Hamia kwenye habari

Mashahidi wa Yehova

Chagua lugha Kiswahili

MACHI 17, 2014
UTURUKI

Uturuki Haitafuata Viwango vya Ulaya Kuhusu Kukataa Utumishi wa Kijeshi kwa Sababu ya Dhamiri

Uturuki Haitafuata Viwango vya Ulaya Kuhusu Kukataa Utumishi wa Kijeshi kwa Sababu ya Dhamiri

“Kila raia wa Uturuki anazaliwa akiwa mwanajeshi.” Msemo huo hufundishwa shuleni, hutajwa katika hotuba za wanasiasa, na kukaziwa tena na tena kwa wanaume wanaojiunga na jeshi. Raia wote wa Uturuki ambao ni wanaume wanapaswa kujiunga na jeshi, na mtu anaposajiliwa jeshini, watu hushangilia sana. Kwa hiyo, si jambo la kushangaza kuona serikali ya Uturuki ikikataa kutambua haki za msingi za wale wanaokataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri.

Uturuki ni mojawapo ya nchi chache katika Baraza la Ulaya ambazo hazitambui haki za wanaokataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri

Hata hivyo, nchi ya Uturuki ni mwanachama wa Baraza la Ulaya, na kwa kuwa imekubali Mkataba wa Ulaya Kuhusu Haki za Kibinadamu uwe sehemu ya sheria zake za nchi, basi lazima nchi hiyo iunge mkono viwango vya Ulaya. Tangu uamuzi ulipotolewa na Baraza Kuu la Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) kuhusiana na kesi ya Bayatyan dhidi ya serikali ya Armenia, serikali ya Uturuki ina wajibu rasmi mbele ya Baraza la Ulaya, wajibu wa kutambua na kuheshimu haki za wale wanaokataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Kwa sababu Uturuki imekataa kufuata viwango hivyo, basi wale wanaokataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri, wanaendelea kutaabika.

Kwa kipindi cha miaka 10, wanaume 55 ambao ni Mashahidi wa Yehova wametuma maombi kwa serikali ya Uturuki wakiiomba itambue haki yao ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Kwa kuwa maombi yao hayajakubaliwa, wameshtakiwa mara nyingi, wametozwa faini kubwa, na wengine hata wamehukumiwa miaka mingi gerezani. Kwa sasa, vijana 15 Mashahidi nchini Uturuki wameshtakiwa kwa mara nyingine kwa sababu ya kukataa kujiunga na jeshi.

‘Ninapaswa Kufuata Dhamiri Yangu’

“Siamini kwamba Nchi yenye mamlaka na nguvu inapaswa kunilazimisha nitende kinyume na dhamiri yangu iliyozoezwa na Biblia na pia maneno yaliyoongozwa na roho ya Mungu katika kitabu cha Isaya 2:4, [maneno ambayo] naamini ninapaswa kuyatii.” Maneno ya andiko hilo yanayojulikana sana yaliyochongwa kwenye jiwe mbele ya makao makuu ya shirika la Umoja wa Mataifa jijini New York City, yanataja waziwazi kwamba watu ambao hawapendi vita ‘wangefua mapanga yao yawe majembe na hawangejifunza vita tena.’ Kwa maneno hayo Feti Demirtaş, raia wa Uturuki ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 25 alieleza ni kwa nini alikuwa tayari kufungwa gerezani kuliko kutumikia jeshini. Akiwa Shahidi wa Yehova, Feti anaamini kabisa kwamba anapaswa kufuata dhamiri yake iliyozoezwa na Biblia. Kwa sababu hiyo, Feti ameshtakiwa mara kumi na kufungwa gerezani kwa mwaka mmoja na nusu.

Alipokamatwa mara ya kwanza, sajenti mmoja alimwamrisha avae sare ya kijeshi lakini Feti alikataa katakata—aliamua kutii dhamiri yake iliyozoezwa na Biblia. Kisha mkuu wa kituo hicho cha kijeshi alimchukua na kumpeleka mbele ya wanaume 400 kisha akamwamrisha avae sare hiyo. Kwa mara nyingine tena, alikataa. Alipofungwa gerezani mara ya kwanza, Feti alitendewa ukatili—alitukanwa, akapigwa mateke kichwani, mabegani, miguuni na hata akapigwa makofi usoni na walinzi wa gereza.

Alipokamatwa kwa mara ya tano na kufungwa mnamo Aprili 2006, walinzi wa gereza walimlazimisha Feti avue nguo zote na abaki na nguo za ndani tu ili avae sare ya jeshi. Alipokataa kuvaa nguo hizo, walinzi hao walimpeleka katika kambi ya kuwatia wafungwa nidhamu na kumweka huko kwa siku nne. Katika jitihada za kumfanya alegeze msimamo wake, waliifunga mikono yake kwenye ufito wa chuma wa kitanda chake wakati wa usiku na wakati wa mchana wakamfunga kwenye chumba cha gereza. Feti anasema, “Niliogopa sana mchana kutwa na daima singeweza kupata usingizi usiku kwa sababu sikujua ni mateso ya aina gani yangefuata. Ingawa niliumia sana kihisia kwa sababu ya jinsi nilivyotendewa, nilikuwa nimeazimia kufuata dhamiri yangu.”

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu Yaingilia Kati Suala Hilo

Mwaka wa 2007 Feti Demirtaş aliwasilisha kesi yake kwenye Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR). Katika kesi hiyo alisema kwamba serikali ya Uturuki ilikiuka haki zake kwa kumhukumu adhabu ya kufungwa gerezani kama mtu aliyekataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Januari 17, 2012, Mahakama hiyo ilitoa uamuzi uliounga mkono kwamba Feti alitendewa kwa njia isiyo ya kibinadamu na alishushiwa heshima, mambo ambayo yalimsababishia maumivu makali na mateso. Zaidi ya hilo, Mahakama hiyo ilithibitisha kwamba haki ya kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya imani ya kidini ni jambo linalotetewa na kulindwa na Mkataba wa Ulaya Kuhusu Haki za Kibinadamu. *

Kufuatia uamuzi huo wa wazi uliotolewa na Mahakama ya ECHR, Feti alitarajia kwamba sasa serikali ya Uturuki ingeacha kumshtaki mara kwa mara. Hata serikali ya Uturuki ilimlipa fidia ya euro 20,000 kama ilivyokuwa imeamriwa na Mahakama ya ECHR. Lakini miezi minne tu baada ya uamuzi huo kutolewa na ECHR katika kesi hiyo ya Feti Demirtaş dhidi ya serikali ya Uturuki, Mahakama ya Jeshi la Uturuki ilimhukumu Feti miezi miwili na nusu gerezani kwa kukataa utumishi wa kijeshi. Feti alikata rufani ambayo bado haijashughulikiwa na Mahakama ya Jeshi.

Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu Inaunga Mkono Kukataa Utumishi wa Kijeshi kwa Sababu ya Dhamiri

Kwa kuongezea, Serikali ya Uturuki imepuuza maagizo ya karibuni kutoka kwa Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu. Mwaka wa 2008 Mashahidi wawili, Cenk Atasoy na Arda Sarkut, waliwasilisha malalamishi yao kwa Kamati hiyo, wakisema kwamba serikali ya Uturuki ilikiuka haki zao kwa kuwashtaki mara kwa mara kwa kuwa walikataa utumishi wa kijeshi. Maoni ya Kamati hiyo yaliyochapishwa Machi 29, 2012, yanasema kwamba “kukataa [kwa wanaume hao] kujiandikisha jeshini kunatokana na imani yao ya kidini” na kwamba “kushtakiwa kwao na kuhukumiwa kufungwa gerezani ni sawa na kukiuka uhuru wao wa dhamiri, jambo ambalo linakiuka kifungu cha 18, fungu la 1 la [Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na za Kisiasa].”

Serikali ya Uturuki imetendaje baada ya kupata maagizo hayo ya wazi? Serikali hiyo inawataka wanaume hao wawili waliokataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri waripoti kwa ajili ya utumishi wa kijeshi kila baada ya miezi minne * la sivyo watashtakiwa na kutozwa faini kubwa.

Mashahidi wa Yehova nchini Uturuki wameazimia kuishi kulingana na amri ya Biblia inayosema kwamba wanapaswa kuwapenda wanadamu wenzao. Wenye mamlaka nchini Uturuki wanapowaambia wajiunge na jeshi, kila Shahidi ana jukumu la kibinafsi la kuamua jinsi atakavyofanya. Feti Demirtaş na Mashahidi wengine wameazimia kwamba hawatabeba silaha kwa sababu kwa kufanya hivyo watakuwa wakivunja amri ya Biblia na watakuwa wakitenda kinyume na dhamiri zao.

Vijana hao wanatarajia kwamba serikali yao itaheshimu mikataba ya kisheria ambayo nchi yao inatarajiwa kutekeleza. Serikali ya Uturuki inatarajiwa kufuata maamuzi yaliyotolewa na Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu na Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu, kwamba inapaswa kutambua haki ya wale ambao dhamiri yao inawakataza kutekeleza utumishi wa kijeshi. Hadi itakapofanya hivyo, serikali ya Uturuki itaendelea kutenda kinyume na maoni ya Baraza la Ulaya kwa kuvunja haki hii ya msingi ya kibinadamu.

^ fu. 10 Haikuwa mara ya kwanza kwa Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu kutoa uamuzi kama huo dhidi ya serikali ya Uturuki kuhusiana na suala la kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Mnamo Novemba 2011 Mahakama hiyo ilitoa uamuzi uliomuunga mkono Shahidi nchini Uturuki anayeitwa, Yunus Erçep. Katika kipindi cha miaka 14, Yunus Erçep alikuwa ameshtakiwa mahakamani mara 41 kwa sababu ya kukataa kujiunga na jeshi.

^ fu. 14 Hivi karibuni serikali iliamua kwamba wanaume watakuwa wakiitwa jeshini kila baada ya miezi mitatu.