“Hukumu juu ya tendo baya isipotekelezwa, watu huendelea kutenda mabaya.” Methali hiyo inathibitika kuwa kweli nchini Ukrainia, ambako Mashahidi wengi wa Yehova wanaendelea kutendewa matendo ya uhalifu kwa sababu ya chuki. Mashahidi wa Yehova wanafurahi kwamba serikali ya Ukrainia imewaruhusu kuwa na uhuru wa ibada, hata hivyo wanaishi kwa hofu kwa sababu visa vya kutendewa vibaya kwa sababu ya chuki vinaongezeka, na wenye mamlaka hawachukui hatua yoyote dhidi ya wanaohusika na uhalifu huo.

Visa vya Kushambuliwa Vinaongezeka

Tangu 2008, kumekuwa na visa 64 ambapo Mashahidi wa Yehova wamepigwa na kutendewa vibaya nchini Ukrainia wanapokuwa katika shughuli zao za kidini au wanapomaliza ibada. Mashambulizi 16 kati ya hayo yalifanywa na makasisi wa Kanisa la Orthodox.

Tangu 2008 hadi 2013 kumekuwa pia na visa 190 vya kuharibu Majumba ya Ufalme na wahalifu walijaribu kuyateketeza majengo hayo mara 13. Kati ya mwaka wa 2012 na 2013, vitendo vya kuharibu Majumba ya Ufalme vimeongezeka maradufu ikilinganishwa na miaka minne iliyotangulia.

Pia, mashambulizi hayo yanazidi kuwa mabaya. Katika 2012, Majumba mawili ya Ufalme katika Eneo la Donetsk yaliteketezwa kabisa. Mwaka wa 2013, visa viwili vya kuwashambulia Mashahidi vilisababisha majeraha mabaya kiasi cha kwamba walioshambuliwa walilazwa hospitalini kwa muda mrefu.

Mashahidi wametafuta ulinzi kutoka kwa wenye mamlaka lakini hawajapata msaada kwa sababu wenye mamlaka hawachukui hatua ya haraka ili kuchunguza visa hivyo na kuchukua hatua ifaayo dhidi ya wahalifu hao.

Kutochukua Hatua kwa Wenye Mamlaka

Jumba la Ufalme lililoteketezwa kwa moto na kuharibiwa huko Horlivka, Eneo la Donetsk, Juni 5, 2014

Uharibifu wa Mali. Polisi hawachukui hatua yoyote au hawatendi haraka wanapopata ripoti kuhusu visa hivyo. Wanapojulishwa kuhusu tendo la uhalifu, mara nyingi wenye mamlaka hawachukui hatua au wanachelewa kufanya hivyo. Hata hatua ya kisheria inapochukuliwa, viongozi wa mashtaka hawawachukulii hatua wahusika au mahakama hazitoi adhabu inayofaa. Tangu 2008 hadi 2012, mamlaka hazijawahukumu waliohusika kuwa na hatia ya uhalifu katika visa vyote 111 vya uharibifu wa mali.

Kupigwa. Mara nyingi Polisi hawafanyi uchunguzi wowote mtu anapopigwa wala hawashughuliki kuwatafuta wahalifu hao. Kesi inapoanzishwa mahakamani, wenye mamlaka hawawashtaki wala kuwapa wahusika adhabu yoyote. Mahakama zinapowaadhibu wahusika, wanatoa adhabu ndogo isiyolingana na uhalifu uliotekelezwa kwa madai ya kwamba mashambulizi hayo si uhalifu unaosababishwa na chuki.

Hali hiyo ya kutochukuliwa hatua imefanya wahalifu waendeleze vitendo vya jeuri

Kupigwa kwa Oleksandr Tretiak

Oleksandr Tretiak

Kisa kibaya zaidi kilitokea Novemba 26, 2013, Oleksandr Tretiak, Shahidi mwenye umri wa miaka 41 aliyevamiwa alipokuwa akirudi nyumbani baada ya ibada. Watu watatu walimpiga vibaya sana Bw. Tretiak kwa muda wa zaidi ya dakika 20. Aliripoti kwamba waliompiga ni Ruslan Ivanov; Anatoliy Dovhan, luteni kanali wa polisi aliyestaafu; na Evheniy Ihlinskiy, mkwe wa Dovhan ambaye ni polisi wa barabarani. Bw. Tretiak alifaulu kutoroka na akapelekwa hospitalini akiwa na majeraha mabaya sana, yaliyotia ndani vidonda na michubuko, majeraha kichwani na pua iliyovunjika.

Licha ya hali yake, aliyechunguza kesi hiyo alisema kwamba watu watatu “wasiojulikana” walimsababishia majeraha “madogo tu.” Baada ya kulazwa hospitalini kwa wiki mbili, Bw. Tretiak aliambiwa arudi nyumbani kwa sababu ikiwa angeendelea kubaki hospitalini, wenye mamlaka wangelazimika kushughulikia kisa hicho kama tendo la uhalifu. Majeraha mabaya aliyopata yalifanya arudishwe hospitalini siku iliyofuata tu. Kwa ujumla, alilazwa siku 23.

Hivi majuzi, Ruslan Ivanov ambaye ni mmoja wa waliompiga alifikishwa mahakamani, lakini baadaye alitoroka. Bw. Tretiak anahofia kwamba huenda waliompiga watamshambulia tena. Anasema hivi: “Nina hakika kwamba walionipiga wanaichukia dini ya Mashahidi wa Yehova na walitaka kuniua.”

Je, Wenye Mamlaka Watachukua Hatua?

Ukrainia ni nchi yenye Mashahidi zaidi ya 150,000 wa Yehova ambao wameabudu kwa uhuru kwa miaka mingi na maofisa wamewasaidia kukabiliana na hali ngumu wakati uliopita. Mashahidi wanatumaini kwamba maofisa nchini Ukrainia watafanya uchunguzi unaofaa kuhusu vitendo hivyo vya uhalifu na kuwachukulia hatua wahusika ili wasiendelee na uhalifu huo bila kuhukumiwa.