Julai 17, 2017, Urusi imeonyesha kutojali kabisa mikataba ya kimataifa ya kulinda uhuru wa ibada, wakati Mahakama Kuu ya Urusi ilipothibitisha uamuzi wake wa awali wa kuufanya utendaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Urusi uonekane kuwa wa kihalifu. Uamuzi huo umepiga marufuku ibada ya Mashahidi wa Yehova katika nchi nzima.

Jopo la majaji watatu la Mahakama Kuu ya Rufaa lilikataa rufaa ya Mashahidi na kuunga mkono uamuzi wa mahakama wa Aprili 20 uliotolewa na Hakimu Yuriy Ivanenko. Hakimu huyo alikuwa ametoa hukumu ya kuunga mkono madai yaliyotolewa na Wizara ya Haki ya “kufunga ‘Kituo cha Usimamizi cha Mashahidi wa Yehova nchini Urusi’ ambacho ni shirika lao la kidini na mashirika ya kisheria yanayosimamiwa na Kituo hicho na kutaifisha mali zote za Kituo hicho ziwe za Shirikisho la Urusi.”

Mawakili wa Kituo cha Usimamizi

Uamuzi huo unafanya usalama na hali za Mashahidi wa Yehova zaidi ya 175,000 nchini Urusi ziwe katika hatari kubwa sana. Philip Brumley, Wakili wa Mashahidi wa Yehova, alisema hivi: “Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote wanahangaishwa sana na hali ya ndugu na dada zao wa kiroho nchini Urusi. Uamuzi wa mahakama ya rufaa umehalalisha kisheria uonevu wanaofanyiwa Mashahidi wa Yehova nchini Urusi na kufanya iwe rahisi kushtakiwa kwa makosa ya uhalifu na watendewe isivyofaa. Wametengwa na jamii katika nchi yao wenyewe.”

Mashahidi wa Yehova nchini Urusi wamekata rufaa ili wapate haki katika Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu na Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu. Wakati huohuo, waabudu wenzao duniani kote wanasali kwamba Serikali ya Urusi ifikirie upya uamuzi wake na kuheshimu haki za msingi za kibinadamu ili Mashahidi waweze “[kuendelea] kuishi kwa amani na utulivu na ujitoaji-kimungu,” kama inavyoelezwa kwenye 1 Timotheo 2:2.