KASUKU wenye rangi maridadi wanaonekana wakiruka angani katika misitu ya Amerika ya Kusini na ya Kati! Mandhari hiyo ndiyo iliyowastaajabisha wavumbuzi kutoka Ulaya walipofika katika eneo hilo mwishoni mwa karne ya 15. Kasuku hao wanaoitwa macaw, wana mikia mirefu na wanapatikana katika maeneo ya kitropiki ya Amerika. Muda mfupi baadaye, picha za ndege hao maridadi zikaanza kuonekana katika ramani za eneo hilo ili kuwakilisha maeneo hayo maridadi.

Kasuku wa jinsia zote mbili wana rangi zinazong’aa. Jambo hilo si la kawaida kati ya ndege wenye rangi nyangavu. Pia, wana akili nyingi, wanaishi katika vikundi, nao hutoa sauti kali sana. Wakiwa katika vikundi vya ndege 30 hivi, wao hutoka katika viota vyao asubuhi na mapema kwenda kutafuta mbegu, matunda, na vyakula vingine. Kwa kawaida, kasuku hutumia kucha zake ndefu kukamata chakula naye hula kwa kutumia mdomo wake mkubwa uliopinda. Wanaweza hata kupasua kokwa gumu sana la mbegu kwa kutumia mdomo huo. Baada ya kula, wao huenda kwenye majabali au kando ya mito ili kula udongo wa mfinyanzi. Udongo huo huwasaidia kupunguza kiasi cha sumu walichokula na kupata kemikali nyingine wanazohitaji.

“[Mungu] amefanya kila kitu kiwe chenye kupendeza kwa wakati wake.”—Mhubiri 3:11

 Kwa kawaida, kasuku hawa hutaga na mwenzi yuleyule maisha yao yote, nao hushirikiana kulea vifaranga. Kasuku hao hutengeneza viota kwenye miti, kingo za mito, vichuguu, nyufa za majabali na unaweza kumwona mmoja akimsafisha mwenzake. Ingawa vifaranga vya kasuku hukomaa baada ya miezi sita, vifaranga hivyo huendelea kukaa na wazazi kwa miaka mitatu hivi. Kasuku hawa huishi kwa kipindi cha miaka 30 hadi 40 hivi wakiwa msituni, lakini kuna wale ambao wameishi kwa miaka zaidi ya 60 wakiwa wamefugwa. Kuna zaidi ya aina 18 za kasuku, na baadhi yake wameonyeshwa hapa.

Macaw mwenye mabawa ya kijani, pia anaitwa macaw wa rangi nyekundu na kijani. Urefu: hufikia sentimita 95

Macaw mwekundu. Urefu: sentimita 85

Hyacinth macaw. Urefu: hufikia sentimita 100. Ndiye kasuku mkubwa kuliko wote, anaweza kufikia uzito wa kilo 1.3