Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

JULAI 27, 2015
URUSI

Urusi Yapiga Marufuku Tovuti Rasmi ya Mashahidi wa Yehova

Urusi Yapiga Marufuku Tovuti Rasmi ya Mashahidi wa Yehova

Wenye mamlaka nchini Urusi walipiga marufuku tovuti rasmi ya Mashahidi wa Yehova miezi saba baada ya Mahakama Kuu ya Shirikisho la Urusi kutanganza kuwa tovuti ya www.jw.org ina msimamo mkali wa kidini. Marufuku ilianza rasmi Julai 21, 2015, Wizara ya Sheria ya Shirikisho la Urusi ilipoingiza tovuti ya jw.org kwenye Orodha ya Serikali ya Habari Zinazowachochea Watu Kuwa na Msimamo Mkali. Kampuni zinazotoa huduma za kusambaza Intaneti nchini Urusi zimewazuia watu wasitembelee tovuti hiyo, na kwa sasa ni kosa la jinai kuhamasisha watu watembelee tovuti hiyo nchini humo. Urusi ndiyo nchi pekee duniani iliyopiga marufuku jw.org.

Matukio Yaliyotangulia Kupigwa Marufuku kwa JW.ORG

Mashahidi wa Yehova nchini Urusi hawakujua kuwa mwaka wa 2013 maafisa wa serikali jijini Tver walifungua kesi kwa siri inayolenga tovuti hiyo. Mwendesha Mashtaka wa Jiji la Tver alipeleka mashtaka kwenye Mahakama ya Wilaya ya Tsentralniy akiomba tovuti ya jw.org ipigwe marufuku kwa sababu ina machapisho machache ya Mashahidi wa Yehova ambayo yalitangazwa na mahakama ya Urusi kuwa yana msimamo mkali wa kidini. * Agosti 7, 2013, mahakama ya wilaya iliunga mkono ombi la mwendesha mashtaka bila kuwajulisha Mashahidi wa Yehova na ikatangaza kuwa tovuti ya jw.org ina msimamo mkali wa kidini.

Mashahidi wa Yehova walipojua uamuzi huo kupitia vyombo vya habari mwezi mmoja baadaye, walikata rufaa na kwa hiari waliondoa machapisho yaliyoshukiwa kwa ajili ya wasomaji nchini Urusi. Januari 22, 2014, Mahakama ya Mkoa ya Tver ilibatilisha uamuzi wa mahakama ya wilaya, na kusema kuwa mahakama hiyo haikuwa na msingi wa kisheria wa kupiga marufuku jw.org na kwamba ilipaswa kuwapa taarifa wenye hati-miliki ya tovuti hiyo ili washiriki katika kesi.

Akiwa hajaridhishwa na uamuzi wa mahakama ya mkoa, Naibu Mwanasheria Mkuu, S. G. Kekhlerov, alikata rufaa katika Mahakama Kuu ya Shirikisho la Urusi. Mashahidi wa Yehova hawakupewa habari kamili kuhusu kesi hiyo. Pamoja na hayo, Desemba 2, 2014, Mahakama Kuu ilisikiliza rufaa ya mwendesha mashtaka bila washtakiwa kuwepo.

Mahakama Kuu ilithibitisha kuwa Mashahidi waliondoa machapisho muda mfupi baada ya kutolewa kwa uamuzi wa kesi ya Agosti 2013 lakini ikadai bila msingi wowote kwamba machapisho hayo yanaweza kurudishwa tena kwenye tovuti. Kwa hiyo, Mahakama hiyo ikaamua kubatilisha uamuzi wa mahakama ya mkoa na kuunga mkono uamuzi wa mahakama ya wilaya kwa kutangaza kuwa tovuti ya jw.org ni yenye msimamo mkali. * Mashahidi wa Yehova walikata rufaa katika Mahakama Kuu wakipinga uamuzi uliotolewa, lakini Mahakama ilikataa rufaa hiyo. Pia wamekata rufaa kwa Mwenyekiti wa Mahakama Kuu, ambaye alikataa rufaa hiyo mnamo Julai 8, 2015.

Uamuzi Wahatarisha Uhuru wa Ibada

Mashahidi wa Yehova wanadai kwamba uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu si wa haki na hauna msingi wowote wa kisheria kwa sababu hakuna machapisho yoyote yaliyotangazwa kuwa na msimamo mkali yanayopatikana kwenye tovuti ya jw.org nchini Urusi tangu majira ya kupukutika ya mwaka 2013. Kutokana na uamuzi huo, wenye mamlaka nchini Urusi wameyaamuru makampuni yanayotoa huduma za Intaneti yawazuie watu wasitembelee tovuti ya jw.org nchini Urusi. Jambo hilo lilifanya wasomaji washindwe kupata Biblia katika zaidi ya lugha 130 na machapisho ya Biblia katika lugha zaidi ya 700, kutia ndani Kirusi na Lugha ya Alama ya Urusi. Kwa sasa, mtu yeyote nchini Urusi anayewahamasisha au kuwahimiza wengine watembelee tovuti hiyo anashtakiwa kwa kosa la kufanya shughuli zenye msimamo mkali wa kidini. Kwa sababu ya marufuku hiyo, zaidi ya Mashahidi wa Yehova 170,000 wameshindwa kupata habari muhimu zinazowaelimisha kiroho na zinazowasaidia katika ibada yao kila siku.

Uamuzi wa Mahakama Kuu unawapa maofisa wa serikali nchini Urusi njia nyingine ya kuzuia shughuli za kidini zinazofanywa kwa amani na Mashahidi wa Yehova. Ikiwa baadhi ya maofisa wa serikali wataendelea kutumia vibaya Sheria ya Kudhibiti Vikundi Vyenye Msimamo Mkali ya serikali ya Urusi, uhuru wa kidini nchini humo utadhibitiwa na hata utakuwa hatarini. Mashahidi wa Yehova wanatumaini maofisa wanaofuata haki watatetea haki ya msingi ya binadamu ya uhuru wa ibada na haki ya kusikilizwa mahakamani, kama inavyoonyeshwa katika katiba na mikataba ya kimataifa ya Urusi.

^ fu. 4 Kufikia Juni 1, 2015, mahakama za Urusi zimetangaza machapisho 78 ya Mashahidi wa Yehova kuwa yenye msimamo mkali wa kidini. Mashahidi wa Yehova wanapinga uamuzi huo katika mahakama za nchini na katika Mahakama ya Ulaya ya Haki za Binadamu.

^ fu. 7 Naibu mwendesha mashtaka alikata rufaa, na Baraza la Hukumu la Kesi za Madai la Mahakama Kuu ilitoa uamuzi uliounga mkono rufaa hiyo.