Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

NOVEMBA 24, 2017
URUSI

Mahakama ya Oryol Imeongeza Tena Kifungo cha Dennis Christensen

Mahakama ya Oryol Imeongeza Tena Kifungo cha Dennis Christensen

HABARI ZA KARIBUNI: Desemba 22, 2017, Mahakama ya Mkoa wa Oryol ilitupilia mbali rufaa iliyokatwa na wakili wa Bw. Christensen ili aachiliwe kutoka mahabusu. Anapaswa kukaa mahabusu mpaka Februari 23, 2018. Muda wowote atapelekwa mahakamani, na huenda akashtakiwa kwa makosa ya uhalifu.

Katika uamuzi wa kesi ya Novemba 20, 2017 iliyochukua saa tatu kusikilizwa, Mahakama ya Wilaya ya Sovietsky iliyoko Oryol, Russia, ilimwongezea Dennis Christensen muda wa kukaa mahabusu hadi Februari 23, 2018. Hii ni mara ya pili kwa mahakama kumwongezea Bw. Christensen muda wa kukaa mahabusu kwa miezi mitatu. Amekaa mahabusu bila kuwa na mashtaka yoyote tangu alipokamatwa mnamo Mei 2017, wakati polisi walipovamia mkutano wa kidini uliofanywa kwa amani jijini Oryol ambao alikuwa amehudhuria.

Bw. Christensen ni raia wa Denmark na ni Shahidi wa Yehova. Kabla hajakamatwa, Mahakama Kuu ya Urusi ilikuwa imepiga marufuku kabisa utendaji wa Mashahidi wa Yehova kwa madai ya kuwa na msimamo mkali. Mahakama ya wilaya iliongeza muda wa kukaa mahabusu kwa mara nyingine ili kuruhusu wakati kwa ajili ya wachunguzi kukusanya “uthibitisho” wa mashtaka ya kufanya utendaji wa kidini kinyume cha sheria. Mahakama ilikataa kumhukumu kifungo cha nje wakati uchunguzi huo ukiendelea na pia ilipuuza uhakikisho wa serikali ya Denmark kwamba isingempatia Bw. Christensen kibali cha kusafiria au ifanye mipango ya kumsaidia aondoke nchini humo.

Wakati anapokamatwa, Bw. Christensen na mke wake ambaye ni raia wa Urusi, walikuwa wakitimiza haki yao ya msingi ya uhuru wa ibada na kukusanyika. Mahakama inaweza kutoa agizo aendelee kubaki mahabusu kwa muda usiozidi miaka miwili. Ikiwa atapatikana na hatia, atakabili kifungo cha miaka sita hadi kumi gerezani.