Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Chagua lugha Kiswahili

Kutoka 36:1-38

MUHTASARI WA YALIYOMO

  • Michango yazidi (1-7)

  • Ujenzi wa hema la ibada (8-38)

36  “Bezaleli atafanya kazi pamoja na Oholiabu na kila mtu mwenye ustadi* ambaye Yehova amempa hekima na uelewaji ili kujua jinsi ya kufanya utumishi wote mtakatifu kama Yehova alivyoamuru.”+  Kisha Musa akamwita Bezaleli na Oholiabu na kila mtu mwenye ustadi ambaye Yehova aliweka hekima moyoni mwake,+ kila mtu ambaye moyo wake ulimsukuma kujitolea kufanya kazi.+  Basi wakachukua kutoka kwa Musa mchango wote+ ambao Waisraeli walileta kwa ajili ya utumishi mtakatifu. Hata hivyo, watu wakaendelea kumletea matoleo ya hiari, asubuhi baada ya asubuhi.  Walipoanza kufanya kazi takatifu, mafundi wote wenye ustadi wakaja, mmoja baada ya mwingine,  nao walikuwa wakimwambia Musa: “Watu wanaleta vitu vingi sana kuliko vinavyohitajika kwa ajili ya kazi ambayo Yehova ameamuru ifanywe.”  Kwa hiyo Musa akaamuru kwamba tangazo litolewe kotekote kambini, likisema: “Wanaume na wanawake, msilete vitu zaidi kwa ajili ya mchango mtakatifu.” Basi watu wakazuiwa wasilete tena kitu chochote.  Vitu walivyoleta vilitosha kukamilisha kazi yote iliyopaswa kufanywa, tena vilizidi.  Kwa hiyo mafundi wote stadi+ walitengeneza hema la ibada+ kwa vitambaa kumi vya kitani bora kilichosokotwa, kwa nyuzi za bluu, sufu ya zambarau, na kitambaa cha rangi nyekundu; akavitarizi* kwa michoro ya makerubi.+  Kila kitambaa cha hema la ibada kilikuwa na urefu wa mikono 28* na upana wa mikono 4. Vitambaa vyote vilikuwa na ukubwa uleule. 10  Akaviunganisha pamoja vitambaa vitano vya hema, na pia akaviunganisha pamoja vile vitambaa vingine vitano. 11  Kisha akatengeneza vitanzi vya nyuzi za bluu kwenye upindo wa kitambaa cha mwisho. Naye akafanya vivyo hivyo kwenye upindo wa kitambaa kile kingine cha mwisho mahali ambapo vingeunganishwa. 12  Akatengeneza vitanzi 50 kwenye kitambaa kimoja na vitanzi vingine 50 kwenye upindo wa kitambaa cha pili ili vitanzi hivyo vielekeane vinapounganishwa. 13  Hatimaye, akatengeneza vibanio 50 vya dhahabu na kuviunganisha vitambaa hivyo pamoja kwa vibanio hivyo, basi hema la ibada likawa na kitambaa kimoja kizima. 14  Kisha akatengeneza vitambaa vya manyoya ya mbuzi vya kufunika hema hilo. Akatengeneza vitambaa 11 vya hema.+ 15  Kila kitambaa kilikuwa na urefu wa mikono 30 na upana wa mikono 4. Vitambaa vyote 11 vilikuwa na ukubwa uleule. 16  Kisha akaunganisha vitambaa vitano pamoja na vile vitambaa vingine sita pamoja. 17  Halafu akatengeneza vitanzi 50 kwenye upindo wa kitambaa cha kwanza, kwenye kipande cha mwisho kabisa, na vitanzi 50 kwenye upindo wa kitambaa cha pili, mahali vinapounganishwa. 18  Naye akatengeneza vibanio 50 vya shaba vya kuunganisha hema pamoja ili liwe na kitambaa kimoja kizima. 19  Akatengeneza kifuniko cha hema kwa kutumia ngozi za kondoo dume zilizotiwa rangi nyekundu na juu yake kifuniko cha ngozi za sili.+ 20  Kisha akatengeneza viunzi vya mbao za mshita+ vilivyo wima kwa ajili ya hema hilo.+ 21  Kila kiunzi kilikuwa na urefu wa mikono kumi na upana wa mkono mmoja na nusu. 22  Kila kiunzi kilikuwa na ndimi mbili* zilizounganishwa pamoja. Hivyo ndivyo alivyotengeneza viunzi vyote vya hema la ibada. 23  Kwa hiyo alitengeneza viunzi 20 kwa ajili ya upande wa kusini wa hema la ibada. 24  Kisha akatengeneza vikalio 40 vya fedha chini ya vile viunzi 20: vikalio viwili chini ya kiunzi kimoja pamoja na ndimi zake mbili na vikalio vingine viwili chini ya kila kiunzi kilichofuata pamoja na ndimi zake mbili.+ 25  Akatengeneza viunzi 20 upande wa pili wa hema, upande wa kaskazini 26  pamoja na vikalio vyake 40 vya fedha, vikalio viwili chini ya kiunzi kimoja na vikalio viwili chini ya kila kiunzi kilichofuata. 27  Akatengeneza viunzi sita sehemu ya nyuma ya hema la ibada, upande wa magharibi.+ 28  Naye akatengeneza viunzi viwili viwe mihimili miwili ya pembeni upande wa nyuma wa hema la ibada. 29  Katika pembe zote mbili kulikuwa na viunzi viwili kuanzia sehemu ya chini mpaka sehemu ya juu, kwenye pete ya kwanza. Hivyo ndivyo alivyotengeneza ile mihimili miwili ya pembeni. 30  Kwa ujumla kulikuwa na viunzi vinane na vikalio vyake 16 vya fedha, vikalio viwili chini ya kila kiunzi. 31  Kisha akatengeneza fito za mshita, fito tano kwa ajili ya viunzi vya upande mmoja wa hema la ibada+ 32  na fito tano kwa ajili ya viunzi vya upande wa pili wa hema la ibada na fito tano kwa ajili ya viunzi vya sehemu ya nyuma ya hema la ibada, upande wa magharibi. 33  Akatengeneza ufito katikati ya viunzi kutoka mwisho mmoja mpaka mwisho mwingine. 34  Akavifunika viunzi hivyo kwa dhahabu, akatengeneza pete za dhahabu ili zishikilie zile fito, naye akazifunika fito hizo kwa dhahabu.+ 35  Kisha akatengeneza pazia+ la nyuzi za bluu, sufu ya zambarau, kitambaa cha rangi nyekundu, na kitani bora kilichosokotwa. Akalitarizi+ kwa michoro ya makerubi.+ 36  Kisha akalitengenezea nguzo nne za mshita na kuzifunika kwa dhahabu, akatengeneza pia kulabu za dhahabu na vikalio vinne vya fedha kwa ajili ya nguzo hizo. 37  Halafu akatengeneza pazia la mlango wa hema kwa nyuzi za bluu, sufu ya zambarau, kitambaa cha rangi nyekundu, na kitani bora kilichosokotwa na kufumwa,+ 38  na pia nguzo zake tano na vibanio vyake. Akafunika kwa dhahabu sehemu ya juu ya nguzo hizo pamoja na kulabu* zake, lakini vikalio vyake vitano vilikuwa vya shaba.

Maelezo ya Chini

Au “mwenye hekima moyoni.”
Inaonekana ni Bezaleli.
Mkono mmoja ulilingana na sentimita 44.5 (inchi 17.5). Angalia Nyongeza B14.
Au “mihimili miwili.”
Au “pete; vitanzi; vibanio” vya kushikia.