Hamia kwenye habari

MEI 7, 2018
URUSI

Mahakama ya Jiji la St Petersburg Imetoa Hukumu Dhidi ya Mashahidi wa Yehova

Mahakama ya Jiji la St Petersburg Imetoa Hukumu Dhidi ya Mashahidi wa Yehova

Mei 3, 2018, Mahakama ya Jiji ya Saint Petersburg ilikataa rufaa iliyokatwa na Mashahidi wa Yehova ambao walifungua kesi ya kupinga kutaifishwa kwa ofisi yao ya taifa iliyoko Solnechnoye. Uamuzi huo sasa umepitishwa na wakati wowote serikali inaweza kuchukua mali hiyo.

Uamuzi huu unaunga mkono uamuzi wa awali uliotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Sestroretskiy ambayo ilitangaza kwamba mkataba uliofanywa miaka 17 iliyopita wa kubadili umiliki wa mali hiyo iliyoko Solnechnoye uwe wa Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania hautambuliki kisheria. Kubatilisha mkataba huo kulifungua njia kwa mahakama kudai kwamba sikuzote mali hiyo ilikuwa ikimilikiwa na Kituo cha Usimamizi cha Mashahidi wa Yehova. Kwa hiyo, Serikali inaweza kutaifisha mali hiyo kwa sababu Kituo cha Usimamizi kilifungwa na Mahakama Kuu mnamo Aprili 2017. “Sababu” hizo zisizo za haki zimefanya serikali ipate haki ya kuchukua mali hiyo kwa njia isiyofaa.

Philip Brumley, Wakili wa Mashahidi wa Yehova, alisema hivi: “Uamuzi huu ni ukosefu mkubwa wa haki. Mali hiyo iliwekwa wakfu kwa Mungu na ilikuwa ikitumiwa kuendeleza utendaji wa kidini wenye amani wa Mashahidi wa Yehova nchini Urusi. Kimsingi, serikali imeiba mali hiyo, na tunapeleka kesi hii ya ukosefu wa haki kwenye Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu.”