwa ndivyo, kuna watu wengi wanaohisi kama wewe. Tangu zamani za kale, watu wamekuwa wakikisia kuhusu wakati ujao wa ulimwengu huu, na wengi wamekata kauli kwamba hakuna matumaini. Kwa maelfu ya miaka, watu wametaka sana kujua jinsi mwisho wa dunia utakavyokuwa.

Kwa mfano, fikiria hadithi za kubuniwa za hivi karibuni. Vitabu vya katuni, televisheni, mamia ya sinema, na maelfu ya vitabu vinasimulia jinsi ambavyo ulimwengu huu utaangamizwa. Hadithi hizo zinasimulia jinsi ambavyo wanadamu watavamiwa na kuangamizwa na vitu fulani vyenye nguvu sana kama vile, roboti zenye kuua, majitu ya kila aina, viumbe kutoka sayari nyingine, madubwana, mizimu, majoka, sokwe, ndege, panya wenye umbo lisilo la kawaida, na nyigu wakubwa sana. Kwa kweli, hakuna mtu anayeweza kuamini hadithi hizo!

Lakini kuna hadithi na nadharia nyingine ambazo huwaogopesha watu fulani. Baadhi ya nadharia hizo zinasemekana kuwa za kisayansi. Nadharia moja inasema kwamba tabaka lote la juu la dunia litasonga ghafula na hilo litasababisha tsunami zenye nguvu, matetemeko ya nchi, na volkano. Nyingine inadai kwamba sayari zote zitajipanga katika mstari mmoja na hilo litasababisha kuongezeka kwa upepo kutoka kwenye jua ambao utaleta uharibifu mkubwa duniani. Na bado nadharia nyingine inasema kwamba ncha za dunia zenye nguvu za sumaku zitajigeuza ghafula kuelekea upande mwingine na kusababisha mnururisho kutoka kwenye jua utuue sisi sote. Usiwe na hofu. Mambo hayo hayatatendeka.  Hata hivyo, matukio hayo ya kuwaziwa bado yanawavutia watu wengi.

Namna gani vitabu vingi na Tovuti kuhusu mwisho wa dunia zinazotabiri kwamba ulimwengu utaisha Desemba 21 mwaka huu? Chanzo kimoja kinadai kwamba sayari ya kuwaziwa inayoitwa Nibiru (au Sayari X) iko mwendoni kuja kugongana na dunia na itafika hapa Desemba 2012. Nadharia hizo na nyingine ambazo haziungwi mkono na mambo hakika zinategemea kalenda ya kale ya Wamaya, ambayo watu fulani wanasema kwamba mwaka wake wa mwisho utakuwa Desemba 2012.

Watu fulani ambao wameamini matabiri kama hayo ya maangamizi, wamejenga mahali pa kujificha nje ya nyumba zao au wamelipa pesa nyingi ili kujihifadhia vyumba katika mahandaki ya umma. Wengine wamehamia milimani mahali ambapo hakuna huduma za umma kama vile maji, vifaa vya kupasha nyumba joto, au umeme.

Bila shaka, kuna watu ambao hawaamini hadithi na nadharia hizo. Wanapuuza wazo la kwamba mwisho wa dunia unakaribia. Kwa mfano, wanasayansi katika shirika la NASA wanasema hivi: “Dunia haitapatwa na madhara yoyote katika mwaka wa 2012. Kwa zaidi ya miaka bilioni 4 hakuna jambo lolote baya limeipata sayari yetu, na wanasayansi wenye kutumainika ulimwenguni pote hawana habari zozote kuhusu tisho linalohusianishwa na mwaka wa 2012.”

Hata hivyo, ni kosa kukata kauli kwamba hakuna hatari yoyote inayowakabili wanadamu au kwamba ni watu wanaodanganyika kwa urahisi ndio huamini kwamba mwisho wa dunia ni jambo hakika. Kweli mwisho wa dunia utafika? Ikiwa ndivyo, utafika lini na jinsi gani?