Hamia kwenye habari

Mashahidi wa Yehova

Chagua lugha Kiswahili

JULAI 31, 2014
URUSI

Mahakama ya Jiji la Taganrog Yawahukumu Mashahidi wa Yehova Kuwa na Hatia kwa Sababu ya Imani Yao

Mahakama ya Jiji la Taganrog Yawahukumu Mashahidi wa Yehova Kuwa na Hatia kwa Sababu ya Imani Yao

Mnamo Julai 30, 2014, Mahakama ya Jiji la Taganrog iliwahukumu kuwa na hatia Mashahidi 7 kati ya 16 walioshtakiwa kwa kuhudhuria na kupanga mikutano yao inayofanywa kwa amani. Walishtakiwa kwa sababu tu ya kushiriki utendaji wa kidini ambao hufanywa ulimwenguni pote na Mashahidi wa Yehova. Uamuzi huo ni hatari kwa sababu unaweza kufanya Mashahidi wa Yehova kotekote nchini Urusi wanyimwe uhuru wa kidini.

Hakimu alipanga kutangaza uamuzi huo Julai 28, 2014, lakini aliahirisha hadi siku iliyofuata. Julai 29, hakimu huyo alisoma uamuzi huo wenye kurasa 100 kwa siku nzima na akaendelea asubuhi ya Julai 30. Aliwahukumu wazee wanne wa kutaniko miaka mitano hadi mitano na nusu gerezani pamoja na faini ya dola 2,800 za Marekani. Mashahidi wengine watatu walitozwa faini ya dola 1,400 hadi 1,700 za Marekani kila mmoja. Hakimu huyo aliondoa faini zote zilizotozwa kwa sababu kulingana na sheria, muda mrefu mno ulikuwa umepita tangu waliposhtakiwa, na akaahirisha pia vifungo vyote vya gerezani. Mashahidi wengine tisa waliondolewa mashtaka.

Ili kufikia uamuzi huo, hakimu alitegemea uamuzi uliofanywa Septemba 2009 na Mahakama ya Wilaya ya Rostov wa kuvunja Shirika la Kidini la Mashahidi wa Yehova jijini Taganrog. Ingawa uamuzi huo wa 2009 ulilenga hasa shirika la kisheria la Mashahidi, hakimu alipiga marufuku utendaji wa Mashahidi wote wa Yehova jijini Taganrog na maeneo mengine ya karibu.

Katika kipindi cha miezi 15 kesi hiyo ilipokuwa ikiendeshwa, walioshtakiwa walisema wazi kwamba hawawezi kukana imani yao na wangeendelea kufanya ibada yao wakiwa Mashahidi wa Yehova. Huenda wale waliohukumiwa wakafungwa kwa tuhuma ya kurudia kosa kwa sababu walisema wazi wataendelea na utendaji wao wa kidini.

Victor Zhenkov, mmoja wa mawakili katika kesi hiyo alisema hivi: “Ninahofia jinsi matokeo ya uamuzi huo yatakavyowaathiri Mashahidi wa Yehova nchini Urusi. Mamlaka za kutekeleza sheria jijini Taganrog na kotekote nchini Urusi wanaweza kutumia uamuzi huo ili kuendeleza kampeni ya propaganda ya kuendelea kuwadhulumu na kuwatesa Mashahidi wa Yehova na kuna uwezekano kwamba watafungwa gerezani kwa sababu ya imani yao.”

Mashahidi wa Yehova jijini Taganrog wamekata rufani katika Mahakama ya Wilaya ya Rostov.