Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Chagua lugha Kiswahili

Esta 4:1-17

MUHTASARI WA YALIYOMO

  • Mordekai aomboleza (1-5)

  • Mordekai amwomba Esta aingilie kati (6-17)

4  Mordekai+ alipojua mambo yote yaliyofanywa+ akayararua mavazi yake, akavaa nguo za magunia na kujimwagia majivu. Kisha akaenda katikati ya jiji, akilia kwa sauti kubwa na kwa uchungu.  Akaenda karibu na lango la mfalme, kwa maana hakuna mtu aliyepaswa kuingia katika lango la mfalme akiwa amevaa nguo za magunia.  Katika kila mkoa*+ ambako neno la mfalme na amri yake ilifika, kulikuwa na maombolezo makubwa miongoni mwa Wayahudi, pia walifunga,+ wakalia, na kuomboleza. Wengi wao walilala chini katika majivu wakiwa wamevaa nguo za magunia.+  Watumishi wa kike na matowashi wa Esta walipokuja na kumwambia habari hiyo, Malkia alifadhaika sana. Akaagiza Mordekai apelekewe mavazi ili avae badala ya nguo za magunia, lakini Mordekai akayakataa.  Ndipo Esta akamwita Hathaki, mmoja wa matowashi wa mfalme, aliyechaguliwa na mfalme kumhudumia Esta, naye akamwagiza amuulize Mordekai maana ya jambo hilo na kilichokuwa kikiendelea.  Basi Hathaki akatoka na kwenda kwa Mordekai kwenye uwanja wa jiji mbele ya lango la mfalme.  Mordekai akamwambia yote yaliyompata na kiasi kamili cha pesa+ ambacho Hamani alikuwa ameahidi kulipa katika hazina ya mfalme ili Wayahudi waangamizwe.+  Pia akampa nakala ya amri iliyoandikwa na kutolewa Shushani*+ kwamba waangamizwe. Hathaki alipaswa kumwonyesha Esta na kumfafanulia+ na kumwambia aende kwa mfalme kumwomba kibali na kumsihi moja kwa moja kwa niaba ya Wayahudi.  Basi Hathaki akarudi na kumwambia Esta mambo yote aliyosema Mordekai. 10  Kisha Esta akamwambia Hathaki amwambie hivi Mordekai:+ 11  “Watumishi wote wa mfalme na watu wa mikoa ya* mfalme wanajua kuna sheria moja tu kwa mwanamume au mwanamke yeyote atakayeingia katika ua wa ndani wa mfalme+ bila kuitwa: Mtu huyo anapaswa kuuawa; ataishi ikiwa tu mfalme atamnyooshea fimbo yake ya ufalme ya dhahabu.+ Nami sijaitwa kuingia kwa mfalme kwa siku 30 sasa.” 12  Mordekai alipopata ujumbe wa Esta, 13  akamjibu hivi Esta: “Usidhani kwamba kwa kuwa unaishi katika makao ya mfalme unaweza kuokoka kati ya Wayahudi wengine wote. 14  Kwa maana ukikaa kimya wakati huu, Wayahudi watapata msaada na ukombozi kutoka chanzo kingine,+ lakini wewe na nyumba ya baba yako mtaangamia. Ni nani ajuaye ikiwa umepata cheo cha umalkia kwa ajili ya wakati kama huu?”+ 15  Kisha Esta akamjibu hivi Mordekai: 16  “Nenda, wakusanye Wayahudi wote walio Shushani* na mfunge+ kwa ajili yangu. Msile wala kunywa kwa siku tatu,+ usiku na mchana. Mimi pia pamoja na watumishi wangu wa kike tutafunga. Kisha nitaingia kwa mfalme, jambo ambalo ni kinyume cha sheria, na ikiwa nitaangamia, acha niangamie.” 17  Basi Mordekai akaenda zake na kufanya mambo yote ambayo Esta alimwagiza afanye.

Maelezo ya Chini

Au “wilaya ya utawala.”
Au “Susa.”
Au “wilaya za utawala za.”
Au “Susa.”