Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mashahidi wa Yehova

Chagua lugha Kiswahili

Luka 15:1-32

15  Sasa wakusanya-kodi+ wote na watenda-dhambi+ wakamkaribia ili wamsikie.  Kwa sababu hiyo Mafarisayo na pia waandishi wakanung’unika, wakisema: “Mtu huyu hukaribisha watenda-dhambi na hula pamoja nao.”+  Ndipo akawaambia mfano huu, akisema:  “Ni nani kati yenu mwenye kondoo 100, anapopoteza mmoja wao, hatawaacha wale 99 nyikani na kwenda kumtafuta aliyepotea mpaka ampate?+  Na akiisha kumpata humweka juu ya mabega yake na kushangilia.+  Naye anapofika nyumbani huwaita rafiki zake na jirani zake pamoja, akiwaambia, ‘Shangilieni pamoja nami, kwa sababu nimempata kondoo wangu aliyekuwa amepotea.’+  Mimi ninawaambia ninyi kwamba ndivyo kutakavyokuwa na shangwe zaidi mbinguni juu ya mtenda-dhambi mmoja anayetubu+ kuliko juu ya waadilifu 99 ambao hawahitaji kutubu.+  “Au ni mwanamke gani mwenye sarafu kumi za drakma, akipoteza sarafu moja ya drakma, hawashi taa na kufagia nyumba yake na kutafuta kwa uangalifu mpaka aipate?  Naye akiisha kuipata huwaita wanawake walio rafiki zake na jirani zake pamoja, akisema, ‘Shangilieni pamoja nami, kwa sababu nimeipata sarafu ya drakma niliyoipoteza.’ 10  Hivyo, ninawaambia ninyi, hivyo ndivyo shangwe hutokea kati ya malaika za Mungu juu ya mtenda-dhambi mmoja anayetubu.”+ 11  Ndipo akasema: “Mtu fulani alikuwa na wana wawili.+ 12  Na yule mdogo kati yao akamwambia baba yake, ‘Baba, nipe sehemu ya mali iliyo fungu langu.’+ Ndipo akawagawia mali+ yake. 13  Baadaye, baada ya siku zisizokuwa nyingi, mwana huyo mdogo akakusanya pamoja vitu vyote akasafiri ng’ambo na kwenda nchi ya mbali, na huko akatapanya mali yake kwa kuishi maisha ya upotovu.+ 14  Alipokuwa ametumia kila kitu, njaa kali ikatokea kotekote katika nchi hiyo, naye akaanza kuwa na uhitaji. 15  Hata alienda na kujishikamanisha na mmoja wa raia wa nchi hiyo, naye akamtuma aende katika mashamba yake akachunge nguruwe.+ 16  Naye alikuwa akitamani kujishibisha kwa maganda ya karuba ambayo nguruwe hao walikuwa wakila, wala hakuna mtu yeyote aliyekuwa akimpa kitu chochote.+ 17  “Aliporudiwa na fahamu zake, akasema, ‘Ni watu wangapi aliowakodi baba yangu ambao wana mkate kwa wingi, na huku mimi ninaangamia hapa kwa njaa kali! 18  Nitaondoka nifunge safari+ kwenda kwa baba yangu na kumwambia: “Baba nimetenda dhambi juu ya mbingu na juu yako wewe.+ 19  Sistahili tena kuitwa mwana wako. Unifanye kama mmoja wa watu wako waliokodiwa.” ’ 20  Kwa hiyo akaondoka akamwendea baba yake. Alipokuwa angali mbali, baba yake akamwona, akamsikitikia, akakimbia, akamwangukia shingoni na kumbusu kwa wororo. 21  Ndipo yule mwana akamwambia, ‘Baba, nimetenda dhambi juu ya mbingu na juu yako,+ sistahili tena kuitwa mwana wako. Unifanye niwe kama mmoja wa watu wako waliokodiwa.’+ 22  Lakini baba huyo akawaambia watumwa wake, ‘Upesi! leteni kanzu, iliyo bora zaidi, mkamvike,+ na mtie pete+ mkononi mwake na viatu miguuni mwake. 23  Nanyi leteni ng’ombe-dume mchanga aliyenoneshwa,+ mchinjeni na tule na kujifurahisha, 24  kwa sababu huyu mwanangu alikuwa amekufa naye yuko hai+ sasa; alikuwa amepotea naye amepatikana.’ Nao wakaanza kujifurahisha. 25  “Sasa mwana wake mkubwa+ alikuwa katika shamba; naye alipoikaribia nyumba akasikia sauti za muziki na dansi. 26  Kwa hiyo akamwita mmoja wa watumishi, akauliza maana ya mambo hayo. 27  Huyo akamwambia, ‘Ndugu+ yako amekuja, na baba+ yako amechinja ng’ombe-dume mchanga aliyenoneshwa, kwa sababu alimpata tena akiwa na afya njema.’ 28  Lakini akawa na ghadhabu na hakutaka kuingia. Ndipo baba yake akatoka, akaanza kumsihi sana.+ 29  Akamjibu, akamwambia baba yake, ‘Nimekutumikia kwa miaka mingi sana wala sijavunja amri yako hata mara moja, hata hivyo hujanipa mwana-mbuzi hata mara moja ili mimi nijifurahishe pamoja na rafiki zangu.+ 30  Lakini mara tu alipofika huyu mwana wako+ aliyekula pamoja na makahaba+ mali yako, ulimchinjia ng’ombe-dume mchanga aliyenoneshwa.’+ 31  Ndipo akamwambia, ‘Mwanangu, wewe umekuwa pamoja nami sikuzote, na vitu vyangu vyote ni vyako;+ 32  lakini ilitupasa tu kujifurahisha na kushangilia, kwa sababu huyu ndugu yako alikuwa amekufa naye yuko hai sasa, alikuwa amepotea naye amepatikana.’ ”+

Maelezo ya Chini