Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

JANUARI 14, 2016
URUSI

Maofisa Nchini Urusi Wakamata Mzigo wa Biblia na Machapisho ya Biblia

Maofisa Nchini Urusi Wakamata Mzigo wa Biblia na Machapisho ya Biblia

Katika mwaka uliopita, wenye mamlaka nchini Urusi wamechukua hatua nyingine zaidi ya kudhibiti uhuru wa kidini, kwa kutoruhusu Biblia zinazochapishwa na Mashahidi wa Yehova kuingizwa nchini humo. Mashahidi walishangaa kusikia Ofisi ya Forodha ya Vyborg ikidai kuwa Biblia hizo huenda zina habari “zenye msimamo mkali.” Kitendo hicho kina madhara makubwa kwa Mashahidi na pia kwa raia wengine wa Urusi wanaoamini kwamba Biblia ni kitabu kitakatifu na msingi wa imani yao.

Madai Yenye Kushtua Dhidi ya Biblia

Julai 13, 2015, maofisa wa forodha kwenye mji wa Vyborg ulio mpakani, waliukamata mzigo wenye nakala 2,013 za Biblia Takatifu—Tafsiri ya Ulimwengu Mpya katika Kirusi. * Maofisa hao walichukua Biblia tatu, na kuzituma kwa “mtaalamu” zichunguzwe ikiwa zina habari “zenye msimamo mkali,” na wakashikilia Biblia zilizobaki. Mwezi wa Agosti, maofisa wa forodha waliifungulia mashtaka ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova ya Finland (kwa kusafirisha machapisho hayo hadi Urusi).

Mei 5, 2015, maofisa wa forodha walikamata mzigo mwingine uliokuwa na machapisho ya kidini ya Mashahidi wa Yehova, kutia ndani Biblia katika Kiossetia. Kitendo hicho kina madhara makubwa kwa Wakristo nchini Urusi wanaozungumza Kiossetia, kwa kuwa Tafsiri ya Ulimwengu Mpya kwa sasa ndiyo tafsiri pekee ya Biblia kamili inayopatikana katika lugha hiyo.

Ingawa wenye mamlaka nchini Urusi wameshawahi kutumia isivyofaa Sheria ya Kudhibiti Vikundi Vyenye Msimamo Mkali ya Serikali ya Urusi ili kuzuia machapisho ya Mashahidi wa Yehova, hii ni mara ya kwanza kwa mamlaka hizo kudai kwamba tafsiri ya Biblia inaweza kuhusianishwa na habari zenye msimamo mkali. * Ikiwa mahakama zitaamua kwamba Biblia hizo ni zenye msimano mkali, zitapigwa marufuku nchini Urusi.

Machapisho Mengine Yazuiwa Kinyume cha Sheria

Baadhi ya machapisho yaliyozuiwa kuingia nchini Urusi

Zaidi ya kuzuia Biblia zisiingizwe nchini Urusi, kuanzia Machi 2015, maofisa wa forodha pia wamezuia machapisho mengine ya kidini ya Mashahidi yasiingie nchini humo. * Maofisa hao wamefuata hatua zilezile kila mara walipokamata mzigo. Kwanza wanaufungua mzigo kinyume cha sheria ili kupata nakala za machapisho za “kuchunguzwa na wataalamu,” * kisha ofisi ya mwendesha-mashtaka inafungua kesi ili machapisho hayo yatangazwe kuwa yenye msimamo mkali. Mapambano marefu ya kisheria yanafuata, kwa kuwa karibu kila mzigo wa machapisho utahitaji kutetewa kisheria katika mahakama mbalimbali.

Pindi moja, Mashahidi wa Yehova walijaribu kuchukua mzigo mmoja wa machapisho. Waliwaonyesha maofisa wa forodha idhini zilizotolewa na mahakama, wataalamu, na kuwaonyesha hati nyingine zilizoonyesha kwamba serikali tayari imetoa kibali kuwa machapisho hayo si yenye msimamo mkali. Hata hivyo, maofisa hao wa forodha walipuuza hati hizo na kuukamata mzigo.

Mbali tu na kuzuiwa kwa machapisho hayo ya Mashahidi, machapisho ya kielektroni ya Mashahidi wa Yehova yamezuiwa pia. Julai 21, 2015, Urusi ndiyo iliyokuwa nchi pekee ulimwenguni kupiga marufuku jw.org—tovuti rasmi ya Mashahidi wa Yehova. Kampuni zote nchini Urusi zinazotoa huduma za Intaneti zimewazuia watu kutembelea tovuti hiyo, na mtu yeyote nchini Urusi anayetangaza kuhusu tovuti hiyo anaweza kufunguliwa mashtaka ya uhalifu au ya kiutawala.

Kupigwa marufuku kwa tovuti hiyo kumefanya iwe vigumu sana kwa Mashahidi wa Yehova kupata machapisho kwenye mfumo wa kielektroni, hasa Mashahidi viziwi na vipofu. Kwa kuwa elimu ya Biblia ni msingi wa shughuli za kidini za Mashahidi, kuzuia machapisho yao kunaathiri ibada yao.

Mashahidi wa Yehova Waomba Haki Itendeke

Mahakama za Urusi zimepinga au kufuta kesi zilizotaka kupiga marufuku vitabu vingine vinavyoonwa kuwa vitakatifu. Mwaka wa 2011, mahakama moja jijini Tomsk nchini Urusi, ilifuta kesi iliyotaka kupiga marufuku toleo la Bhagavad Gita ya dini ya Kihindu. Mwaka wa 2013, mahakama ya rufani ilipinga uamuzi uliotolewa kwamba tafsiri moja ya Kurani ni yenye msimamo mkali.

Mashahidi wa Yehova wanatumaini kwamba mahakama nchini Urusi hazitakubaliana na madai ya maofisa hao wa forodha kwamba tafsiri fulani ya Biblia ni yenye msimamo mkali na ziwaamuru waziachilie Biblia hizo na machapisho mengine ya kidini ya Mashahidi wa Yehova.

Mfululizo wa Matukio

 1. Machi 1, 2015

  Maofisa wa forodha wakamata mzigo wa machapisho na kuchukua kinyume cha sheria nakala kadhaa za machapisho.

 2. Mei 4, 2015

  Wenye mamlaka wakamata mzigo wa machapisho uliokuwa njiani kwenda Urusi. Baadaye wanakagua mzigo huo na kuchukua machapisho kadhaa—kutia ndani Biblia za lugha ya Kiossetia—ili kukagua ikiwa ni “yenye msimamo mkali.”

 3. Mei 28, 2015

  Mahakama yaamuru taasisi moja jijini St. Petersburg ifanye “utafiti wa kitaalamu” kwenye machapisho yaliyokamatwa Machi 1, 2015.

 4. Juni 2015

  Maofisa wa forodha wakamata mizigo miwili ya machapisho mpakani jijini Vyborg.

 5. Julai 13, 2015

  Maofisa wa forodha wakamata mzigo wenye Biblia za Kirusi tu.

 6. Agosti 13, 2015

  Maofisa wa forodha jijini Vyborg waamua kuwanyang’anya Mashahidi Biblia 2,013 kutoka katika mzigo uliokamatwa Julai 13, wakidai kwamba huenda ni “zenye msimamo mkali.” Wenye mamlaka wakafungua kesi dhidi ya ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova nchini Finland.

 7. Septemba 1, 2015

  Katika kesi iliyojadili mzigo uliokamatwa Mei 4 uliokuwa na Biblia za Kiossetia na machapisho mengine, hakimu alikataa maombi ya Mashahidi na kuwazuia mawakili wao wasitoe maelezo ya kumalizia.

 8. Oktoba 30, 2015

  Mahakama ya Jiji la Vyborg yatoa uamuzi kwamba maofisa wa forodha walikagua mzigo uliokamatwa Mei 4 kinyume cha sheria.

 9. Novemba 17, 2015

  Mahakama yasikiliza kesi kuhusu mzigo wa Biblia uliokamatwa Julai 13 na kuiahirisha hadi wakati mwingine.

^ fu. 4 Biblia Takatifu—Tafsiri ya Ulimwengu Mpya ni tafsiri ya Biblia katika lugha ya kisasa inayochapishwa na Mashahidi wa Yehova na kutolewa bila malipo katika zaidi ya lugha 120.

^ fu. 6 Kuanzia Januari 1, 2016, mahakama nchini Urusi zimeamua kwamba machapisho 82 ya Mashahidi wa Yehova ni yenye msimamo mkali. Mashahidi wamefungua kesi kupinga maamuzi hayo kwenye mahakama nchini humo na pia, kwenye Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu.

^ fu. 8 Tangu Desemba 2015, maofisa wa forodha jijini Vyborg wamekamata mizigo saba ya machapisho yaliyokusudiwa kuwafikia Mashahidi wa Yehova nchini Urusi.

^ fu. 8 Sheria ya nchi ya Urusi inasema kwamba maofisa wanahitaji kibali kutoka mahakamani ili kukagua na kukamata mzigo wowote na ukaguzi huo lazima ufanywe mbele ya wahusika. Katika kila tukio, maofisa wa forodha walikiuka sheria hiyo.