Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Chagua lugha Kiswahili

Mwanzo 23:1-20

MUHTASARI WA YALIYOMO

  • Kifo cha Sara na mahali alipozikwa (1-20)

23  Na Sara aliishi miaka 127; hiyo ndiyo iliyokuwa miaka ya maisha ya Sara.+  Basi Sara akafa huko Kiriath-arba,+ yaani, Hebroni,+ katika nchi ya Kanaani,+ naye Abrahamu akaanza kumwombolezea Sara na kumlilia.  Kisha Abrahamu akainuka na kutoka mahali ambapo maiti ya mke wake ilikuwepo, akawaambia wana wa Hethi:+  “Mimi ni mgeni na mhamiaji miongoni mwenu.+ Nipeni ardhi ya kuzikia miongoni mwenu ili niweze kuwazika watu wangu waliokufa.”  Ndipo wana wa Hethi wakamwambia Abrahamu:  “Tusikilize, bwana wetu. Wewe ni kiongozi aliyechaguliwa na Mungu* miongoni mwetu.+ Unaweza kuwazika watu wako waliokufa mahali bora zaidi katika maeneo yetu ya kuzikia. Hakuna yeyote kati yetu atakayekunyima mahali pa kuwazika watu wako waliokufa.”  Basi Abrahamu akasimama na kuinama mbele ya wenyeji wa nchi, wana wa Hethi,+  akawaambia: “Ikiwa mmekubali nimzike mtu wangu aliyekufa, basi nisikilizeni na mumsihi Efroni mwana wa Zohari  aniuzie pango lake la Makpela; liko ukingoni mwa shamba lake. Na aniuzie mbele yenu kwa kiasi kamili cha fedha+ ili niwe na mahali pa kuwazikia watu wangu.”+ 10  Sasa Efroni alikuwa ameketi kati ya wana wa Hethi. Kwa hiyo Efroni Mhiti akamjibu Abrahamu mbele ya wana wa Hethi, na mbele ya wote walioingia katika lango la jiji,+ akasema: 11  “Hapana, bwana wangu! Nisikilize. Ninakupa shamba hilo pamoja na pango lililomo. Ninakupa mbele ya wana wa watu wangu. Mzike mtu wako aliyekufa.” 12  Ndipo Abrahamu akainama chini mbele ya wenyeji wa nchi 13  na kumwambia hivi Efroni mbele ya watu: “Tafadhali, nisikilize! Nitakupa kiasi kamili cha fedha kwa ajili ya shamba hilo. Zichukue kutoka mikononi mwangu, ili nimzike humo mtu wangu aliyekufa.” 14  Kisha Efroni akamwambia Abrahamu: 15  “Bwana wangu, nisikilize. Thamani ya shamba hili ni shekeli 400 za fedha,* lakini hiyo ni nini kati yangu na wewe? Mzike mtu wako aliyekufa.” 16  Abrahamu akamsikiliza Efroni, na Abrahamu akampimia Efroni kiasi cha fedha alichokuwa amemtajia mbele ya wana wa Hethi, shekeli 400 za fedha* kulingana na uzito uliokubaliwa na wafanyabiashara.+ 17  Kwa hiyo shamba la Efroni lililokuwa Makpela, mbele ya Mamre—shamba na pango lililokuwemo na miti yote iliyokuwa ndani ya mipaka ya shamba hilo—likathibitishwa kuwa 18  mali ya Abrahamu aliyoinunua mbele ya wana wa Hethi, mbele ya wote walioingia katika lango la jiji lake. 19  Baada ya hayo Abrahamu akamzika Sara mke wake katika pango la shamba la Makpela mbele ya Mamre, yaani, Hebroni, katika nchi ya Kanaani. 20  Hivyo wana wa Hethi wakamkabidhi Abrahamu lile shamba pamoja na pango lililokuwemo ili awazike watu wake humo.+

Maelezo ya Chini

Au labda, “kiongozi mkuu.”
Shekeli moja ilikuwa na uzito wa gramu 11.4. Angalia Nyongeza B14.
Shekeli moja ilikuwa na uzito wa gramu 11.4. Angalia Nyongeza B14.