KUWA MWAJIBIKAJI KUNAHUSISHA NINI?

Watu wanaowajibika ni wenye kutegemeka. Wao hujitahidi kufanya vizuri kazi walizopangiwa na kuzimaliza kwa wakati.

Watoto wanaweza kujifunza kuwa wawajibikaji, licha ya uwezo wao mdogo. “Mtoto huanza kuwa na uwezo wa kushirikiana na wengine anapokuwa na miezi kumi na tano, na kufikia umri wa miezi kumi na nane hivi anaanza kutamani kushiriki shughuli zinazoendelea. Katika jamii nyingi, wazazi huanza kuwazoeza watoto wao kufanya kazi wanapokuwa na umri wa kati ya miaka mitano hadi saba, na licha ya umri huo mdogo, watoto wanaweza kushiriki kazi nyingi za nyumbani.”​—Kitabu Parenting Without Borders.

KWA NINI NI MUHIMU KUWA MWAJIBIKAJI?

Baadhi ya vijana huondoka nyumbani na kujaribu kujitegemea, lakini maisha huwawia vigumu na hivyo wanaamua kurudi kuishi nyumbani kwa Baba na Mama. Wakati mwingine, hali hiyo hutokea kwa sababu vijana hawakufundishwa jinsi ya kutumia pesa vizuri, kusimamia nyumba, au kushughulikia majukumu ya kila siku.

Kwa hiyo inafaa umzoeze mtoto wako kutimiza majukumu sasa ili asihangaike akiwa mtu mzima. “Hungetaka aendelee kukutegemea hadi atakapofikisha umri wa miaka kumi na nane, kisha umtelekeze akapambane na ulimwengu.”​—Kitabu How to Raise an Adult.

JINSI YA KUWAFUNDISHA WATOTO KUWAJIBIKA

Wapangie kazi za kufanya nyumbani.

KANUNI YA BIBLIA: “Kila aina ya kazi ngumu ina faida.”​—Methali 14:23.

Watoto wadogo huwa na hamu ya kufanya kazi pamoja na wazazi wao. Hivyo, tumia fursa hiyo kuwapangia kazi za nyumbani.

Baadhi ya wazazi husita kuwapangia watoto kazi. Wanajiambia kwamba watoto wao ambao bado wanasoma wanapewa kazi nyingi sana za shule kila siku, hivyo, kwa nini wawaongezee mzigo mwingine?

Hata hivyo, kuna uwezekano mkubwa wa watoto ambao hufanya kazi za nyumbani kufaulu shuleni, kwa kuwa kazi hizo huwafundisha kukubali majukumu na kuyakamilisha. Kitabu Parenting Without Borders, kinasema kwamba, “tunapopuuza tamaa ya watoto ya kufanya kazi wakiwa wadogo, wanajijengea wazo la kwamba si muhimu kwao kuchangia katika mambo mbalimbali . . . Pia, wanaanza kutazamia kuhudumiwa na wengine.”

 Kama maelezo hayo yanavyoonyesha, kufanya kazi za nyumbani huwazoeza watoto kuwatumikia wengine na si kutumikiwa, kuwa watoaji na si wapokeaji. Kazi za nyumbani huwasaidia watoto kuhisi wanathaminiwa na wana jukumu la pekee katika familia.

Wasaidie watoto wako kuwajibika kwa makosa yao.

KANUNI YA BIBLIA: “Sikiliza mashauri na ukubali nidhamu, ili uwe na hekima wakati wako ujao.”​—Methali 19:20.

Mtoto wako akikosea, usiwe na mwelekeo wa kuficha kosa lake. Mpe nafasi ya kuwajibika kwa makosa yake. Kwa mfano, ikiwa ameharibu kitu cha mtu bila kukusudia, atahitaji kuomba msamaha, na hata ikihitajika, kufidia kitu hicho.

Watoto wanapoelewa kwamba wanawajibika kwa makosa wanayofanya, wanajifunza

  • kuwa wanyoofu na kukubali makosa yao

  • kutowalaumu wengine

  • kutotoa visingizio

  • kuomba msamaha inapohitajika