Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

FEBRUARI 5, 2015
UFARANSA

Mahakama ya Juu Zaidi Nchini Ufaransa Yakomesha Ubaguzi

Mahakama ya Juu Zaidi Nchini Ufaransa Yakomesha Ubaguzi

Baada ya kukutana nawe, nina furaha na hata ninaimba. Ziara yako inanifariji, na kujifunza Biblia kunanipa kusudi maishani.

Nilitaka kuwashukuru kwa mipango ya kisheria, kiserikali, na ya kiroho mliyofanya ili kuwe na maandalizi haya.

Maandalizi haya ni jibu la sala zangu.

Maelezo hayo kutoka kwa wafungwa nchini Ufaransa yanaonyesha uthamini wao kwa msaada wa kiroho uliotolewa na mhudumu wa Mashahidi wa Yehova.

Oktoba 16, 2013, Mahakama Kuu ya Utawala nchini Ufaransa ilitoa uamuzi uliokomesha ubaguzi dhidi ya Mashahidi wa Yehova nchini humo. Uamuzi huo unawaruhusu Mashahidi wa Yehova kutembelea magereza wakiwa wahudumu wa kidini waliosajiliwa kisheria ili kutoa msaada wa kiroho kwa wafungwa wanaoomba kutembelewa. *

Wahudumu Mashahidi Wanyimwa Usajili

Kwa miaka mingi, wenye mamlaka katika magereza waliwaruhusu wahudumu Mashahidi kutembelea na kutoa mwongozo na ushauri wa kiroho kwa wafungwa licha ya kutokuwa na cheti kilichowatambulisha rasmi kuwa wahudumu wa kidini. Hilo lilibadilika mwaka wa 1995 baada ya Tume ya Bunge kutoa ripoti yenye utata iliyokuwa na orodha ya madhehebu yaliyodhaniwa kuwa hatari kutia ndani Mashahidi wa Yehova. Hilo liliharibu sifa nzuri ya Mashahidi na pia lilifanya waanze kubaguliwa. Baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa ni magereza.

Ingawa ripoti za bunge hazionwi kuwa sheria, baadhi ya wenye mamlaka katika magereza walitumia ripoti ya 1995 kama msingi wa kuwanyima Mashahidi ruhusa ya kuwatembelea wafungwa walioomba kusaidiwa kiroho. Shahidi angeruhusiwa kumtembelea mfungwa kama raia lakini si kama mhudumu wa kidini aliyewekwa rasmi. Hakuruhusiwa kuja na Biblia au chapisho lolote la kidini. Ziara zote zilifanywa katika chumba cha watu wote ambapo hapakufaa mazungumzo ya kiroho. Shahidi mmoja alisema mazingira katika chumba cha wageni “yalikuwa kama katika kituo cha treni kutia ndani na kelele zake.” Katika baadhi ya magereza, wafungwa walivuliwa nguo na kupekuliwa baada ya ziara eti kwa sababu mhudumu aliyewatembelea hakuwa amesajiliwa na serikali.

Katika jitihada za kutafuta haki sawa na wahudumu waliosajiliwa wa dini nyingine, Mashahidi wa Yehova walianza kutafuta usajili kupitia mamlaka za magereza ya Ufaransa mwaka wa 2003. Maombi yote yalikataliwa. Mashahidi walikata rufani kwa mamlaka za juu zaidi na bado wakakatiliwa. Sababu rasmi iliyotolewa na Wizara ya Sheria ya Ufaransa ya kukataa kuwasajili Mashahidi ni kwamba Mashahidi wa Yehova hawako kwenye orodha ya dini zinazoruhusiwa kutembelea magereza. Pia, Wizara hiyo ilisema kwamba kumpa kibali Shahidi wa Yehova kungefanya dini nyingine ndogondogo kutaka pia vibali vya kutembelea magereza. Baada ya kushindwa kutatua suala hilo kupitia Wizara ya Sheria, Mashahidi hawakuwa na la kufanya ila kupeleka suala hilo mahakamani.

Serikali Yakataa Kukomesha Ubaguzi

Mwaka wa 2006, Mashahidi wa Yehova walianzisha kesi mahakamani kupinga uamuzi wa Wizara ya Sheria wa kukataza Mashahidi wapewe vibali vya kuwa wahudumu wa kidini waliosajiliwa. Mahakama zote za Utawala na za Rufani zilizosikiliza kesi hiyo nchini Ufaransa ziliamua kwamba kuwanyima Mashahidi kibali ni kinyume cha sheria. Zaidi ya hilo, mwaka wa 2010, Mamlaka Kuu ya Ufaransa ya Kupinga Ubaguzi na Kutetea Usawa ilipinga uamuzi huo wa Wizara na kupendekeza Waziri wa Sheria akomeshe ubaguzi huo.

Serikali ya Ufaransa ilipuuza onyo hilo na hukumu za mahakama, na zaidi ya hayo ikakata rufani kwa Baraza la Nchi, mahakama ya juu zaidi nchini Ufaransa.

Uamuzi wa Kihistoria Watetea Mashahidi wa Yehova

Hatimaye, mwaka wa 2013, kesi za Mashahidi zilipelekwa kwenye Baraza la Nchi, ambapo ziliunganishwa na nyingine tisa ili zichunguzwe pamoja. Katika uamuzi wake wa Oktoba 16, 2013, Mahakama hiyo ilipinga rufani zilizowasilishwa na serikali ya Ufaransa. Ilieleza kwamba ili kuheshimu haki za mfungwa, Mamlaka ya Magereza inapaswa, “kusajili idadi ya kutosha ya wahudumu wa kidini mara tu ombi linapotolewa, wakizingatia tu usalama na utaratibu mzuri wa gereza husika.” Zaidi ya hilo, ikirejelea Katiba ya Ufaransa na Mkataba wa Ulaya wa Haki za Kibinadamu, Baraza la Nchi lilisema kwamba “wafungwa wana uhuru wa maoni, wa dhamiri na dini na kwamba wanaweza kuabudu katika dini yoyote wapendayo.” Kwa sababu ya uamuzi huo, kufikia sasa, vyeti 105 vya wahudumu vimeidhinishwa nchini Ufaransa, kutia ndani maeneo ya mbali yaliyo chini ya utawala wa Ufaransa, na kufanya iwezekane kwa wafungwa hao kupata ziara za uchungaji kutoka kwa Mashahidi wa Yehova.

Januari 2014, Mamlaka ya Magereza ya Ufaransa ilimteua Jean-Marc Fourcault, kuwa mhudumu wa kitaifa wa Mashahidi wa Yehova. Katika cheo hicho, Bw. Fourcault ana kibali cha kutembelea magereza yote ya Ufaransa. Ameteuliwa pia kuwa mwakilishi wa Mashahidi wa Yehova kwenye Mamlaka ya Magereza. Bw. Fourcault anaeleza hivi: “Kuanzia sasa na kuendelea, Mashahidi wa Yehova wataweza kukutana na wafungwa wakiwa peke yao au katika maeneo mengine yanayofaa, kama katika chumba cha mfungwa, kama tu ilivyo kwa wawakilishi wa dini nyingine zilizo na kibali.”

Uamuzi huu ni wa muhimu sana katika uhuru wa kidini nchini Ufaransa. Unaruhusu wafungwa kuwa na haki ya kuabudu katika dini wapendayo na kutembelewa na mhudumu yeyote wapendaye. Mashahidi wa Yehova wanashukuru kwamba mahakama za Ufaransa zimekomesha ubaguzi huo, na kupiga hatua katika kutambua dini ya Mashahidi wa Yehova nchini Ufaransa.

^ fu. 6 Baadhi ya wafungwa wanakuwa Mashahidi wa Yehova baada ya kukutana na Mashahidi wakiwa gerezani. Wengine huenda walikuwa wamekutana na Mashahidi awali au walilelewa katika familia za Mashahidi kabla ya kujiingiza katika uhalifu na sasa wangependa kurudi kutanikoni. Hata iwe ni sababu gani iliyofanya wafungwa waombe kutembelewa na Mashahidi wa Yehova gerezani, wafungwa hao wana haki sawa ya uhuru wa kidini kama wafungwa wa imani nyingine.