Mnamo Aprili 19, 2012, katika jiji la Perm’ lililo katikati ya Urusi, Aleksandr Solovyov, ambaye ni Shahidi wa Yehova alitozwa faini ya rubo 1,000 (karibu dola 30 za Marekani) kwa sababu ya kupanga ‘mkutano wa kidini usio halali’ katika jumba lililokodiwa.

Baada ya kusikiliza kwa makini ‘ushahidi’ wote uliotolewa dhidi ya Solovyov, jaji wa mahakama ya wilaya alifutilia mbali uamuzi wa mahakama ya chini na kufuta faini hiyo.

Jaji huyo alisoma uamuzi wake kisha akamgeukia Shahidi huyo aliyepata ushindi na kusema: “Licha ya kwamba utaratibu wa sheria haufuatwi na baadhi ya watu wana maoni yenye ubaguzi, hatuishi katika mwaka wa 1937 wakati ambapo tunaweza kufumbia macho ukweli ulio wazi. Kazi yenu ya kuwaelimisha watu na iendelee kuwasaidia watu katika jamii yetu wawe na maadili mazuri.

Mnamo Julai 1937, Stalin, aliyekuwa dikteta wa Muungano wa Sovieti, alitoa Amri nambari 00447, iliyoanzisha kipindi cha mateso makali. Mtu yeyote aliyeonekana kuwa na maoni tofauti na serikali alikamatwa na kushtakiwa mahakamani bila ushahidi wowote. Rekodi za serikali zinaonyesha kwamba makumi ya maelfu ya watu walipelekwa kwenye kambi za kazi ngumu na zaidi ya 300,000 walihukumiwa kifo na kuuawa.