Mnamo Septemba 26, 2012, Mahakama Kuu ya Ukrainia ilizuia jaribio lisilo la haki la watu waliotaka kunyakua sehemu kubwa ya uwanja ambao ofisi ya tawi ya Mashahidi Yehova nchini Ukrainia imejengwa.

Mashahidi walinunua kihalali uwanja huo katika mwaka wa 1998. Hata hivyo, katika mwaka wa 2008, mmiliki wa awali aliuzia shirika la Sport Development Center LLC (SDC) uwanja huohuo. Nchini Ukrainia kitendo kama hicho kinajulikana kama uvamizi wa viwanja.

Mahakama ya biashara iliamua kwamba mkataba wa kuuzia SDC uwanja huo ulikuwa halali, na rufani za mashahidi zilitupiliwa mbali.

Hata hivyo, haki ilishinda. Mnamo Desemba 2011, mahakama kuu ya biashara ilitoa uamuzi wa kuunga mkono Mashahidi na katika Aprili 2012 walitupilia mbali rufaa ya SDC. Hilo lilithibitisha kwamba uwanja huo ni mali halali ya Mashahidi wa Yehova. Miezi mitatu baadaye mahakama ya rufani ya biashara katika mji wa Lviv ilibatilisha uamuzi usio wa haki wa mahakama ya biashara uliosema SDC ndio wamiliki wa uwanja huo.

Katika jaribio la mwisho la kudai umiliki, SDC ilikata rufani dhidi ya uamuzi wa Aprili kwenye Mahakama Kuu ya Ukrainia. Hata hivyo, Septemba 26, mahakama ilitoa uamuzi upesi wa kutupilia mbali rufani hiyo, na hatimaye kesi hiyo ikatatuliwa kabisa.

Iwapo unyakuzi huo wa ardhi ungefaulu, Mashahidi wa Yehova wangepoteza jengo lao la ofisi na sehemu kubwa ya uwanja, na hilo lingezuia kazi zinazofanywa katika makao makuu ya Mashahidi wa Yehova nchini Ukrainia.