MBALI na madai yaliyotajwa katika makala iliyotangulia kuhusu mwisho wa dunia, kuna mambo tunayopaswa kufikiria kwa uzito. Watu wengi wanahofu kwamba idadi ya watu itaongezeka sana duniani na kwa sababu hiyo kutakuwa na ukosefu wa maji na chakula. Wengine wana wasiwasi kuhusu matokeo ya kuporomoka kwa uchumi ulimwenguni pote. Namna gani kuhusu misiba ya asili, kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza, au vita vya nyuklia? Je, mambo hayo yanaweza kusababisha msiba mkubwa ulimwenguni pote?

Acheni tuzungumzie kifupi hali fulani ambazo watu wanasema zitasababisha mwisho wa dunia. Si hali zote zinazotishia kuua kila mtu duniani, lakini zinaweza kuleta madhara makubwa kwa wanadamu. Hali hizo zinatia ndani mambo yafuatayo.

 Volkano Zinazosababisha Uharibifu Mkubwa

Katika mwaka wa 1991, Mlima Pinatubo huko Filipino ulilipuka na kuwaua watu zaidi ya 700 na kuwaacha watu 100,000 hivi bila makao. Wingu kubwa la majivu liliinuka kilomita 30 angani na kisha kuanguka ardhini na kufunika mazao na kusababisha paa za majengo kuporomoka. Mlima Pinatubo na volkano nyingine kama hiyo husababisha mabadiliko ya hali ya hewa kwa miaka kadhaa baada ya kulipuka.

Iwapo milipuko mikubwa itatokea, kama ile ambayo imetokea miaka mingi iliyopita, itakuwa mikubwa zaidi na mibaya zaidi kuliko milipuko yoyote ambayo imewahi kutokea katika historia na itasababisha uharibifu mkubwa zaidi. Mbali na kusababisha uharibifu mkubwa mara moja, mabadiliko ya hali ya hewa yataharibu mazao, yatasababisha ukosefu wa chakula, na hilo litafanya watu wengi wafe njaa.

“Volkano za kawaida huua mimea na wanyama wanaoishi mbali sana na mahali ambapo mlipuko ulitokea; volkano zenye nguvu zaidi zinatishia kuangamiza jamii nzimanzima kwa kusababisha mabadiliko ya hali ya hewa ulimwenguni pote.”​—National Geographic.

Mawe Kutoka Angani

Asubuhi moja katika mwaka wa 1908, mwanamume fulani alikuwa ameketi nje ya duka moja katika kituo cha kibiashara huko Vanavara, Siberia wakati mlipuko fulani ulipomrusha kutoka katika kiti chake. Alihisi joto kali sana ni kana kwamba shati lake lilikuwa likiwaka moto. Mlipuko huo ulitokea umbali wa kilomita 60 hivi kutoka mahali alipokuwa. Mlipuko huo ulisababishwa na jiwe kutoka angani lililokuwa na kipenyo cha mita 35 na uzito wa kilogramu milioni 100 hivi. Baada ya kuingia kwenye angahewa la dunia, jiwe hilo lililipuka kwa sababu ya shinikizo kubwa na joto lililotokezwa jiwe hilo lilipokuwa likiteremka. Mlipuko huo ulitokeza nishati inayolingana na mabomu 1,000 kama yale yaliyoangushwa huko Hiroshima na uliharibu eneo lenye ukubwa wa kilomita 2,000 hivi za mraba katika msitu wa Siberia. Bila shaka, jiwe kubwa zaidi ya hilo linaweza kusababisha uharibifu mkubwa zaidi, kutokeza mioto mikubwa, na kusababisha kiwango cha joto ulimwenguni pote kupungua sana na hivyo kusababisha wanyama na mimea mingi kutoweka.

“Katika historia yote ya dunia, nyota-mikia na mawe kutoka angani yameanguka duniani. Mambo hayo yalitukia mara nyingi zaidi zamani, na yatatukia tena. Lakini hatujui ni lini.”​Chris Palma, mhadhiri mkuu wa astronomia na fizikia ya anga katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Pennsylvania.

 Mabadiliko ya Hali ya Hewa

Wanasayansi wanaamini kwamba mambo kama vile kupanda kwa kiwango cha joto duniani, hali mbaya sana ya hewa, kuyeyuka kwa barafu iliyo kwenye vilele vya milima na miamba ya barafu, kutoweka kwa matumbawe na aina muhimu za wanyama na mimea, kunaonyesha kwamba hali ya hewa inabadilika ulimwenguni pote. Ingawa watu wana maoni yanayotofautiana, wengi wanaamini kwamba tatizo hilo linasababishwa na magari na viwanda vinavyotumia makaa ya mawe, mafuta, na gesi za asili​—nishati hizo za asili hutokeza kiasi kikubwa cha gesi ya kaboni dioksidi angani.

Wataalamu fulani wanasema kwamba gesi hizo zinachangia kuongezeka kwa joto duniani kwa kuwa zinazuia joto lisitoke duniani na kurudi angani. Kwa sababu miti hufyonza kaboni dioksidi, huenda ukataji wa miti mingi ukachangia pia kubadilika kwa hali ya hewa.

“Ikiwa kiwango cha sasa cha kuongezeka kwa joto duniani kitaendelea na utokezaji wa kaboni dioksidi hautapunguzwa, wanasayansi wengi wasema kwamba kiwango cha wastani cha joto duniani kitaendelea kuongezeka na kutokeza mabadiliko makubwa ya hali ya hewa na bahari zitafurika na kuhatarisha maisha ya watu wengi wanaoishi sehemu za pwani.”​—A Mind for Tomorrow: Facts, Values, and the Future.

Kuenea kwa Magonjwa ya Kuambukiza

Katika karne ya 14, Tauni iliua asilimia 33 ya watu wote barani Ulaya katika muda wa miaka miwili tu. Kati ya mwaka wa 1918 na 1920, Homa ya Hispania iliua watu milioni 50 hivi. Njia duni za usafiri zilizuia magonjwa hayo yasienee haraka. Hata hivyo, kwa kuwa leo kuna ukuzi mkubwa wa majiji na njia rahisi zaidi za usafiri wa kimataifa, magonjwa kama hayo yanaweza kuenea haraka sana katika mabara yote.

Ugonjwa hatari kama huo unaweza kusababishwa na vitu vya asili. Lakini kuna hofu inayozidi kuongezeka ya silaha za kibiolojia, yaani, viini vya magonjwa vinavyotengenezwa na wanadamu kwenye maabara. Wataalamu katika nyanja hiyo wanasema kwamba watu wachache wenye ujuzi unaohitajika wanaweza kununua vifaa kwenye Intaneti na kutengeneza silaha hatari za kibiolojia.

“Ugonjwa unaotokea kwa njia ya asili ni tisho kubwa kwa afya; hata hivyo, ikiwa adui mwenye ujuzi atapata viini hivyo​—au viini sugu visivyoweza kutibiwa kwa dawa, au vilivyotengenezwa katika maabara—anaweza kusababisha madhara makubwa sana.”​—Kituo cha Utafiti Kuhusu Ugaidi cha Bipartisan WMD.

 Kutoweka kwa Aina Muhimu za Viumbe Hai

Katika muda wa miaka mitano iliyopita, wafugaji wa nyuki nchini Marekani wamepoteza karibu asilimia 30 ya nyuki wao kila mwaka kwa sababu ya kutoweka ghafula na kwa njia isiyoeleweka kwa vikundi vizima-vizima vya nyuki, jambo ambalo linatendeka ulimwenguni pote. Nyuki hufanya mengi zaidi ya kutengeneza asali. Wao huchavusha mazao muhimu kama vile zabibu, matofaa, soya, na pamba. Nyuki ni muhimu sana kwetu.

Pia mwani ni muhimu kwetu. Mwani usipokuwepo, samaki hawatakuwepo. Bila minyoo ambayo husaidia kuingiza hewa kwenye udongo, tungevuna mazao machache. Kutoweka kwa aina hizo muhimu kungesababisha upungufu wa chakula na njaa, na hilo lingetokeza jeuri na vurugu. Uchafuzi, kuongezeka kwa idadi ya watu, kutumia mali za asili kupita kiasi, uharibifu wa mazingira, na mabadiliko ya hali ya hewa huchangia kutoweka kwa aina za wanyama labda zaidi ya mara 1,000 kuliko wanavyotoweka kwa njia ya asili.

“Kila mwaka, kati ya aina 18,000 na 55,000 za viumbe hai hutoweka. Kisababishi: utendaji wa wanadamu.”​—Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo.

Vita vya Nyuklia

Mlipuko mmoja wa nyuklia unaweza kufutilia mbali mara moja jiji zima—ukweli wenye kuhuzunisha ambao ulionekana wazi mara mbili mnamo Agosti 1945. Mlipuko wa nyuklia una nguvu nyingi sana zenye kutisha, nao unaharibu na kuua kwa kutokeza wimbi la shinikizo la hewa, upepo, joto, moto, na mnururisho. Mnururisho hutia sumu kwenye chakula na maji. Vita vya nyuklia vingesababisha kiasi kikubwa cha vumbi kutupwa hewani na hivyo kufunika mwangaza wa jua na kusababisha kiwango cha joto ulimwenguni kushuka. Mazao na mimea mingine ingekufa. Bila chakula, wanadamu na wanyama wangekufa. Inasemekana kwamba nchi tisa hivi zina uwezo wa kurusha makombora ya nyuklia. Nchi nyingine chache ziko katika harakati ya kutengeneza silaha zao za nyuklia. Na mashirika ya kigaidi yanatamani sana kupata silaha hizo.

“Silaha za nyuklia ndizo tisho kuu na hatari zaidi kwa jamii ya kibinadamu. . . . Bado kuna silaha 25,000 hivi za nyuklia ulimwenguni pote . . . Siku moja, magaidi watapata silaha hizo.”​—Muungano wa Wanasayansi Wanaojali.