Eneo la Donetsk

HORLIVKA—Jumba la Ufalme latekwa na kikosi chenye silaha.

 • Mwishoni mwa Juni 2014, wanaume wenye silaha walivamia Jumba la Ufalme kwenye eneo la 3A Viliamsa Akademika Street, wakaiba vifaa vya kielektroni, na kubadili vitasa. Walilitumia kuwa kambi yao.

 • Aprili 13, 2015, Mashahidi wa Yehova walirudishiwa jengo hilo.

Mji wa Horlivka, Mtaa wa 75 Akademika Koroliova.

HORLIVKA—Jumba la Ufalme latekwa na kikosi chenye silaha.

 • Julai 5, 2014, wanaume wenye silaha waliteka Jumba la Ufalme. Waliligeuza kuwa kambi na hifadhi ya silaha, lakini mnamo Septemba 2014 wakaondoka na kuliacha. Mashahidi walirudi na kutumia Jumba hilo la Ufalme kwa ajili ya mikutano yao ya kidini.

 • Oktoba 12, 2014, wanaume wenye silaha walisimamisha ibada katika Jumba la Ufalme na kuamuru wote waliokuwemo waache utendaji wao wa kidini. Walieleza kuwa dini pekee inayokubalika katika eneo hilo ni ya Kiothodoksi na kwamba karibuni wanapanga “kuwaondolea mbali Mashahidi wa Yehova.” Wanaume hao walitumia Jumba la Ufalme kama kambi yao.

Jiji la Donetsk, Mtaa wa 10 Karamzina.

DONETSK—Jumba la Ufalme latekwa na kikosi chenye silaha.

 • Agosti 13, 2014, wanaume wenye silaha wavunja milango ya Jumba la Ufalme na kuweka kambi humo.

 • Agosti 19, 2014, wanaume hao waiba mfumo wa sauti na kuhama jengo hilo. Mashahidi wakarudi na kuendelea kutumia Jumba la Ufalme kufanya mikutano yao ya kidini.

 • Oktoba 18, 2014, wawakilishi wa Kikosi cha Nne cha Oplot waliingia kwenye Jumba la Ufalme baada ya ibada, na kutangaza kwamba wanaliteka.

 • Novemba 18, 2014, wanaume wenye silaha walazimisha Mashahidi kutia sahihi mkataba wa kubadili umiliki wa Jumba la Ufalme kwenda kwa Ofisi ya Kamanda wa Wilaya za Petrovskyi na Kirovskyi. Wanaume hao wamegeuza majengo hayo kuwa kambi yao.

Mji wa Horlivka, Mtaa wa 4 Hertsena.

HORLIVKA—Jumba la Ufalme latekwa na raia.

 • Septemba 30, 2014, stesheni ya televisheni ya eneo hilo ilimhoji “mmiliki mpya” wa Jumba hilo la Ufalme, aliyeeleza kuwa Mashahidi wa Yehova walinyang’anywa jengo hilo ili liwe shule ya ndondi. Tangu 2013, Jumba hilo la Ufalme limevamiwa mara kadhaa na kuchomwa moto. Jaribio la mwisho la kulichoma lilikuwa Juni 5, 2014.

DONETSK—Jumba la Ufalme latekwa na kikosi chenye silaha.

 • Oktoba 26, 2014, wanaume wenye silaha kutoka Kikosi cha Shakhtar cha Jamhuri ya Watu wa Donetsk (DPR) walivamia Jumba la Ufalme na sasa wamepiga kambi hapo.

Mji wa Zhdanivka, Mtaa wa 14 Komsomolska.

ZHDANIVKA—Jumba la Ufalme latekwa na kikosi chenye silaha.

 • Oktoba 27, 2014, wanaume wa kikosi chenye silaha cha Horlivka waliliteka Jumba la Ufalme kwa mujibu wa amri iliyotolewa na Kamanda. Kamanda Msaidizi wa Horlivka alieleza kwamba dini ya Othodoksi ndiyo dini pekee inayokubalika katika eneo hilo na kwamba nyingine zote zimepigwa marufuku.

 • Novemba 21, 2014, kamanda wa kikosi kingine chenye silaha alichukua mamlaka ya Jumba hilo na kuwaeleza Mashahidi wa Yehova kwamba sasa Jumba la Ufalme liko chini ya mamlaka ya wasaidizi wake.

 • Novemba 20, 2015, wanaume hao wenye silaha walilitelekeza Jumba hilo na Mashahidi wa Yehova wakaendelea kulimiliki.

Kijiji cha Telmanove, Mtaa wa 112 Pervomaiska.

TELMANOVE—Jumba la Ufalme latekwa na kikosi chenye silaha.

 • Novemba 4, 2014, wanaume wenye silaha waliingia kwa kutumia nguvu ndani ya jengo hilo na kuliweka chini ya ulinzi wa askari mwenye silaha.

 • Desemba 11, 2014, wanaume hao walileta silaha katika jengo hilo na kupiga kambi hapo.

Mji wa Makiivka, Mtaa wa 17 Pecherska.

MAKIIVKA—Jumba la Ufalme latekwa na kikosi chenye silaha na baadaye kutelekezwa.

 • Novemba 5, 2014, wanaume wenye silaha kutoka Kikosi cha Rus walivamia Jumba la Ufalme. Wakawaamuru Mashahidi wawapatie funguo za Jumba na wasirudi kamwe. Siku iliyofuata, kamanda msaidizi aliondoa kibao cha Jumba la Ufalme na kuweka bendera ya kikosi hicho.

 • Novemba 26, 2014, kikosi chatelekeza jengo hilo.

HORLIVKA—Jumba la Ufalme latekwa na kikosi chenye silaha na baadaye kutelekezwa.

 • Novemba 29, 2014, wanaume wenye silaha waliingia kwenye Jumba la Ufalme lililopo kwenye eneo la 105-A Vitchyzniana Street na kutangaza kwamba wanaliteka. Mmoja wa wanaume hao alisema kwamba serikali ya DPR inaruhusu tu utendaji wa dini ya Othodoksi katika eneo hilo. Kisha wakaliweka jengo chini ya ulinzi wenye silaha na kuwaonya Mashahidi wasirudi hapo. Siku iliyofuata, wanaume hao wakalitelekeza.

 • Julai 22, 2016, wanaume wenye silaha walivamia tena Jumba la Ufalme na kuwaamuru wahudhuriaji wote waondoke mara moja. Jumba hilo liliporwa.

Mji wa Zuhres, Mtaa wa 1 Cherniakhovskoho.

ZUHRES—Jumba la Ufalme latekwa na kikosi chenye silaha.

 • Desemba 20, 2014, kamanda wa mji huo alitangaza kwamba analiteka jengo. Akaamuru Mashahidi wampatie funguo za Jumba na wasirudi kamwe.

 • Aprili 19, 2015, Jumba hilo lilirudishiwa Mashahidi.

DONETSK—Jumba la Ufalme latekwa na kikosi chenye silaha.

 • Februari 1, 2015, wanaume wenye silaha waliingia kwenye Jumba la Ufalme. Wakaamuru kwamba Mashahidi wawape funguo za Jumba la Ufalme na kuweka sahihi mkataba wa kubadili umiliki wa jengo hilo kwenda kwa kikosi hicho kwa kipindi chote cha vita.

 • Februari 29, 2016, Mashahidi walirudishiwa jengo hilo lakini lilihitaji kurekebishwa ili liweze kutumiwa tena kwa ajili ya mikutano ya kidini.

YENAKIEVE—Jumba la Ufalme latekwa na kikosi chenye silaha.

 • Machi 3, 2015, wanaume wenye silaha waamuru Mashahidi wa Yehova wawape funguo za Jumba la Ufalme ili litumiwe kama kambi.

HORLIVKA—Jumba la Ufalme latekwa na kikosi chenye silaha.

 • Julai 25, 2016, wanaume wenye silaha waliingia kwenye Jumba la Ufalme lililopo eneo la 9 Simferopolska Street, na kutangaza kwamba ni dini tatu tu ndizo zinazoruhusiwa kuwepo kwenye eneo hilo na kwamba wanakusudia “kuwang’oa Mashahidi wa Yehova.”

Eneo la Luhansk

Mji wa Antratsyt, Mtaa wa 4 Komunarska.

ANTRATSYT—Jumba la Ufalme latekwa na raia.

 • Mara mbili katika mwezi wa Septemba 2014, watu wasiojulikana walivamia Jumba la Ufalme. Waliiba vifaa vya kielektroni na kuandika ukutani maneno, “Orthodox Cossacks!” (Waothodoksi wa jamii ya Cossack)

 • Septemba 25, 2014, kituo cha televisheni katika eneo hilo kiliripoti kwamba Majumba ya Ufalme ya Mashahidi wa Yehova yametekwa na kutumiwa kwa makusudi mengine, kama vile shule za chekechea.

 • Mei 2015 Jumba hilo lilirudishwa kwa Mashahidi wa Yehova.

Mji wa Rovenky, Mtaa wa 84-A Dzerzhynskoho.

ROVENKY—Jumba la Ufalme latekwa na kikosi chenye silaha.

 • Septemba 23, 2014, wanaume wenye silaha kutoka kikosi cha Mt. George wavamia Jumba la Ufalme na kuamuru Mashahidi wasirudi tena. Wameligeuza kuwa kambi yao.

 • Agosti 2015 Jumba hilo lilirudishwa kwa Mashahidi wa Yehova.

PEREVALSK—Jumba la Ufalme latekwa na kikosi chenye silaha.

 • Novemba 5, 2014, wanaume wenye silaha chini ya uongozi wa Mkuu wa Ofisi ya Kamanda wa Jeshi waliingia katika Jumba na kutangaza kwamba wanaliteka jengo hilo na kulitumia kama chumba cha kulia chakula. Msaidizi wake alisema hivi: “Mashahidi wa Yehova wamefikia mwisho wao.” Kisha akawaambia Mashahidi kwamba hawatashiriki tena katika utendaji wao wa kidini.

Mji wa Krasnyi Luch, Mtaa wa 37 Radianska.

KRASNYI LUCH—Jumba la Ufalme latekwa na kikosi chenye silaha.

 • Desemba 5, 2014, wanaume wenye silaha wavamia Jumba la Ufalme. Waliweka jengo chini ya ulinzi mkali na kuegesha magari ya kijeshi katika ua wa jengo hilo.

BRIANKA—Jumba la Ufalme latekwa na kikosi chenye silaha.

 • Machi 26, 2015, wanaume wenye silaha wavamia Jumba la Ufalme. Wachukua fanicha zote na badala ya kibao cha Jumba la Ufalme wakaweka kibao chenye maneno, “The Almighty Don Host.” (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Don)