Juni 26, 2014, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) ilitoa uamuzi uliowatetea Mashahidi wa Yehova na haki yao ya kuabudu bila kuvurugwa na serikali ya Urusi. Katika uamuzi ambao haukupingwa, Mahakama hiyo ilitambua kwamba Urusi imevunja Kifungu cha 5 (haki ya uhuru na usalama) na Kifungu cha 9 (uhuru wa kufikiri, dhamiri, na kidini) katika Mkataba wa Ulaya wa Haki za Kibinadamu, polisi walipovamia na kuvuruga ibada usiku wa Aprili 12, 2006.

Usiku huo, Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote walikusanyika kwa ajili ya ukumbusho wa kifo cha Yesu Kristo wanaofanya kila mwaka. Makutaniko mawili jijini Moscow yalikodi ukumbi wa shule kwa ajili ya mkutano huo wa pekee na yalitarajia waabudu zaidi ya 400 wahudhurie. Mkutano huo ulipokuwa ukiendelea, polisi wa kukabiliana na ghasia waliwasili mahali hapo katika gari kumi za polisi na basi mbili ndogo, zilizobeba Kikosi Maalumu cha Polisi (OMON) kilichojihami pamoja na polisi wengine wengi. Mara moja walizingira jengo hilo, na bila kibali cha operesheni hiyo, wakavuruga mkutano huo wa ibada. Waliwaamuru wote waliohudhuria kuondoka kwenye jengo hilo, kisha wakapekua jukwaani, wakachukua machapisho ya kidini, na kuwakamata wanaume 14 waliohudhuria na kuwapeleka kwenye kituo cha polisi kilichokuwa karibu na kuwafungia huko. Wakili aliyeombwa kuwawakilisha Mashahidi waliokamatwa alipofika kwenye kituo hicho cha polisi ili kuwasaidia, polisi walipekua vitu vyake, wakamwangusha chini, na kumshikia kisu kooni, na kutisha kwamba ikiwa angewashtaki, familia yake ingeumia. Baada ya karibu saa nne, waliokamatwa waliachiliwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani kwao.

Nikolay Krupko, mlalamishi mkuu katika kesi hiyo

Nikolay Krupko, pamoja na Mashahidi wengine waliokamatwa, waliwashtaki wenye mamlaka kwa kuvuruga mkutano wa ibada, kuwakamata na kuwafunga kinyume cha sheria. Mahakama ya Wilaya ya Lyublino na Mahakama ya Jiji la Moscow zilipokataa malalamishi hayo, wanaume hao walikata rufani kwa ECHR mnamo Juni 2007.

Katika uamuzi wake wa Juni 26 kwenye kesi ya Krupko na Wengine dhidi ya Urusi, ECHR ilisema hivi: “Tangu zamani mahakama hii imeshikilia kwa uthabiti kwamba hata katika visa ambapo mamlaka hazikujulishwa ifaavyo kuhusu tukio la umma lakini wahusika hawakuvuruga amani ya wengine, polisi hawapaswi kuvuruga mkutano unaofanywa kwa amani ‘katika jamii ya kidemokrasia.’ . . . Hilo linakazia kwa uthabiti hata zaidi kwamba mkutano uliovunjwa haukuwa tukio lililofanywa uwanjani kwa fujo bali ilikuwa sherehe ya kidini iliyofanywa kwa amani katika ukumbi wa mikutano ambao haukusababisha vurugu wala kuvuruga utaratibu katika jamii. Uvamizi wa polisi wengi wa kuzuia ghasia wakiwa na lengo la kuvuruga sherehe hiyo, hata ikiwa wenye mamlaka walifikiri kwa unyoofu kwamba kufanya mkutano huo bila kujulishwa mapema kuliufanya uwe kinyume cha sheria, pamoja na kukamatwa kwa walalamishi na kuzuiliwa kwa saa tatu, si kisingizio cha kutosha kwamba walikuwa wakidumisha utaratibu katika jamii.”

Huu ni uamuzi wa nne dhidi ya Urusi kwamba imekiuka haki za Mashahidi wa Yehova. Mwaka wa 2007, katika uamuzi wa kesi ya Kuznetsov na Wengine dhidi ya Urusi, ECHR iliamua kwamba Urusi ilikiuka Mkataba wa Ulaya wakati wenye mamlaka walipovuruga mkutano wa Mashahidi wasio na uwezo wa kusikia huko Chelyabinsk. Mnamo 2010, ECHR iliwatetea Mashahidi wa Yehova dhidi ya Urusi katika kesi ya Mashahidi wa Yehova wa Moscow dhidi ya Urusi, ambapo Hakimu wa Jiji la Moscow alilivunja na kulipiga marufuku shirika la kisheria la Mashahidi la Moscow. Katika mwaka wa 2013, ECHR iliamua kwenye kesi ya Avilkina na Wengine dhidi ya Urusi kwamba Urusi ilikiuka haki ya msingi ya kuwa na faragha wakati Kiongozi wa Mashtaka wa Jiji la St. Petersburg alipoamuru habari za kibinafsi za kitiba zifunuliwe.

Uamuzi wa ECHR ni uthibitisho zaidi wa kwamba mamlaka za Urusi, katika jitihada zao za kukandamiza ibada ya Mashahidi wa Yehova nchini Urusi, zimekiuka uhuru mbalimbali unaotetewa katika Katiba ya Shirikisho la Urusi na pia katika Mkataba wa Ulaya.