Wamefungwa kwa Sababu ya Imani Yao—Urusi
Historia ya kisasa ya Mashahidi wa Yehova nchini Urusi imejaa ukandamizaji na mateso. Katika sehemu kubwa ya karne ya 20, wenye mamlaka nchini Urusi waliwatendea isivyo haki Mashahidi, ingawa walijulikana kuwa watu wanaopenda amani, na raia wanaotii sheria. Lengo la serikali ya Muungano wa Sovieti lilikuwa ni kuwalazimisha Mashahidi wawe wafuasi wa itikadi za kisovieti. Hawakuruhusiwa kuwa na Biblia au machapisho ya kidini. Kwa kuwa walikuwa wakifuatiliwa sana walilazimika kufanya mikutano kwa siri. Ikiwa wangegunduliwa, basi wangepigwa sana au kuhukumiwa vifungo vya muda mrefu gerezani. Serikali hiyo iliwapeleka maelfu ya Mashahidi uhamishoni huko Siberia.
Hali hiyo ilianza kubadilika mwaka wa 1991 wakati serikali ya Urusi ilipowasajili kisheria Mashahidi wa Yehova na kuwaruhusu kuabudu kwa uhuru bila kuingiliwa na serikali. Hata hivyo, kipindi hicho cha amani hakikudumu kwa muda mrefu.
Mwaka wa 2009, upinzani ulianza tena wakati Mahakama ya Juu ya Urusi ilikubali uamuzi wa mahakama ya chini iliyodai kwamba kutaniko fulani la Mashahidi wa Yehova ni lenye “msimamo mkali.” Baada ya kesi zilizodumu kwa miaka kadhaa, Aprili 2017 Mahakama ya Juu nchini Urusi ilipiga marufuku mashirika ya kisheria ya Mashahidi wa Yehova kwa tuhuma za kuwa na msimamo mkali. Muda mfupi baada ya hapo wenye mamlaka nchini Urusi walitaifisha mali za Mashahidi, wakafunga maeneo yao ya ibada, na wakatangaza kwamba machapisho yao yanawachochea watu kuwa na “msimamo mkali.”
Baada ya kupiga marufuku mashirika ya kisheria ya Mashahidi wa Yehova wenye mamlaka walianza kuwashambulia Mashahidi mmoja-mmoja. Wanavuka mipaka kwa kuhusianisha ibada ya Shahidi mmoja-mmoja na shirika lililopigwa marufuku. Polisi huwavamia Mashahidi nyumbani kwao na kuwatesa au kuwahoji kwa ukali. Mashahidi wa umri mbalimbali wa kike na wa kiume wamekamatwa, na wakahukumiwa kwenda gerezani au kupewa vifungo vya nyumbani.
Tangu marufuku ilipotangazwa Aprili 2017, mamia ya Mashahidi wamepelekwa kizuizini au kufungwa gerezani kwa kutuhumiwa kwamba wana msimamo mkali. Kufikia Februari 15, 2023, jumla ya Mashahidi 103 wako gerezani.
Malalamiko Kuhusu Jinsi Urusi Inavyowatesa Mashahidi wa Yehova
Mamlaka nchini Urusi zinaendelea kuwahukumu Mashahidi kwa madai kwamba wanashiriki utendaji wenye msimamo mkali ingawa jamii ya kimataifa imetoa malalamiko na kuitaka Urusi kuacha kuwatesa Mashahidi. Inapendeza kwamba baadhi ya mahakama za Urusi zimekataa kuwaita Mashahidi wa Yehova kuwa wenye “msimamo mkali” na wamewaachilia huru Mashahidi walioshtakiwa chini ya kifungu cha 282 cha Sheria ya Uhalifu ya Shirikisho la Urusi kuhusu msimamo mkali. Maamuzi ya mahakama hizo yanapatana na azimio lililorekebishwa la hivi karibuni la Mahakama ya Juu ya Urusi. Oktoba 2021, mahakama hiyo ilifafanua kwamba, ibada inayofanywa na mtu mmoja-mmoja haipaswi kuonwa kuwa ni kushiriki katika utendaji wa shirika la kidini lililopigwa marufuku.
Wachunguzi mbalimbali na mahakama kutoka nje ya Urusi wameishutumu serikali ya nchi hiyo kwa kuendelea kuwatesa Mashahidi wa Yehova.
Tangazo Kutoka kwa Baraza la Kudumu la Shirika la Usalama la Ushirikiano wa Ulaya: “Umoja wa Ulaya unaendelea kuwa na wasiwasi mwingi kuhusu hali wanazokabili Mashahidi wa Yehova nchini Urusi kama vile mateso yanayoendelea kutia ndani, kuvamiwa nyumbani kwao, kuwekwa kizuizini kiholela, kushtakiwa kwamba ni wahalifu, na kupewa vifungo vya hadi miaka saba gerezani. . . . Tunaliomba Shirikisho la Urusi litende kupatana na wajibu wake wa kimataifa wa kulinda haki za kibinadamu, uhuru wa kusema, ushirikiano, kukusanyika kwa amani, dini au imani kutia ndani haki za mtu kuwa katika kikundi kidogo, na haki ya kesi kusikilizwa kupatana na sheria.”
Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu: Juni 7, 2022, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu ilitoa hukumu muhimu dhidi ya Urusi na kuishutumu nchi hiyo kwa sababu ya kuwatesa Mashahidi wa Yehova (Taganrog LRO and Others v. Russia, nos. 32401/10 and 19 others). Mahakama hiyo ilitoa uamuzi dhidi ya Urusi kwa sababu ya kutenda kinyume na sheria na kuwapiga marufuku Mashahidi wa Yehova mwaka wa 2017. Urusi iliamuriwa “kufanya yote inayoweza ili kufuta kesi zote zinazoendelea za Mashahidi wa Yehova . . . na kuwaachilia . . . Mashahidi wa Yehova [walio gerezani].” Kwa kuongezea, Urusi iliamuriwa irudishe mali zote ilizotaifisha au ilipe zaidi ya dola milioni 60 kama fidia, na pia iwalipe wale waliopeleka malalamiko yao zaidi ya dola milioni 3 kama fidia.
Barua Kutoka kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Ulaya: Barua ya Desemba 9, 2022, iliyotumwa kwa Waziri wa Urusi wa Mambo ya Nje, Marija Pejčinović Burić ilisema: “Katika kesi ya Jehovah’s Witnesses of Moscow and Others na kesi ya Krupko and Others, zinazohusu kupigwa marufuku kwa shirika la Mashahidi kutia ndani utendaji wao, kuvurugwa kwa mkutano wenye amani wa kidini na kufungwa gerezani kwa baadhi ya washirika, Kamati yetu iliwasihi wenye mamlaka kuondoa marufuku dhidi ya utendaji wa mashirika yote ya Mashahidi wa Yehova na kusitisha kesi zote za uhalifu zinazoendelea dhidi yao.”
Hukumu Ndefu za Kikatili
Misako Yenye Kudhalilisha, Kesi, na Kufungwa Gerezani. Desemba 19, 2022, Mahakama ya Wilaya ya Birobidzhan iliwahukumu wanaume wanne ambao ni Mashahidi vifungo vya gerezani vya hadi miaka saba kwa madai kwamba walishirikiana na shirika lenye msimamo mkali. Mei 17, 2018, maofisa 150 walifanya msako katika nyumba nyingi za Mashahidi lakini walikazia hasa nyumba za wanne hao. Upelelezi na pia kesi yenyewe zilifanywa kwa muda wa miaka minne na nusu, jambo ambalo halijawahi kutokea hapo awali. Dmitry Zagulin alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu na nusu gerezani; Alam Aliyev, alihukumiwa kifungo cha miaka sita na nusu; na Sergei Shulyarenko na Valery Krieger, walihukumiwa kifungo cha miaka saba kila mmoja.
Faini Kubwa Kupita Kiasi. Desemba 23, 2022, Mahakama ya Wilaya ya Alatyrskiy iliyo katika Jamhuri ya Chuvash iliwahukumu Andrey Martynov na mke wake, Nina, kwa madai kwamba walishiriki utendaji wenye msimamo mkali. Andrey Martynov, mwenye umri wa miaka 59, alihukumiwa kifungo cha nje cha miaka sita. Ingawa mke wake, Nina, hakupewa kifungo cha gerezani, alipigwa faini ya rubo 350,000 (Dola 5,000 hivi za Marekani), hiyo ni faini kubwa sana kwa mwalimu wa chekechea. Wakati huohuo, dada Zoya Pavlova, mwenye umri wa miaka 57 na ambaye pia amestaafu alipigwa faini ya rubo 350,000.
Vifungo Virefu vya Gerezani. Desemba 29, 2022, Mahakama ya Wilaya ya Zeyskiy iliyo katika Eneo la Amur ilimhukumu Yevgeniy Bitusov kifungo cha miaka sita gerezani na Leonid Druzhinin kifungo cha miaka sita na nusu gerezani kwa madai kwamba walishiriki katika utendaji wenye msimamo mkali. Mara tu baada ya hukumu hiyo kutolewa, walipelekwa gerezani. Yevgeniy na Leonid wote wameoa, na Yevgeniy ana watoto wawili, mmoja ana miaka 21 na mwingine miaka 13.
Wazee Watendewa Vibaya. Vilen Avanesov mwenye umri wa miaka sabini ni mojawapo kati ya Mashahidi wenye umri mkubwa ambao wamefungwa gerezani nchini Urusi. Vilen amepitia hali ngumu maishani mwake. Mwaka wa 1988, Vilen, mke wake, na watoto wao wawili waliokuwa wadogo walilazimika kuondoka nyumbani kwao na kuwa wakimbizi nchini Armenia. Mwaka huohuo, tetemeko la ardhi lilipiga Yerevan, na wakapoteza makao yao na vitu vyao. Familia hiyo ilihamia eneo la Rostov-on-Don kusini mashariki mwa Urusi. Mei 2019, Vilen na mwana wake, Arsen, walikamatwa kwa madai ya uwongo kwamba walishiriki katika utendaji wenye msimamo mkali. Sasa Vilen na mwanaye wamefungwa katika Gereza Na. 3, lililo katika Eneo la Ulyanovsk na inatazamiwa kwamba wataachiliwa 2024.
Jitihada Zinazoendelea za Kukomesha Vifungo vya Gereza Visivyo vya Haki
Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote wanahuzunika sana kwa sababu waabudu wenzao wanateswa nchini Urusi. Mamilioni ya Mashahidi ulimwenguni pote wametuma barua kwa maofisa wa serikali nchini Urusi, kuwaomba waache kuwatesa Mashahidi. Mawakili wa Mashahidi wamekata rufaa kwenye ngazi zote za mahakama za Urusi na wametuma kesi nyingi kwenye Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu. Mashahidi wa Yehova pia wametuma malalamiko yao kwa Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu na Kikundi cha Umoja wa Mataifa Kinachoshughulikia Vifungo Vilivyo Kinyume cha Sheria. Isitoshe, wamepeleka ripoti mbalimbali kwenye mashirika ya kimataifa yanayofuatilia ukiukaji wa haki za kibinadamu. Mashahidi wa Yehova wataendelea kufanya yote wanayoweza ili kuwafahamisha wengine kuhusu mateso wanayopata waamini wenzao nchini Urusi ili mateso hayo yakomeshwe.
Mfuatano wa Matukio
Februari 15, 2023
Jumla ya Mashahidi 103 wako gerezani.
Mei 24, 2022
Ndugu Dennis Christensen aliachiliwa, baada ya kufungwa gerezani kwa miaka mitano.
Mei 4, 2022
Baada ya kufungwa kwa zaidi ya mwaka mmoja dada Valentina Baranovskaya aliachiliwa.
Januari 12, 2022
Wizara ya Haki ya Shirikisho la Urusi inaongeza programu ya JW Library kwenye Orodha ya Serikali ya Vitabu na Habari Zinazowachochea Watu Kuwa na Msimamo Mkali wa Kidini. Hiyo ndiyo mara ya kwanza kwa programu kupigwa marufuku nchini Urusi kwa msingi wa kuwa yenye msimamo mkali.
Oktoba 25, 2021
Mahakama ya Wilaya ya Trusovskiy iliyo Astrakhan iliwahukumu Rustam Diarov, Yevgeniy Ivanov, na Sergey Klikunov kifungo cha miaka nane gerezani. Olga Ivanova amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu na miezi sita gerezani.
Septemba 27, 2021
Mahakama ya jiji la Saint Petersburg yakataa rufaa dhidi ya uamuzi wa Machi 31, 2021, uliotangaza kwamba programu ya JW Library ni yenye msimamo mkali na kuipiga marufuku isitumiwe kotekote katika eneo la Shirikisho la Urusi na Crimea. Uamuzi wa awali wa mahakama utaanza kutumika mara moja.
Septemba 23, 2021
Mahakama ya Wilaya ya Volgograd Traktorozavodsky yamhukumu Sergey Melnik na Igor Yegozaryan miaka sita gerezani. Valeriy Rogozin ahukumiwa miaka sita na miezi mitano gerezani.
Agosti 11, 2021
Baada ya Mahakama ya Wilaya ya Abinskiy iliyo Katika Eneo la Krasnodar kusikiliza kesi ya Vasiliy Meleshko kwa siku mbili, alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani.
Juni 30, 2021
Mahakama ya Jiji la Blagoveshchensk ya Eneo la Amur ilimhukumu Aleksey Berchuk kifungo cha miaka minane na Dmitriy Golik akahukumiwa kifungo cha miaka saba gerezani.
Februari 24, 2021
Mahakama ya Jiji la Abakan ya Jamhuri ya Khakassia yamhukumu Valentina Baranovskaya kifungo cha miaka miwili gerezani. Na mwana wake pia, Roman Baranovskiy, alihukumiwa kifungo cha miaka sita gerezani.
Februari 10, 2021
Mahakama ya Wilaya ya Abinskiy iliyo katika Eneo la Krasnodar ilimhukumu Aleksandr Ivshin kifungo cha miaka saba gerezani.
Septemba 2, 2020
Mahakama ya mji wa Berezovsky eneo la Kemerovo yamhukumu Sergey Britvin na Vadim Levchuk kifungo cha miaka minne gerezani.
Agosti 3, 2020
Mahakama ya Eneo la Pskov ilifanya uamuzi wa kumwachilia Gennady Shpakovskiy kutoka gerezani. Ilidumisha hukumu yake lakini ikabadili kifungo chake cha miaka sita na nusu gerezani kuwa kifungo cha nje kwa muda uliokuwa umeamuliwa awali.
Julai 13, 2020
Nyumba 100 hivi za Mashahidi zapekuliwa katika maeneo ya Voronezh na Belgorod.
Juni 9, 2020
Mahakama ya Jiji la Pskov yamhukumu Ndugu Gennady Shpakovskiy mwenye umri wa miaka 61 kifungo cha miaka saba na nusu gerezani.
Februari 6, 2020
Mashahidi watano kati ya wale sita waliohukumiwa Septemba 19, 2019, wamehamishiwa kwenye gereza la Penal Colony Na. 1 lililo Orenburg. Walipowasili walinzi wa gereza waliwapiga sana kwa mateke na rungu. Bw. Makhammadiyev alivunjwa ubavu, kisha mapafu yakaumia na pia ini lake lilipata madhara.
Septemba 19, 2019
Hakimu Dmitry Larin wa Mahakama ya Wilaya ya Leninskiy iliyo Saratov amewahukumu wanaume sita ambao ni Mashahidi wafungwe gerezani. Majina yao ni—Konstantin Bazhenov, Aleksey Budenchuk, Feliks Makhammadiyev, Roman Gridasov, Gennadiy German, na Aleksey Miretskiy—kwa kuwasingizia kwamba ‘wamepanga shughuli zenye msimamo mkali.’
Mei 23, 2019
Mahakama ya Mkoa wa Oryol yakataa rufaa ya Dennis Christensen na kuunga mkono hukumu ya kifungo cha gerezani cha miaka sita.
Aprili 26, 2019
Kamati ya Umoja wa Mataifa ya vifungo visivyo vya Haki iliona kwamba Dimtriy Mikhailov alitendewa isivyo haki na kutangaza wazi kwamba nchi ya Urusi inawatendea Mashahidi wa Yehova kikatili.
Februari 6, 2019
Mahakama ya Wilaya ya Zheleznodorozhniy yamtangaza Dennis Christensen kuwa na hatia na kumhukumu kifungo cha miaka sita.
Oktoba 9, 2018
Polisi na kikosi maalumu walivamia nyumba jijini Kirov. Wanaume kadhaa Mashahidi kutia ndani Andrzej Oniszczuk, ambaye ni raia wa Poland, walikamatwa na kuwekwa mahabusu
Julai 15, 2018
Polisi wafanya msako katika nyumba kadhaa za Mashahidi jijini Penza. Vladimir Alushkin alikamatwa na kuwekwa mahabusu.
Julai 4, 2018
Polisi wavamia nyumba katika eneo la Omsk. Sergey na Anastasia Polyakov walikamatwa na kuwekwa mahabusu. Bi. Polyakova ni Shahidi wa kwanza ambaye ni mwanamke kukamatwa na kuwekwa mahabusu kwa mashtaka ya kuwa na msimamo mkali nchini Urusi.
Juni 12, 2018
Polisi wavamia nyumba katika eneo la Saratov. Wanaume kadhaa Mashahidi walikamatwa na kuwekwa mahabusu.
Juni 3, 2018
Polisi wavamia nyumba katika eneo la Tomsk na Pskov. Sergey Klimov akamatwa na kuwekwa mahabusu.
Februari 19, 2018
Kesi ya uhalifu ya Dennis Christensen yaanza kusikilizwa katika Mahakama ya Wilaya ya Zheleznodorozhniy. Hakimu Aleksey Rudnev ndiye anayeshughulikia kesi hiyo.
Julai 20, 2017–Novemba 2018
Dennis Christensen aongezewa mara kadhaa muda wa kubaki mahabusu, mara ya kwanza na Mahakama ya Wilaya ya Sovietskiy na kisha Mahakama ya Wilaya ya Zheleznodorozhniy. Kwa sasa amefungwa mpaka Februari 1, 2019.
Mei 26, 2017
Mahakama ya Wilaya Sovietskiy ya Oryol yamhukumu Dennis Christensen kubaki mahabusu kwa miezi miwili kabla ya kesi yake kusikilizwa.
Mei 25, 2017
Polisi wavamia wakati wa ibada jijini Oryol na kumkamata Dennis Christensen.
Aprili 20, 2017
Mahakama Kuu za Shirikisho la Urusi inaamua kufunga ofisi ya Mashahidi wa Yehova na kufuta mashirika 395 ya kidini (LRO) ya Mashahidi wa Yehova.