Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

APRILI 22, 2014
URUSI

Raia wa Urusi Washtakiwa kwa Sababu ya Imani Yao

Raia wa Urusi Washtakiwa kwa Sababu ya Imani Yao

Kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya kisasa ya nchi ya Urusi, Mashahidi wa Yehova * 16 kutoka Taganrog wameshtakiwa kwa kosa la uhalifu eti kwa sababu ya imani yao * na kwa kukutana pamoja kwa amani wakati wa ibada. Wakipatikana na hatia, wanaweza kutozwa faini ya rubo 300,000 (dola 10,000 za Marekani) au hata wahukumiwe kifungo cha miaka minane. Mashahidi hao 16 wameagizwa wasitoke Taganrog hadi mahakama itakapofikia uamuzi wake.

Kukandamizwa kwa Mashahidi wa Yehova huko Taganrog kulianza Juni 2008 wakati Mwendesha Mashtaka wa Eneo la Rostov alipowasilisha shtaka la kulifutilia mbali na kulipiga marufuku Shirika la Mashahidi wa Yehova la Taganrog. Alisema kwamba machapisho ya kidini yanayotolewa na Mashahidi wa Yehova yanatumia lugha inayowachochea watu wawe na msimamo mkali sana. Mahakama ya wilaya ilimuunga mkono mwendesha mashtaka huyo, na Mahakama Kuu ya Shirikisho la Urusi ikakubaliana na uamuzi huo Desemba 8, 2009.

Baada ya Mahakama Kuu ya Shirikisho la Urusi kukubali uamuzi huo, wenye mamlaka wa Taganrog walichukua Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova (nyumba ya ibada), jambo lililowalazimisha Mashahidi hao waanze kukutana katika nyumba za watu binafsi kwa ajili ya ibada. Mahakama hiyo pia ilitoa agizo kwamba machapisho 34 ya Mashahidi wa Yehova yaongezewe kwenye Orodha ya Serikali ya Vitabu Vinavyowachochea Watu Kuwa na Msimamo Mkali wa Kidini. Mashahidi wa Yehova wamepinga uamuzi huo na wamewasilisha kesi yao kwa Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu ili haki itendeke.

Kwa sababu ya uamuzi huo uliotolewa na mahakama ya wilaya, wenye mamlaka wa Taganrog wamewasumbua na kuwatisha Mashahidi. Mwaka wa 2011, mapema saa 12 asubuhi, polisi walivamia nyumba 19 za Mashahidi na kuamsha familia nzima nzima, kutia ndani wazee na watoto katika upekuzi uliochukua saa 8 hadi 11. Polisi hao walikuwa wakitafuta machapisho yanayodaiwa na serikali kuwa yana msimamo mkali. Walichukua machapisho yote ya kidini pamoja na vitu vya kibinafsi vya Mashahidi hao. Wenye mamlaka wa eneo hilo walirekodi kisiri ibada za Mashahidi na pia Shahidi mmoja mmoja aliyehudhuria ibada hizo ili watumie video hizo kuwafungulia mashtaka. Matukio hayo ya Taganrog yaliyoungwa mkono na serikali ya Urusi, yamewafanya Mashahidi wa Yehova wanyanyaswe na kutendewa isivyo haki kotekote nchini humo. *

Mashahidi wa Yehova ni dini inayotambuliwa duniani pote. Uhuru wa ibada umetajwa waziwazi katika Katiba ya Urusi na pia katika Mkataba wa Ulaya Kuhusu Haki za Kibinadamu. Mahakama kuu ulimwenguni pote zimesema kwamba Mashahidi wanastahili kuwa na uhuru wa ibada. Licha ya hilo, wenye mamlaka wa Taganrog wanatenda kana kwamba Mashahidi hawastahili kamwe kuwa na haki hiyo.

Kesi hiyo ingali inaendelea na huenda uamuzi ukatolewa mwezi wa Mei baada ya mahakama kusikiliza mashtaka yote yanayohusika. Mahakama ikiamua kuwahukumu Mashahidi hao 16, jambo hilo litahatarisha uhuru wa Mashahidi zaidi ya 800 wanaoishi Taganrog. Huenda jambo hilo pia likafanya kesi nyingine za mashtaka ya uhalifu dhidi ya Mashahidi katika maeneo mengine ya Urusi zishughulikiwe kwa njia hiyohiyo.

Grigory Martynov, msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Urusi alisema: “Jambo hili la kuingilia uhuru wa ibada halifai hata kidogo. Mashahidi wa Yehova hawahatarishi kwa njia yoyote ile usalama na uaminifu wa Shirikisho la Urusi. Unyanyasaji na ubaguzi huu unatendeka eti kwa sababu wao ni Mashahidi wa Yehova.”

^ fu. 2 Ni Mashahidi 10 tu kati ya wale 16 walio katika picha hapo juu.

^ fu. 2 Wenye mamlaka nchini Urusi waliwashtaki Mashahidi hao 16 katika mwaka wa 2012 chini ya Kifungu cha 282.2(1) na (2) cha Sheria ya Uhalifu ya Shirikisho la Urusi, ambapo mtu anaweza kufungwa hadi miaka mitatu gerezani. Wazee wanne wa kutaniko pia wameshtakiwa chini ya Kifungu cha 150(4) cha Sheria ya Uhalifu, ambapo mtu anaweza kufungwa kwa kipindi cha miaka 5 hadi 8 gerezani.

^ fu. 5 Tangu uamuzi wa Desemba 8, 2009 uliotolewa na Mahakama Kuu ya Shirikisho la Urusi, polisi wamewazuilia Mashahidi zaidi ya 1,600, wamepiga marufuku machapisho zaidi ya 70 ya kidini na kuyaorodhesha kuwa yana “msimamo mkali,” wamepekua nyumba zaidi ya 171 za Mashahidi na sehemu za ibada, na hata wamevuruga mikutano 69 ya ibada.