Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

Nyumba ya Shahidi wa Yehova iliyoko Lutsino, Mkoa wa Moscow ikichomwa moto

JUNI 16, 2017
URUSI

Uamuzi wa Mahakama Kuu ya Urusi Umekuwa na Matokeo Mabaya kwa Mashahidi wa Yehova

Uamuzi wa Mahakama Kuu ya Urusi Umekuwa na Matokeo Mabaya kwa Mashahidi wa Yehova

Uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu ya Urusi Aprili 20, 2017, umekuwa na matokeo mabaya kwa mashahidi wa Yehova nchini kote. Wenye mamlaka wamekiuka haki za msingi za uhuru wa Mashahidi na kufanya utendaji wao wa kidini usiwe halali. Wakati huohuo, baadhi ya raia wa Urusi wametumia uamuzi huo kama sababu ya kuwabagua Mashahidi na kuwatendea jeuri kwa chuki.

Serikali ya Urusi Yakiuka na Kuzuia Haki za Kibinadamu

Dennis Christensen

Mashtaka ya Uhalifu Dhidi ya Wahudumu wa Mashahidi wa Yehova

 • Mei 25, polisi walivamia mkutano wa kidini wa Kutaniko la Oryol la Mashahidi wa Yehova. Polisi hao walimkamata Dennis Christensen, raia wa Denmark na mzee wa Kutaniko la Oryol. Bw. Christensen amewekwa mahabusu hadi Julai 23 wakati ambapo mwendesha mashtaka atafungua kesi dhidi yake kuhusu kufanya “utendaji wenye msimamo mkali.” Ikiwa atapatikana na hatia, Bw. Christensen anaweza kuhukumiwa kifungo cha miaka sita hadi kumi gerezani.

Maofisa Watoa Onyo kwa Mashirika ya Kidini ya Mashahidi

 • Mnamo Mei 4, ofisi ya mwendesha mashtaka ilitoa onyo kwa mwenyekiti wa Shirika la Kidini la Krymsk (LRO). Onyo hilo linasema kwamba mwenyekiti na washiriki wa shirika hilo la kidini wanaweza kuchukuliwa hatua za kisheria na kufunguliwa kesi ya uhalifu kwa kuendesha mikutano ya kidini.

 • Tangu kutolewa kwa uamuzi wa Mahakama Kuu, mashirika matano ya kidini (LROs) yamepewa onyo kama hilo.

Polisi Wavamia Maeneo ya Ibada

 • Aprili 22, polisi waliingia kwenye jengo la ibada la Mashahidi lililoko Dzhankoy, Jamhuri ya Crimea, mikutano hiyo ilipokuwa imemalizika. Maofisa hao walisisitiza kwamba baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu, Mashahidi hawakuwa na haki ya kukusanyika pamoja kwa ajili ya ibada. Walipekua jengo hilo na kisha kulifunga ili kuzuia lisitumiwe tena kwa ajili ya mikutano ya kidini.

 • Tangu kutolewa kwa uamuzi wa Mahakama Kuu, kumekuwa na matukio matano hivi ambayo polisi wamevuruga ibada ya Mashahidi, tukio moja lilifanywa kwenye nyumba ya mtu binafsi.

“Ninasikitishwa sana kwa kuufanya utendaji wenye amani wa Mashahidi wa Yehova nchini Urusi uonekane kuwa ni uhalifu bila sababu za msingi. . . . Ninawasihi wenye mamlaka nchini Urusi wahakikishe kwamba haki ya Mashahidi wa Yehova ya uhuru wa ibada au imani, uhuru wa kutoa maoni na kujieleza, uhuru wa kukusanyika pamoja na kushirikiana unatetewa kulingana na wajibu wa nchi chini ya sheria za kimataifa za haki za kibinadamu na OSCE [Shirika la Usalama na Ushirikiano la Ulaya].”—Michael Georg Link, Mkurugenzi wa Ofisi ya OSCE inayoshughulikia Taasisi za Kidemokrasia na Haki za Kibinadamu.

Wanafunzi Ambao ni Mashahidi Washambuliwa

 • Aprili 24, mwalimu katika kijiji cha Bezvodnoye, Mkoa wa Kirov, aliwaaibisha wanafunzi wawili ambao mama yao ni Shahidi wa Yehova. Mwalimu huyo alitetea matendo yake kwa kueleza kwamba Mashahidi wamepigwa marufuku nchini Urusi.

 • Mei 17, katika Mkoa wa Moscow, mkuu wa shule aliwaandikia barua ya onyo wazazi wa mwanafunzi mwenye umri wa miaka nane ambaye alikuwa akizungumza kuhusu Mungu na mwanafunzi mwenzake. Barua hiyo ya onyo ilirejelea uamuzi wa Mahakama Kuu wa kupiga marufuku “mambo yote yasiyohusiana na elimu” katika maeneo ya shule. Mkuu huyo wa shule alitishia kutoa ripoti kuhusu jambo hilo kwa polisi ili “mtoto huyo apewe mafunzo ya kubadili tabia.”

Wanaume Ambao ni Mashahidi Wazuiwa Kufanya Utumishi wa Badala wa Kiraia

 • Aprili 28, Tume ya Kuandikisha Watu Jeshini ya eneo la Cheboksary na Marposadskiy ilikataa maombi ya utumishi wa badala wa kiraia wa Shahidi wa Yehova. Tume hiyo ilisema kwamba Mashahidi wa Yehova wana “msimamo mkali” na hawawezi kukubaliwa kufanya utumishi badala wa kiraia.

 • Maombi ya Mashahidi wengine wawili hivi ya utumishi wa badala wa kiraia yalikataliwa.

Philip Brumley, mshauri mkuu wa Mashahidi wa Yehova, anasema hivi kuhusu kupishana kwa kauli za serikali: “Kwa upande mmoja, serikali inakataa kuwapa vijana ambao ni Mashahidi utumishi wa badala wa kiraia kwa sababu ‘wana msimamo mkali,’ wakati huohuo inadai kwamba haohao ‘wenye msimamo mkali’ waitwe jeshini. Kweli inapatana na akili kwamba serikali inaweza kuruhusu ‘wenye msimamo mkali’ wawe wanajeshi?”

Kutendewa Vibaya na Jamii na Kubaguliwa

Matendo ya Jeuri dhidi ya Mashahidi

 • Aprili 30, katika Lutsino, Mkoa wa Moscow, nyumba ya familia ya Shahidi ilichomwa moto pamoja na nyumba ya wazazi wake ambao ni wazee, iliyokuwa imeunganishwa na nyumba yao. Kwanza, mtu aliyeteketeza nyumba hizo alieleza jinsi anavyochukia dini ya familia hiyo na kisha akaanza kuzichoma moto.

 • Mei 24, katika eneo la Zheshart, Jamhuri ya Komi, watu walichoma moto jengo linalotumiwa na Mashahidi wa Yehova kwa ajili ya ibada na kusababisha uharibifu mkubwa.

  Jumba la Ufalme lililoko Zheshart lililoharibiwa kwa kuchomwa moto

 • Majumba tisa hivi ya ibada yameharibiwa tangu kutolewa kwa uamuzi wa Mahakama Kuu Aprili 20, 2017.

 • Aprili 26, Shahidi wa Yehova jijini Belgorod alikuwa akitoka nyumbani kwake aliposhambuliwa na mtu aliyesema kwa sauti kubwa, “Mmepigwa marufuku!” na kisha kumpiga Shahidi huyo.

 • Mei 11, kikundi cha wanaume kilivuruga mkutano wa Mashahidi wa Yehova jijini Tyumen na wakitumia lugha chafu na ya matusi, walitishia kuwadhuru wahudhuriaji.

Mashahidi Wafukuzwa Kazi

 • Mei 15, wasimamizi wa kiwanda cha kemikali jijini Dorogobuzh, Mkoa wa Smolensk, waliwafuta kazi waajiriwa wote ambao ni Mashahidi wa Yehova. Wasimamizi hao walieleza kwamba walikuwa wamepokea agizo kutoka FSB la kuwafuta kazi Mashahidi wote kwa sababu watu wenye “msimamo mkali” hawapaswi kufanya kazi kwenye kiwanda hicho.

 • Kuna visa vingine vitatu hivi tangu kutolewa kwa uamuzi wa Mahakama Kuu, ambavyo Mashahidi walioajiriwa walikuwa wametishiwa kufutwa kazi kwa sababu wanashirikiana dini yenye “msimamo mkali.” Katika kijiji cha Yashkino, Mkoa wa Kemerovo, polisi walimshinikiza Shahidi mmoja kufunua habari kuhusu Mashahidi wengine, lakini akakataa. Maofisa hao walisema kwamba ni kosa kisheria kuwa mshiriki wa dini iliyopigwa marufuku na aliwalinganisha Mashahidi wa Yehova na magaidi wa kundi la ISIS.

Tunahangaikia Hali Njema ya Mashahidi wa Yehova Nchini Urusi

Kwa kipindi cha miaka kumi kabla ya uamuzi wa Mahakama Kuu, Mashahidi wa Yehova nchini Urusi wamekuwa wakishambuliwa na watu waliochochewa na serikali kuingilia uhuru wao wa ibada na kuwasumbua sana. Sasa, baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, usalama wao umekuwa hatarini zaidi. Uamuzi huo umewashushia heshima Mashahidi na umewapa baadhi ya watu na maofisa wa serikali ujasiri wa kuwatendea Mashahidi isivyofaa hata zaidi, kama mifano iliyoelezwa mwanzoni ambayo ilitokea karibuni. Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote wanahangaika kuhusu kile kitakachowapata Mashahidi wenzao nchini Urusi ikiwa Mahakama Kuu ya Rufaa itaunga mkono uamuzi huo itakapokuwa ikisikiliza rufaa ya kesi hiyo Julai 17, 2017.

Bw. Brumley alisema hivi: “Hakuna mtu yeyote ambaye ameleta uthibitisho ambao hata kwa kadiri ndogo unawahusianisha Mashahidi wa Yehova na msimamo mkali. Madai ya kwambaMashahidi ni hatari kwa jamii hayalingani kwa njia yoyote na mateso ambayo wamevumilia kufikia sasa. Urusi inahitaji kufikiria upya matendo yake dhidi ya Mashahidi wa Yehova kwa kuzingatia katiba yake na mikataba ya kimataifa iliyotia sahihi ambayo inawahakikishia watu uhuru wa ibada.”