Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

Kituo cha Usimamizi cha Mashahidi wa Yehova nchini Urusi

APRILI 27, 2016
URUSI

Onyo Lilitolewa Dhidi ya Makao Makuu ya Mashahidi Nchini Urusi Latishia Uhuru wa Ibada

Onyo Lilitolewa Dhidi ya Makao Makuu ya Mashahidi Nchini Urusi Latishia Uhuru wa Ibada

Wenye mamlaka nchini Urusi wamechukua hatua nyingine kubwa ya kuwakandamiza Mashahidi. Mpango huo unaungwa mkono na serikali. Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu imetishia kufunga Kituo cha Usimamizi cha Mashahidi wa Yehova nchini Urusi kwa madai kwamba kinafanya “shughuli zenye msimamo mkali.” Katika barua ya ofisi hiyo ya Machi 2, 2016, Kaimu Mwendesha Mashtaka Mkuu V. Ya. Grin alikiagiza Kituo cha Usimamizi kiondoe “ukiukwaji” wote wa sheria katika kipindi cha miezi miwili.

Onyo hilo linalenga kuendeleza kampeni ya Urusi ya kuwashushia heshima Mashahidi na kuondoa uhuru wao wa ibada. Ikiwa Kituo cha Usimamizi kitafungwa, basi kitajumuishwa katika orodha ya mashirika yenye msimamo mkali na mali zake zote zitataifishwa. Kituo hicho kinashirikiana na mashirika ya kisheria 406 ya Mashahidi wa Yehova na pia makutaniko 2500. Ikiwa Kituo hicho kitafungwa, basi mashirika hayo na kisheria na makutaniko huenda yatafungwa. Matokeo ni kwamba Mashahidi wa Yehova nchini Urusi wanaweza kupotezaMajumba ya Ufalme (majengo ya ibada). Hatimaye kufungwa kwa Kituo cha Usimamizi kunaweza kupoteza haki ya Mashahidi ya kushiriki katika shughuli zao za dini.

Mipango ya Urusi ya kuwashambulia Mashahidi wa Yehova inayotegemea uthibitisho wa uwongo na kutumiwa vibaya kimakusudi kwa Sheria ya Serikali ya Urusi ya Kupambana na Vikundi Vyenye Msimamo Mkali. Mwaka 2015, Kamati ya Umoja ya Mataifa ya Haki za Binadamu ilionyesha hofu yake “kuhusu ripoti nyingi zinaonyesha kwamba sheria [ya Shughuli Zenye Msimamo Mkali] imetumiwa hasa kuzuia uhuru wa kujieleza. . . na uhuru wa kuabudu, kuwalenga, Mashahidi wa Yehova pamoja na vikundi vingine.” *

Mashahidi wa Yehova ni dini inayojulikana sana duniani pote. Wanafurahia uhuru wa ibada katika nchi za kidemokrasia pamoja na nchi zote ambazo ni wanachama wa Umoja wa Ulaya. Nchi ya Urusi pekee inawanyima uhuru. Kampeni za nchi hiyo zinazolenga ibada inayofanywa kwa amani ya Mashahidi zimeendelea kuongezeka hatua kwa hatua tangu katikati ya miaka ya 1990. Jitihada za kukandamiza uhuru wa ibada zimeongezeka zaidi baada ya kutungwa kwa sheria ya msimamo mkali na sheria hiyo inatumiwa vibaya kama chombo cha ukandamizaji.

Maana ya Shughuli Zinazochochea Msimamo Mkali Kutokuwa Wazi—Chanzo cha Ukandamizaji

Mwaka 2002, Urusi iliunda Sheria ya Kupambana na Shughuli Zinazochochea Msimamo Mkali ya Serikali ya Urusi ili kukabiliana na matukio ya kigaidi. Hata hivyo, tangu sheria hiyo ianzishwe, ufafanuzi usio wazi wa sheria hiyo ya shughuli zenye msimamo mkali umezua hofu kwamba maofisa wa Urusi wangeitumia vibaya kama njia ya ukandamizaji. Mwaka 2003, Kamati ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia Haki za Binadamu iliishauri Urusi iboreshe sheria ya shughuli zenye msimamo mkali na maana ya sheria hiyo iwe wazi ili “isitokeze fursa yoyote ya kutumia vibaya sheria hiyo.” *

Badala ya kuiboresha, sheria hiyo iliongezewa matumizi. Mwaka 2012, Baraza la Bunge la Ulaya lilisema hivi: “Katika sheria ya awali, msimamo mkali ulitafsiriwa kifupi kuwa ni ‘kuchochea migogoro ya kijamii, kikabila, kitaifa au kidini inayohusisha jeuri au uchochezi wa jeuri.’ Marekebisho ya sheria hiyo ya mwaka 2006 yameondoa kipengele kinachosema ‘inayohusisha jeuri au uchochezi wa jeuri.’ . . . Kutoeleweka kwa maana ya “msimamo mkali” kumechangia kutokea kwa matendo yasiyo ya haki yanayofanywa na wenye mamlaka.”

Hofu ya kwamba sheria hiyo ingetumiwa isivyo haki ilikuwa na msingi. Mwaka 2007, Ofisi ya Mwendesha-Mashtaka Mkuu ilitoa amri ya kuanza kuwachunguza Mashahidi wa Yehova. Kaimu Mwendesha Mashtaka Mkuu V. Ya. Grin—ambaye alitia sahihi onyo la hivi karibuni lililotumwa kwenye Kituo cha Usimamizi—ndiye aliyetuma barua rasmi iliyowaamuru waendesha mashtaka wote waanze kuwachunguza Mashahidi wa Yehova. Barua hiyo ilionyesha kwa mara ya kwanza kwamba kampeni dhidi ya Mashahidi ingekuwa ya kitaifa na ingeendeshwa na ofisi moja.

Ingawa Mashahidi hawajihusishi na aina yoyote ya uhalifu, waendesha-mashtaka katika nchi nzima ya Urusi waliwaandama na tangu mwaka 2007 matukio zaidi ya 500 ya kuchunguzwa kwa Mashahidi yalitokea. Ripoti ya Baraza la Bunge la Ulaya ya 2012 ilisema hivi: “Sheria ya Urusi ya ‘kupambana na shughuli zenye msimamo mkali’ (Sheria ya Msimamo Mkali), iliyoanzishwa mwaka 2002, imetumiwa vibaya kama silaha dhidi ya utendaji wa baadhi ya dini, hasa Mashahidi wa Yehova ambao idadi yao ni 162,000 nchini Urusi. Matumizi hayo mabaya ya sheria hiyo yameongezeka tangu sheria hiyo ifanyiwe marekebisho mwaka 2006.” *

“Sheria ya Urusi ya ‘kupambana na shughuli zenye msimamo mkali’ imetumiwa vibaya dhidi ya utendaji wa dini fulani, hasa ya Mashahidi wa Yehova.”—Baraza la Bunge la Ulaya

Kupiga Marufuku Machapisho—Ni Mwanzo wa Ukandamizaji

Kabla ya kutimiza malengo yao kuelekea Kituo cha Usimamizi kilichopo karibu na jiji la St. Petersburg, wenye mamlaka walianza kwa kuchunguza machapisho ya Mashahidi. Waendesha-Mashtaka jijini Taganrog na Gorno-Altaysk walifungua kesi mahakamani wakidai machapisho kadhaa ya Mashahidi yatangazwe kuwa yanachochea “msimamo mkali” na yawekwe kwenye Orodha ya Serikali ya Vitabu na Habari Zinazowachochea Watu Kuwa na Msimamo Mkali wa Kidini.

Waendesha-Mashtaka walidai kwamba walikuwa na ushahidi kutoka kwa waliodai kuwa ni wataalamu hivyo walishinda katika kesi hiyo kwenye majiji hayo ya Taganrog na Gorno-Altaysk mwaka 2009 na 2010. Uamuzi huo uliotolewa katika majiji mawili, uliosababisha machapisho yetu 52 yapigwe marufuku, umekuwa chanzo cha kufunguliwa kwa kesi nyingi dhidi ya Mashahidi wa Yehova. Wenye mamlaka kwenye maeneo mengine ya nchi wameiga mambo yaliyofanywa Taganrog na Gorno-Altaysk. Kufikia sasa, mahakama zimeagiza machapisho 87 ya Mashahidi yawekwe kwenye orodha ya Vitabu na Habari Zinazowachochea Watu Kuwa na Msimamo Mkali wa Kidini.

Mashahidi wanapinga maamuzi yaliyotolewa katika majiji ya Taganrog na Gorno-Altaysk pamoja na mahakama nyingine za Urusi zilizotangaza kwamba machapisho yao yanachochea msimamo mkali. Wamefungua kesi 28 kwenye Mahakama ya Ulaya ya Haki za Binadamu (ECHR) ili kutoa malalamiko kuhusu mashtaka ya kuchochea msimamo mkali na ukosefu wa haki unaohusiana na matumizi mabaya ya sheria hiyo. Tunatarajia hivi karibuni Mahakama hiyo itatoa maamuzi ya kesi 22. Serikali ya Urusi imejitetea katika Mahakama hiyo ya Ulaya na kukubali kwamba machapisho ya Mashahidi yaliyopo kwenye orodha ya Vitabu na Habari Zinazowachochea Watu Kuwa na Msimamo Mkali wa Kidini “hayawachochei watu moja kwa moja wafanye jeuri au kuchochea jeuri.”

Uhuru wa Kusema Washambuliwa

Wenye mamlaka nchini Urusi walipofanikiwa kufanya machapisho yetu yatangazwe kwamba yanachochea “msimamo mkali” kupitia mahakama, walipata sababu halali ya kuandaa mashambulizi dhidi ya Mashahidi na kuzuia zaidi uhuru wa kusema wa Mashahidi.

  • Mwaka 2010, wenye mamlaka walikataa kuwapa Mashahidi kibali cha kuingiza na kusambaza magazeti ya Mnara wa Mlinzi na Amkeni! nchini Urusi. Gazeti la Mnara wa Mlinzi limechapishwa tangu mwaka 1879. Machapisho hayo yote yanasambazwa zaidi kuliko gazeti lolote lingine ulimwenguni.

  • Tangu Machi 2015, maofisa wamekataa kuruhusu kuingizwa nchini kwa chapisho lolote la dini ya Mashahidi wa Yehova.

  • Tangu Julai 2015 tovuti rasmi ya Mashahidi, jw.org, ilipigwa marufuku nchini Urusi, na kufanya iwe vigumu kwa mtu yeyote katika nchi hiyo kupata machapisho yaliyopatikana kwenye intaneti. Kuwaeleza watu watembelee tovuti hiyo ni kosa la jinai.

  • Mwanzoni mwa mwaka 2016, mwendesha-mashtaka katika mji wa Vyborg alifungua kesi akidai kwamba Biblia Takatifu Tafsiri ya Ulimwengu Mpya, ambayo huchapishwa na Mashahidi itangazwe kuwa inachochea “msimamo mkali.”

Licha ya kuzuia uhuru wa kusema, wenye mamlaka wametumia machapisho yaliyowekwa kwenye orodha ya Vitabu na Habari Zinazowachochea Watu Kuwa na Msimamo Mkali wa Kidini kama msingi wa kuchunguza mashirika ya kisheria ya Mashahidi na kuwafungulia mashtaka Shahidi mmoja mmoja kwa sababu ya utendaji wao wa dini.

Mfululizo wa Ukaguzi na Kutiwa Hatiani

Chapisho likiwekwa kwenye orodha ya Vitabu na Habari Zinazowachochea Watu Kuwa na Msimamo Mkali wa Kidini, linapigwa marufuku kusambazwa kwa watu, kuchapishwa au kuhifadhiwa kwa kusudi la kusambaza. Wenye mamlaka katika maeneo mbalimbali wametumia amri hiyo ya mahakama kuchunguza nyumba nyingi za Mashahidi na Majumba yao ya Ufalme ili watafute machapisho ya dini yaliyopigwa marufuku.

Mara nyingi ukaguzi huo unafanywa kwa kutozingatia haki na wenye mamlaka wanafanya mambo kinyume na sheria kwa kupora vitu vya kibinafsi pamoja na machapisho yote ya dini hata yale yasiyo katika orodha ya machapisho yaliyopigwa marufuku.

  • Agosti 2010, maofisa 30 hivi wa polisi wakiwa na silaha jijini Yoshkar-Ola, walivuruga ibada. Maofisa hao waliwakaba baadhi na Mashahidi na kuikunja mikono kwa nyuma kama wanataka kuwafunga pingu. Maofisa hao walifanya ukaguzi na kuchukua vitu vyao vya kibinafsi, hati na machapisho.

  • Julai 2012, katika Jamhuri ya Karelia, maofisa wa polisi wakiwa wamebeba silaha na wakiwa wameziba nyuso walimshambulia Shahidi kwenye eneo la umma na kuinamisha kichwa chake chini katika sehemu ya mbele ya gari na kuikunja mikono yake kwa nyuma. Maofisa walikagua nyumba za Mashahidi kadhaa na kuchukua vitu vyao vya kibinafsi na machapisho ya dini bila kujali ikiwa hayakuwa katika orodha ya machapisho yaliyopigwa marufuku.

  • Machi 2016, huko Jamhuri ya Tatarstan, polisi walivamia Jumba la Ufalme na baadhi ya Nyumba za Mashahidi. Walichukua vifaa vya kompyuta, kompyuta zao za mkononi na machapisho ya dini.

Video inayoonyesha “ushahidi” uliopandikizwa wa machapisho yaliyopigwa marufuku

Wenye mamlaka waliweka kisiri kamera za kurekodi video katika nyumba za Mashahidi na Majumba ya Ufalme. Wanarekodi mawasiliano ya simu ya Mashahidi, wanachunguza barua pepe zao na kutumia njia nyingine zisizo za haki ili kukusanya habari. Wakiwa na lengo la kuthibitisha madai yao baadhi ya polisi hata waliweka kwa siri machapisho yaliyopigwa marufuku kwenye Majumba ya Ufalme. Kwa sababu ya matukio hayo Mashahidi wengi wamefunguliwa kesi za uhalifu.

Kufungwa kwa Mashirika ya Kisheria Kumesababisha Mashtaka ya Makosa ya Jinai

Zaidi ya kufungulia kesi Shahidi mmoja mmoja, wenye mamlaka wametumia machapisho yaliyopigwa marufuku ambayo waliyaingiza kisiri katika Majumba ya Ufalme kama “uthibitisho” wa kuyafunga mashirika ya kisheria ya Mashahidi. * Mashirika ya kisheria yanapopigwa marufuku kwa sababu ya “msimamo mkali” Serikali inataifisha mali zake. Matokeo ni kwamba Mashahidi wanapoteza majengo yao ya ibada. Jambo hilo tayari limetokea jijiniTaganrog na Samara. Wenye mamlaka katika majiji mengine wanaiga mambo yaliyofanywa katika majiji hayo.

Mashahidi wa Yehova wakiwa mahakamani jijini Taganrog, Urusi

Shirika la kisheria lilipopigwa marufuku jijini Taganrog, walichukua hatua isiyo ya haki kwa kulinganisha kukutanika kwa ajili ya kusali na kufanya ibada kuwa sawa na “ kuendeleza kinyume cha sheria utendaji wa shirika la dini lililopigwa marufuku.” Kwa kutumia mbinu hiyo wenye mamlaka jijini Taganrog wamewatia hatiani Mashahidi wa Yehova 16 kwa sababu tu ya kufanya kwa amani ibada. Ibada ileile ambayo hufanywa na Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote. Kwa mara ya kwanza tangu kuvunjika kwa Muungano wa Sovieti, ni kosa la jinai jijini Taganrog kwa Shahidi wa Yehova kufanya ibada yake.

Onyo Dhidi ya Kituo cha Usimamizi ni Dalili ya Hatari

Eneo la nje la Kituo cha Usimamizi

Ikiwa maofisa watakizuia Kituo hicho, watakifunga na kupiga marufuku utendaji wake katika nchi nzima ya Urusi. Kama waabudu wenzao wa Taganrog, Mashahidi wa Yehova nchi nzima watashtakiwa kuwa ni wahalifu ikiwa watahudhuria mikutano ya Kikristo au kuwaeleza wengine kuhusu imani yao. Mashahidi wa Yehova nchini Urusi wanaweza kujikuta katika hali itakayowaruhusu wawe huru kuamini chochote wanachotaka lakini wasiruhusiwe kushiriki ibada pamoja na waabudu wenzao. *

Philip Brumley, Mwakilishi wa Ofisi ya Mashahidi wa Yehova, alisema hivi: “Mashahidi wa Yehova kuonwa kama kikundi chenye msimamo mkali na machapisho yao kuwekwa kwenye orodha machapisho yanayochochea ugaidi si haki kabisa. Wenye mamlaka nchini Urusi wametumia vibaya sheria na kupingana na jumuiya ya kimataifa, viwango vya Baraza la Ulaya, mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, na katiba ya Urusi. Wametumia sheria hiyo kuzuia ibada inayofanywa kwa amani na kushambulia Kituo cha Usimamizi cha utendaji wa Mashahidi nchini Urusi.”

Vasiliy Kalin, Mwakilishi wa Kituo hicho cha Usimamizi, anasema hivi: “Mashahidi wa Yehova wamekuwa wakifanya ibada nchini Urusi tangu karne ya 19 na wamevumilia mateso mengi kipindi cha utawala wa Sovieti. Serikali imetambua rasmi unyanyasaji huo wa Mashahidi. Tungependa kuendelea kufanya ibada zetu kwa amani nchini Urusi. Mashtaka yanayotolewa kwamba tuna “msimamo mkali” ni hila iliyojificha ya watu wasiokubaliana na imani yetu. Sisi hatuna msimamo mkali wa dini.”

Mashahidi wa Yehova wana tumaini kwamba Urusi italinda uhuru wao wa ibada kama zinavyofanya nchi nyingine. Pia, wanaiomba Ofisi ya Mwendesha-Mashtaka Mkuu iache mashambulizi yake dhidi ya Kituo cha Usimamizi na kwamba Urusi itetee haki za binadamu za dini nyingine ndogondogo. Swali ni: Je, Urusi itatetea haki za binadamu? Au itaendelea kuwakandamiza Mashahidi wa Yehova kama ulivyofanya utawala wa Sovieti?

^ fu. 4 “Hitimisho la ripoti ya saba ya uchunguzi uliofanywa nchini Urusi,” Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, CCPR/C/RUS/CO/7, 28 Aprili 2015, fungu la 20.

^ fu. 7 “Mazungumzo Kuhusu Ripoti Zilizotolewa na Nchi Shirikishi chini ya kipengele cha 40 cha Mkataba, Maelezo ya Kumalizia ya Kamati ya Haki za Binadamu nchini Urusi,” Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, CCPR/CO/79/RUS, Desemba 1, 2003, fungu la 20.

^ fu. 10 “Serikali ya Urusi iheshimu makubaliano na mikataba,” Makala ya. 13018, Baraza la Bunge la Ulaya, tarehe 14 Septemba 2012, fungu la 497.

^ fu. 30 Nchini Urusi, dini inayokidhi viwango vya kisheria inaunda mashirika ya kisheria. Mashirika hayo ya kisheria yanashughulikia utendaji wa eneo fulani tu la nchi kama vile jiji au mji na si nchi nzima. Kuwa na shirika la kisheria kunawasaidia waabudu wa dini hiyo katika eneo husika kukodi au kununua sehemu za ibada.

^ fu. 33 Matendo hayo ni ukiukwaji wa Kipengele cha 28 cha Katiba ya Urusi, inayosema hivi: “Kila mtu anapaswa kuwa na uhuru wa dhamiri, uhuru wa ibada, kutia ndani haki ya kuabudu kibinafsi ama wakiwa kikundi katika dini yoyote au wasishirikiane na dini yoyote, kuwa huru kuchagua, kuamini na kushiriki maoni ya dini au mengine na kutenda kulingana na nayo.”

^ fu. 40 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania ni shirika la kimataifa lisilo la kibiashara linalotumiwa kutegemeza utendaji wa Mashahidi wa Yehova duniani pote. Shirika hilo lina hati-miliki ya machapisho ya Mashahidi.