Hamia kwenye habari

FEBRUARI 23, 2018
URUSI

Mahakama ya Oryol Imemwongezea Dennis Christensen Muda wa Kubaki Mahabusu

Februari 22, 2018, Hakimu Aleksey Rudnev, wa Mahakama ya Wilaya ya Zheleznodorozhniy jijini Oryol, alitoa uamuzi kwamba Dennis Christensen aendelee kubaki mahabusu hadi Agosti 1, 2018. Bw. Christensen anashtakiwa kwa kupanga utendaji wa shirika la kidini ambalo lilikuwa limetangazwa kuwa lina msimamo mkali. Ukweli ni kwamba alikamatwa alipokuwa akihudhuria mkutano wa kidini wa Kikristo ambao ulivamiwa na polisi mnamo Mei 2017.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa Februari 19, siku ambayo hakimu aliahirisha kutoa uamuzi kuhusu maombi ya pande zote mbili. Hata hivyo, kesi hiyo ilipokuwa ikisikilizwa Februari 22, hakimu alikataa maombi yote yaliyowasilishwa na mawakili wa Bw. Christensen na kutoa uamuzi wa kuongeza muda wa kukaa mahabusu. Kesi ya uhalifu aliyofunguliwa imeratibiwa kuanza kusikilizwa Februari 26 saa 8:30 mchana.

Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote wanahangaikia hali ya Bw. Christensen na wanasali kwa ajili ya mke wake, Irina, aweze kuwa imara licha ya kukosa utegemezo wa mume wake. Bw. Christensen amekuwa mahabusu kwa miezi tisa.