Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

SEPTEMBA 15, 2015
URUSI

Uamuzi wa Kesi Iliyosikilizwa Upya ya Mashahidi wa Yehova 16 huko Taganrog, Waahirishwa

Uamuzi wa Kesi Iliyosikilizwa Upya ya Mashahidi wa Yehova 16 huko Taganrog, Waahirishwa

Kesi iliyosikilizwa upya ya Mashahidi wa Yehova 16 huko Taganrog, Urusi imeendeshwa kwa miezi tisa sasa. Kesi hiyo imesikilizwa zaidi ya mara 20 katika majira ya kiangazi, na imepangwa kusikilizwa tena Oktoba. Wakipatikana na hatia, Mashahidi hao watakabili vifungo na faini kwa sababu tu ya kuhudhuria ibada, kusoma Biblia, na kushirikiana na waamini wenzao.

Kesi Inayoendeshwa kwa Muda Mrefu Yawaathiri Washtakiwa

Tangu kuanza kwa kesi hiyo iliyosikilizwa upya mapema mwaka huu, washtakiwa wametumia karibu siku 50 mahakamani. Kwa ujumla wamekwenda mahakamani kwa zaidi ya miaka miwili, kutia ndani muda waliotumia kwenye kesi ya kwanza. Jambo hilo linafanya iwe kesi ya jinai ya Mashahidi wa Yehova iliyotumia muda mrefu zaidi nchini Urusi.

Muda uliotumika katika kusikiliza kesi hiyo umewasababishia madhara makubwa washtakiwa. Mmoja wao, Kirill Kravchenko, anaeleza hivi: “Hatuwezi kufanya kazi; hatuna muda wa kukaa na familia zetu au kupumzika vya kutosha.” Washtakiwa kadhaa wamefukuzwa kazi au wameshinikizwa kuacha kazi kwa sababu ya muda wanaotumia katika kesi hiyo au kwa sababu wanakashifiwa hadharani kwa kuwa wao ni Mashahidi wa Yehova. Katika miaka miwili iliyopita, mahakama iliwaagiza waombe kibali rasmi wanapotaka kusafiri nje ya jiji la Taganrog.

Pia washtakiwa wameteseka sana kihisia kwa sababu ya muda unaotumika katika kesi. Tatyana Kravchenko anasema,“Afya yangu inaathirika. Siwezi kulala, au ninashtuka usiku wa manane. Wakati wote ninafikiria kesi, haitoki akilini, nina wasiwasi mwingi.” Nikolay Trotsyuk, ambaye pia ni mshtakiwa, amelazwa mara kadhaa kwa sababu ya mfadhaiko wa kesi hiyo.

Matukio Yaliyopelekea Kesi Kusikilizwa Upya huko Taganrog

Mwaka 2011, polisi waliwapeleleza kwa siri Mashahidi wa Yehova huko Taganrog. Mashahidi wa Yehova kumi na sita walishtakiwa mwaka 2012, na kesi yao ilianza kusikilizwa Mei 2013. Baada ya miezi 15 ya kusikilizwa kwa kesi hiyo, Mahakama ya Jiji la Taganrog iliwahukumu washtakiwa saba kwa madai ya kuwa na msimamo mkali. Hakimu aliwatoza faini kubwa washtakiwa wote saba na kuwahukumu vifungo vya gereza vya muda mrefu wanne kati yao, lakini baada ya muda mfupi aliondoa faini zote alizowatoza na akaahirisha vifungo vyao. Hakimu aliwaondolea mashtaka Mashahidi tisa waliobaki kwa sababu ya kukosa ushahidi lakini aliunga mkono kwamba walijihusisha na shughuli zenye msimamo mkali.

Mashahidi hao 16 walikata rufaa katika Mahakama ya Mkoa wa Rostov, wakiomba waondolewa mashtaka ya uhalifu. Mwendesha mashtaka alikata pia rufaa, akipinga kuahirishwa kwa vifungo na kudai ni uendekevu.

Desemba 12, 2014, Mahakama ya Mkoa wa Rostov ilifikiria rufaa zote na kubatilisha uamuzi wa Mahakama ya Mji wa Taganrog. Hata hivyo, badala ya kuwaondolea mashtaka Mashahidi, Mahakama ya Mkoa wa Rostov ilikubali madai ya mwendesha mashtaka na kurudisha kesi kwenye Mahakama ya Jiji la Taganrog ili isikilizwe upya na hakimu tofauti. Kesi iliyosikilizwa upya ilianza Januari 22, 2015, na Mashahidi walitarajia uamuzi utolewe Juni 2015. Kwa kuwa sasa hakimu amepanga kesi isikilizwe mwezi Oktoba, inaonekana kwamba ataoa uamuzi wa kesi hiyo mwishoni mwa mwaka 2015.

Je, Sheria ya Msimamo Mkali Inazuia Uhuru wa Ibada?

Sheria ya Kudhibiti Vikundi Vyenye Msimamo Mkali ya Shirikisho la Urusi mwanzoni ilikusudiwa kupambana na ugaidi, lakini baadhi ya wenye mamlaka nchini Urusi wanaitumia vibaya kuzuia shughuli halali na zenye amani za ibada. Wenye mamlaka kotekote nchini wamevuruga mikutano ya Mashahidi, wamepekua nyumba zao, na kupiga marufuku na kuwanyang’anya machapisho, wakitumia sheria ya msimamo mkali kama kisingizio cha kutetea vitendo vyao. Huko Taganrog, wenye mamlaka walitumia vibaya sheria hiyo kufunga shirika la kisheria la Mashahidi wa Yehova la eneo hilo na kuchukua Majumba yao ya Ufalme. Hivi karibuni, wenye mamlaka huko Samara na Abinsk wamefanya hivyo pia kwa kufunga shirika la kisheria la Mashahidi na kuchukua mali zao.

Kutokana na hatua hizo kali zilizochukuliwa na wenye mamlaka nchini Urusi, Mashahidi wa Yehova wamepeleka kesi 28 katika Mahakama ya Ulaya ya Haki za Binadamu (ECHR) ili kutafuta utatuzi. Kwa kuwa kesi 22 kati ya hizo zinahusisha ukiukwaji wa haki za binadamu, kwa sasa ECHR inazishughulikia kesi zote kwa pamoja. Kulingana na wakili wa Mashahidi, ECHR inaweza kutoa uamuzi wa kesi hizo kufikia mwishoni mwa mwaka 2015.

Tishio la Kuongezeka kwa Chuki ya Kidini

Kwa sasa Urusi iko kwenye njia panda kuhusu suala la uhuru wa dini. Ikiwa wale wanaoshtakiwa huko Taganrog watakutwa na hatia, Mashahidi wa Yehova nchini Urusi wanatarajia kwamba huenda Mashahidi wenzao watashtakiwa huko Samara, Abinsk, na maeneo mengine. Wanatumaini kwamba serikali ya Urusi itakomesha mateso hayo na kutetea uhuru wa ibada wa raia zake wote.

Mfululizo wa Matukio

 1. Juni 9, 2008

  Ofisi ya Mwendesha Mashtaka ya Mkoa wa Rostov yawashtaki Mashahidi wa kwa madai ya kujishughulisha na utendaji wenye msimamo mkali.

 2. Septemba 11, 2009

  Mahakama ya Mkoa wa Rostov yatangaza machapisho 34 ya kidini ya Mashahidi wa Yehova kuwa yenye msimamo mkali na yapiga marufuku Shirika la Dini la Mashahidi wa Yehova Jijini Taganrog (LRO).

 3. Desemba 8, 2009

  Mahakama Kuu ya Shirikisho la Urusi yatetea uamuzi wa Septemba 2009 wa Mahakama ya Mkoa ya Rostov.

 4. Machi 1, 2010

  Wizara ya Sheria yaingiza machapisho 34 katika Orodha ya Serikali ya Habari Zinazowachochea Watu Kuwa na Msimamo Mkali ambayo yalitangazwa na Mahakama ya Mkoa ya Rostov kuwa yana msimamo mkali. Wenye mamlaka wachukua Majumba ya Ufalme ya Mashahidi jijini Taganrog.

 5. Juni 1, 2010

  Mashahidi wa Yehova wa Taganrog wamefungua kesi Taganrog LRO na Wengine dhidi ya Urusi katika Mahakama ya Ulaya ya Haki za Binadamu.

 6. Aprili 30, 2011

  Mashirika ya upelelezi yameanza kutumia video kurekodi kwa siri shughuli za dini za Mashahidi huko Taganrog.

 7. Julai 6, 2011

  Wenye mamlaka waongeza shirika la Taganrog la LRO kwenye Orodha ya Serikali ya Mashirika Yenye Msimamo Mkali.

 8. Agosti 2011

  Wenye mamlaka wawafungulia mashtaka ya uhalifu Mashahidi huko jijini Taganrog na kupekua nyumba 19.

 9. Mei 31, 2012

  Wapelelezi wapeleka mashtaka rasmi ya kwanza dhidi ya Mashahidi wa Yehova wa jiji la Taganrog kwa sababu ya shughuli zao za kidini.

 10. Mei 2013

  Kesi ya Mashahidi 16 walioshtakiwa kwa kosa la kujihusisha na shughuli za msimamo mkali wa kidini yaanza katika Mahakama ya Jiji la Taganrog.

 11. Julai 29-30, 2014

  Mahakama ya Jiji la Taganrog yawahukumu Mashahidi saba kwa madai ya kujihusisha na shughuli za dini. Baadaye, washtakiwa 16 pamoja na mwendesha-mashtaka wakata rufaa.

 12. Desemba 12, 2014

  Rufaa iliposikilizwa, Mahakama ya Mkoa ya Rostov yaamua kwamba kesi hiyo isikilizwe upya na jaji tofauti.

 13. Januari 22, 2015

  Kesi iliyosikilizwa upya ya Mashahidi 16 yaanza katika Mahakama ya Jiji la Taganrog.

^ fu. 44 “Majukumu na Ahadi Zinazopaswa Kutekelezwa na Shirikisho la Urusi” Azimio namba 1896 (la 2012), Mkutano wa Bunge la Baraza la Ulaya, fungu la 25.31.

^ fu. 45 “Tathmini ya Ripoti ya Saba ya Shirikisho la Urusi,” Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, fungu la 20.