Mashahidi wa Yehova wamekuwepo nchini Uturuki tangu mwaka 1931. Wamekabili mateso kwa sababu ya imani yao mpaka mwishoni mwa miaka ya 1980. Katika miaka iliyofuata, serikali ilipunguza mateso na iliwaruhusu Mashahidi kufanya ibada zao, lakini ilikataa kuwasajili kisheria. Hali ilibadilika Julai 2007, mahakama ya Uturuki ilipotoa uamuzi unaowaunga mkono Mashahidi na kufanya wasajiliwe rasmi. Sasa Mashahidi wa Yehova wanaweza kufanya ibada na shughuli za dini kwa uhuru.

Hata hivyo serikali ya Uturuki haitambui haki ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Kwa miaka mingi Mashahidi wa Yehova waliokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri wameitwa mara nyingi ili wajiunge na jeshi, wameteswa, wametozwa faini kubwa na kufungwa. Tangu mwaka 2011, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Binadamu (ECHR) imetoa maamuzi ya kesi tatu na kuwaunga mkono Mashahidi, na mwaka 2012, Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ilitoa uamuzi unaowaunga mkono Mashahidi. Hata hivyo, bado Uturuki inaendelea kuwatesa Mashahidi vijana wanaokataa kujiunga na jeshi.

Mwaka 2003, sheria za majimbo zilirekebishwa na kuwaruhusu watu ambao si Waislamu wajenge na kumiliki majengo ya ibada. Hata hivyo, manispaa na mahakama zimekataa kutambua Majumba ya Ufalme ya Mashahidi wa Yehova kama “majengo ya ibada.” Tayari kesi mbili kuhusu jambo hilo zimepelekwa kwenye mahakama ya Ulaya (ECHR).