Hamia kwenye habari

Mashahidi wa Yehova

Chagua lugha Kiswahili

JULAI 24, 2017
URUSI

Mahakama ya Oryol Imeongeza Muda wa Kifungo cha Dennis Christensen

Mahakama ya Oryol Imeongeza Muda wa Kifungo cha Dennis Christensen

Julai 20, 2017, Mahakama ya Wilaya ya Sovietskiy jijini Oryol imeamua Dennis Christensen aongezewe muda wa kukaa mahabusu hadi Novemba 23, 2017. Bw. Christensen, raia wa Denmark na Shahidi wa Yehova ambaye alikamatwa Mei 25 wakati wawakilishi wa Idara ya Usalama wa Taifa, pamoja na maofisa wa polisi wenye silaha walioziba nyuso na walipovamia mkutano wa kidini uliofanywa kwa amani jijini Oryol ambao yeye alihudhuria.

Wakili wake walitoa maombi aachiliwe kwa dhamana na walifanya mipango ya kulipia gharama zinazohusika. Hata hivyo, mahakama ilikataa kumwachilia kwa dhamana licha ya kwamba Bw. Christensen hana rekodi yoyote ya kuwa mhalifu au historia ya kushiriki katika matendo ya jeuri.

Kuendelea kuwekwa mahabusu kwa Bw. Christensen kunatokana na uamuzi wa Julai 17 wa Mahakama Kuu ya Rufaa ambayo ilithibitisha hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu ya kupiga marufuku mashirika yote ya kisheria ya Mashahidi nchi nzima na utendaji wao. Baada ya kampeni ya zaidi ya miaka kumi ya kuwatesa Mashahidi na kuwaweka kwenye orodha ya watu “wenye msimamo mkali,” sasa wenye mamlaka nchini Urusi wamefanikiwa kuunda mbinu ya kisheria ya kufanya mnyanyaso dhidi ya utendaji wao wa kidini uonekane halali.

Akitoa maoni yake kuhusu mambo yote yanayowakabili Mashahidi nchini Urusi, Kate M. Byrnes, Kaimu Balozi wa Tume ya Marekani ya Shirika la Usalama na Ushirikiano la Ulaya, alisema hivi: “Tumeshtushwa sana na uamuzi wa Julai 17 wa Mahakama Kuu ambao uliunga mkono kupigwa marufuku kwa utendaji wa Mashahidi wa Yehova na kufungwa kwa Kituo cha Usimamizi pamoja na mashirika ya kisheria 395 ya Mashahidi wa Yehova kwa madai ya ‘utendaji wenye msimamo mkali.’ Inasikitisha sana kwamba kwa sasa Mashahidi wa Yehova zaidi ya 175,000 nchini Urusi wanaweza kushtakiwa kwa kosa la uhalifu kwa sababu tu ya kushiriki katika utendaji wa dini yao. Kupanua matumizi ya sheria inayohusu ‘msimamo mkali’ ili kuvilenga kimakosa vikundi vya kidini vya amani vyenye washiriki wachache nchini Urusi kunasikitisha.”