Juni 7, 2017, saa 8:00 mchana Mahakama ya Mkoa ya Oryol itasikiliza rufaa ya kumwachilia raia wa Denmark aliyewekwa mahabusu anayeitwa Dennis Christensen. Bw. Christensen, ni mzee wa kutaniko la Mashahidi wa Yehova la Oryol, ambaye alikamatwa Mei 25, 2017 polisi walipovamia mkutano wa kidini wa katikati ya juma.

Serikali ya Urusi imeendelea kushambulia uhuru wa ibada wa Mashahidi wa Yehova. Shirika la Kidini la Oryol (LRO) lilishtakiwa kwa madai ya “kuchochea msimamo mkali” na lilipigwa marufuku mnamo Juni 2016. Hivi karibuni Mahakama Kuu ilikifunga Kituo cha Usimamizi na Mashirika ya Kidini (LROs) ya Mashahidi wa Yehova nchini Urusi. Idara ya Usalama wa Taifa (FSB) imedai kwamba Mashahidi jijini Oryol wanaendeleza shughuli za shirika lenye msimamo mkali kinyume cha sheria kwa kukusanyika pamoja kwa ajili ya ibada.

FSB imeanzisha uchunguzi wa kihalifu dhidi ya Bw. Christensen kwa sababu wanadai kwamba alikuwa mshiriki wa shirika la kidini lililopigwa marufuku la Oryol. Hata hivyo, Bw. Christensen hakuwahi kuwa mshiriki wa shirika hilo la kisheria. Kwa sasa amewekwa mahabusu mpaka Julai 23, 2017 kwa sababu mwendesha mashtaka alisema kwamba akiwa raia wa kigeni anaweza kutoroka kabla FSB haijatafuta uthibitisho kwa ajili ya kesi yake.

Isitoshe, kwa rufaa hiyo iliyokatwa dhidi ya kuwekwa mahabusu kwa Bw. Christensen, Mashahidi wa Yehova wameibua upya malalamiko waliyopeleka katika mahakama za kimataifa. Baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu, Mashahidi wengi wa Yehova nchini Urusi wanaendelea kuteswa na na kukabili matokeo mabaya ya matendo ya serikali.