Januari 16, 2017, Mahakama ya Jiji la Moscow ilitupilia mbali rufani ya Mashahidi ambayo ilidai uhalali wa onyo lililotolewa na Mwendesha-Mashtaka Mkuu dhidi ya makao makuu ya Mashahidi. Jopo la mahakimu watatu lilikataa hoja zote zilizotolewa na mawakili wa Mashahidi na baada ya mapumziko ya dakika 10, jopo hilo lilitoa uamuzi wake. Uamuzi huo uliunga mkono ule wa Mahakama ya Wilaya ya Tverskoy uliotolewa Oktoba 12, 2016, ambao uliipa ushindi Ofisi ya Mwendesha-Mashtaka Mkuu. Onyo hilo lililotolewa Machi 2, 2016, sasa limetiwa nguvu. Hata hivyo, mambo hayajawa wazi kabisa kuhusu jinsi onyo hilo litakavyoathiri uhuru wa ibada ya Mashahidi nchini Urusi.